Ulazimishaji huu sarufi unawakera watumiaji wasanifu wasijitutumue

27Jul 2021
Michael Eneza
Dar es Salaam
Nipashe
Ulazimishaji huu sarufi unawakera watumiaji wasanifu wasijitutumue

JITIHADA za kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika nyanja tofauti za maisha na uchumi kwa jumla zinaendana na juhudi za taasisi zinazohusika na kukua kwa lugha kutoa mwanga pale ambapo kuna hitilafu katika matumizi ya lugha. 

Wadau wakijichagulia vitabu vya Kiswahili katika duka lililoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.: PICHA MTANDAO.

Kwa mfano kupatikana kwa neno pale ambapo hitaji lipo mathalani, ‘mask’ wakati huu wa corona jina lililoibuliwa ni ‘barakoa’. 

Jitihada hizo za kitaasisi kujenga lugha zimewezesha maeneo mengi kupatikana kwa mifumo ya kujieleza ambayo labda ingechukua muda kujijenga yenyewe miongoni mwa watu, au isingekuwapo. 

Hata hivyo, mara nyingi jitihada hizo hazielekei kujaza pengo halisi ila kulijaza kwa lafudhi ya Kiswahili.

Hapo ndipo unazuka utatanishi kuhusu matumizi ya misemo tofauti kama ni Kiswahili sanifu, au ni ‘Kiswahili gani na kuna baadhi ya wataalamu wa Kiswahili wameanza kukosoa baadhi ya matumizi katika lugha ya kawaida kuwa ni mifumo ya kuongea Kiingereza na haifuatani na sarufi ya Kiswahili. 

Tatizo hapo ni kuwa watu wakishaanza kuwasiliana au kuzungumza kwa mfumo fulani unaoeleweka, hakuna anayeweza kuja kama mtaalamu akaanza kuwafundisha kitu kingine.

Ni kwa sababu lugha zinatokana na mifumo ya nasibu hutokea bila kutazamiwa au kuzuka kwa bahati.

Inakuwa kana kwamba wanahitaji kufaulu mtihani wakati sivyo, au waongee Kiswahili kinachofurahisha wataalamu au kundi fulani. 

Wanafunzi wa shule za msingi na zaidi sekondari wanafahamu kitabu kinachoitwa ‘Common Mistakes in English,’ makosa yanayofanywa kila wakati katika kuongea Kiingereza, lakini pengine kwa Kiswahili si rahisi kuwa na kitabu kama hicho.

Yako maeneo kwa uhakika unaweza kusema kuwa ni ‘common mistake,’ ni kosa la kawaida linafanyika katika maongezi, halafu ziko sehemu nyingine ambako ni matumizi ya kawaida na siyo makosa ya kuainishwa kwa njia isiyopingika.

Kwa mfano katika mazungumzo redioni unasikia mwanamuziki akumbushie ‘nyimbo hii’ aliitunga katika mazingira gani.

Ni wazi kuwa umoja ungestahili kutumika hapo, ambao ni ‘wimbo’ badala ya ‘nyimbo’ lakini katika lugha hakuna amri au sheria ni wapi kuna majina au maneno yasiyotofautiana na wingi wake, na ni sehemu ipi tofauti inajitokeza. 

Kwa mfano hakuna wingi kwa wanyama ng’ombe, kuku, mbuzi, kondoo au farasi wanaowataja wanabakia kusema ‘wengi,’ badala ya kubadilisha neno.

Kuku wengi, farasi wengi, lakini siyo kundi hilo tu la majina, kuna ‘nyota’ iwe ni moja au ziwe nyingi au anga nzima bado ni nyota.

Hivyo kuna uwezekano katika Kiswahili kuwa na mazoea ya kupuuza wingi au umoja, mradi tu neno liwe ‘linatamkika,’ na ndiyo huu usemi wa ‘nyimbo hii’ ambao sasa ni kama ‘fashion.’ 

Kuna eneo jingine ambalo haliwezi kuingizwa katika usanifu ila kuonekana katika matumizi ya lugha, hata kama wasanifu wa lugha wataona kama inatumika kwa makosa, kwa maana ya hisia ya kubania ‘pumzi’ katika kujieleza. Dhamira hapo inakuwa ni kupunguza makali ya kitu kinachozungumziwa, au kuainisha (kuweka mkazo wa aina fulani), ingawa inaonekana kubana kujieleza kwa hisia halisi inatokea mara nyingi zaidi.

Kwa mfano ni kawaida kusema ‘naomba’ sukari, wakati unanunua bidhaa hiyo, na hivyo ‘huombi’ ila ni kukwepa kusema ‘lete,’ ‘nipe’ au ‘nataka,’ kwa sababu za ustaarabu na upole ambayo ni sawa na ‘adabu’ kwa Kiswahili, licha ya kuwa ‘kutaka’ sukari dukani siyo ‘kukosa adabu.’

Halafu kuna hisia miongoni mwa ‘wanazuoni’ wa Kiswahili au wasanifu ambazo kimsingi hutokana na jamii inayowazunguka, si kwa maana ya jamii pana ya Watanzania ila jamii finyu kwa mfano ya wakazi wa Kariakoo, au kundi la mtaani ambako mzungumzaji au msanifu, huyo anakuwapo mara kwa mara, na hata iwe familia anakoishi. 

 Kwa mfano mtaalamu mmoja ambaye lafidhi anasema ‘lafudhi’ kwa jinsi ulimi wake ulivyokuwa unasikika redioni ni mkazi wa maeneo ambako watu wa jamii ya Kiarabu ni wengi.  

Anasema kutamka ‘nachukua nafasi hii’ ni kosa, ingekuwa ‘natumia nafasi hii’ suala ambalo halina uhakika kama ni ukosoaji sahihi na pia anadai kuwa ‘nawaambieni’ siyo sahihi ila ‘nakuambieni,’ mwelekeo ambao pia una utata kudai hayo ni matumizi sahihi zaidi ukiwa mbele za watu. 
 
Hapo kuna maeneo mawili ya hisia yanayokinzana, kwanza ni eneo la matumizi ya adabu ukiwa mbele za watu, ambako ‘nachukua nafasi hii’ ina ladha nzuri zaidi ya ‘natumia nafasi hii,’ na kwa upande mwingine ‘nawaambieni’ inakubalika kihisia, kiadabu, wakati ‘nakuambieni’ ina shari ndani yake. Ndiyo maana mara kadhaa baadhi ya wadadisi wanaona kuwa wasanifu wangetafiti matumizi ya lugha na mapana yake, wakaandika kamusi za vina vya matumizi ya maneno, si kupania kuwa viranja wa lugha kuondoa ‘Kiingereza’ katika sarufi, wakati jambo hilo linatokana na matumizi ya kawaida. 

Si uelewa wa Kiingereza, ila ni kweli yako maeneo ambako Kiingereza kilisaidia kufuma na kuunda lugha nyingine nyingi kwa jumla.