Ulaya yaachana na hewa ukaa, nchi changa ziko njia panda

04Jul 2019
Jenifer Julius
BONN
Nipashe
Ulaya yaachana na hewa ukaa, nchi changa ziko njia panda
  • Zataka zisaidiwe kifedha kujinusuru

MKUTANO  mdogo wa hali ya mabadiliko ya tabianchi  umemalizika wiki iliyopita jijini Bonn, Ujerumani na tayari nchi zilizoendelea 17 zimeingia makubaliano ya kuondoa kabisa uzalishaji wa hewa chafu inayoongeza joto duniani.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mkurugezi wa Kitengo cha Wataalamu wa Nishati na Hali ya Hewa  kutoka Umoja wa Mataifa, Richard  Black,  alipofanya mkutano na waandishi wa habari.

Akitaja nchi ambazo zimeshaanza utekelezaji huo, Richard alisema ni Bhutan and Suriname tayari zinanyonya mara mbili zaidi ya oksjeni inayozalishwa huku Norway na Sweden zimejiwekea mikakati ya kisheria ya  kupunguza hewa ya ukaa  mpango mingine kadha  ipo njiani.

“Inaleta faraja kuona kuwa nchi hizo na mikoa yake   11 pamoja na majiji 23 yana mipango ya kuondoa kabisa uzalishaji wa hewa ukaa “, alisema Black  akiwa na uso uliojaa matumaini.

JITIHADA ZA UINGEREZA

Uingereza imeshaanza utekelezaji wa kuzuia uzalishaji wa hewa ukaa kwa asilimia 100 kwa kuachana na  matumizi ya makaa ya mawe katika shughuli mbalimbali za viwandani, majumbani na maeneo mengine yaliyokuwa yanategemea nishati hiyo.

Ni kwa mujibu wa  Archieng Young, Mkurugenzi wa Hali ya Hewa na Nishati nchini Uingereza. Akizungumza katika mkutano huo na wanahabari alisema wakazi wa nchi yake wameshaanza kusahau matumizi ya makaa ya mawe na wamejikita kwenye umeme wa vyanzo vingine kwa matumizi ya nyumbani.

“Mwanzoni utekekelezaji ulikuwa wa tabu sana, ilikuwa vigumu kuwashawishi wananchi kuacha kutumia makaa ya mawe, lakini serikali iliongeza nguvu ya uhamasishaji na uelimishaji na sasa tupo katika nafasi nzuri”, alisema Young.

CHANGAMOTO

Ingawa mataifa yamekubaliana kuzuia uzalishaji wa hewa ukaa  katika nchi zao, matokeo yanaweza kutofautiana kutokana tofauti za kiitikadi na kiuongozi anaeleza  Black.

Moja ya sababu aliyoitaja ni tofauti ya sheria na taratibu za nchi husika, akihusisha vipaumbele ilivyojiwekea, mfano wakati Uingereza imeshapitisha sheria ya kutotumia makaa ya mawe, wakati  Sweden ndio inatengeneza muswada wa kuzuia uzalishaji wa hewa hiyo.

Sababu ya pili ni shughuli za kiuchumi kutegemea nishati ya makaa , ukizingatia kuwa nchi nyingi zilizoendelea zinategemea viwanda ambavyo ndiyo chanzo kikuu cha hewa ya kabon  kwa hivyo kunahitajika teknolojia mbadala  kuzuia hewa hiyo kuzalishwa.

Anataja sababu ya tatu kuwa ni utofauti wa sera baina ya nchi moja hadi nyingine, wakati será ya nchi moja imeipa kipaumbele sayansi na teknolojia katika kuzuia uzalishwaji wa hewa chafu mfano matumizi ya nishati jadidifu, nchi nyingine mipango imeegemea kwenye kupanda miti mingi ili kusafisha hewa.

NCHI ZINAZOENDELEA

Kwa upande wa nchi zinazoendelea, Black alisema zitakubali kuingia makubaliano ya kumaliza kabisa uzalishwaji wa kaboni ikiwa tu kutakuwa na uhakika wa kupewa msaada wa kifedha kusaidia miradi itakayopelekea kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Hoja hii ilijikita kwenye sababu kuwa nchi zinazoendelea bado hazijasimama imara kuzuia uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 100 kwa kuwa zinatakiwa kutumia nguvu nyingi kujiendeleza ili zikue kiuchumi.

“Ili nchi izuie uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 100 na kufikia lengo la kiwango cha sifuri -‘zero net’ inahitaji kuzuia miradi mingi ya kimaendeleao kama vile kutumia makaa ya mawe, gesi na mafuta, vitu ambavyo nchi zinazoendelea zinavihitaji kwa sasa ili kupiga hatua kimaendeleo”, alisema Michael Richard, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, uliomalizika Juni 27, mwaka huu huko Bonn, Ujerumani.

Naye mmoja wa wajumbe kutoka Japan, Joeng Chin, alisema  kama nchi zinazoendelea zitapata fedha hizo ni vyema kuwekeza katika miradi itakayosaidia kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile nishati jadidifu na miradi ya kaboni.

 

Mjumbe mwingine kutoka nchi zinazoendelea ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema haoni sababu ya mataifa yenye uchumi unaokua kujikita katika kuondoa kabisa kuzalisha  hewa ya kaboni kwa sababu zipo nyuma kimaendeleo na zinahitaji nishati inayotokana na nguvu za makaa ya mawe,  mafuta na gesi ili kuendelea .

“Unapoongelea suala la kuondoa uzalishaji wa hewa hii kwa nchi zinazoendelea nadhani halitawezekana kwa sasa, Ina maana ziachane na biashara kama vile ya mafuta, makaa ya mawe na  gesi  ambayo ndio chanzo cha nishati kwa maendeleo yao. Mimi nadhani hili tuwaachie nchi zilizoendelea kwa sababu wenzetu wapo vizuri kiuchumi, sisi tuangalie kwanza maendeleo ya nchi zetu labda kama tutapatiwa fedha za kutosha,” alisema .

Lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha kuwa joto la dunia haliongezeki kufikia nyuzi joto 1.5 kama ilivyotabiriwa katika ripoti ya jopo la wanasayansi  lijulikanalo kama IPCC lililofanyia uchunguzi wa kisayansi mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi, ukizingatia kuwa kwa sasa nyuzi joto ya dunia imefikia moja.

Mkutano mkubwa wa hali ya athari ya mabadiliko ya tabianchi ujulikanao kama Cop  25, unatarajiwa kufanyika Novemba nchini Chile ambapo hoja mbalimbali zitajadiliwa zikiwamo ambazo hazijapatiwa ufumbuzi katika mkutano uliomalizika Bonn, ikiwamo jinsi ya kuzisaidia nchi zinazoendelea katika kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi chini ya Makubaliano ya Paris.

 

TANZANIA JE?

Wakati jitihada za kuachana na makaa ya mawe, gesi na nishati ya mafuta Tanzania inajizatiti kuwekeza kwenye uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi inayopatikana mikoa ya Mtwara na Lindi.

Aidha, inaandaa mikakati ya kutumia makaa ya mawe ya Mchuchuma na Ngaka, ili kupata umeme wa kutosha wa kuendesha uchumi wa viwanda.

Mapema mwaka huu, serikali ilitangaza nia ya uwekezaji wa kimkakati wa uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe utakaofanywa na Shirika la Mendeleo ya Taifa (NDC) ili kuiwezesha Tanzania kuwa na umeme wa kutosha wa viwanda na matumizi ya kijamii.

Katika mazingira hayo ya kufikia uzalishaji wa kaboni kwa kiwango cha sifuri, taifa lisipopata fedha na teknolojia mbadala pengine kama wataalam walivyosema ni vigumu kuzizuia nchi zinazoendelea kama Tanzania kutumia vyanzo hivyo kupata umeme.

Makaa ya mawe, gesi na mafuta vinapochakatwa kupata nishati huzalisha kiwango kikubwa cha hewa ukaa, inayodhoofisha utando wa ozoni na kuongeza kiwango cha joto duniani hivyo kuleta athari za mabadiliko ya tabianchi zaidi.