Ulinzi na usalama ni wajibu wako nami

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ulinzi na usalama ni wajibu wako nami

MAKUZI ya mwanadamu yanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo majanga na matatizo mengi yaliyogawanyika katika makundi mbalimbali.

Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Ahmed Msangi, picha mtandao

Wakati mwingine, inaaminika binadamu huwa ndiye kisababishi cha kutenda au kutotoa taarifa za haraka, ili kero au changamoto zinazomkabili ziweze kutatuliwa. Miongoni mwa kero na changamoto hizo, ni uhalifu.

Hilo ni tatizo linalosababishwa na mwanadamu ndani ya jamii na kusababisha madhara kwa watu, jamii na taifa kwa ujumla. Ni tatizo linalojenga hofu kwa watu na jamii, jambo linaloifanya jamii kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kwa hofu ya kutendewa uhalifu.

Wananchi wanapaswa kutambua kuwa, suala la kuzuia uhalifu ni jukumu la kila mtu ndani ya jamii. Ili jamii iweze kuepuka madhara ya vitendo vya uhalifu, wananchi hawana budi kushirikiana na Jeshi la Polisi, katika kutekeleza mkakati wa ulinzi jirani unaowawezesha wananchi kujilinda wenyewe, kwa kupeana taarifa zitakazosaidia kuweka makazi yao katika hali ya amani na usalama.

Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Ahmed Msangi, anasema mpango wa ulinzi jirani, ni moja ya mikakati ya kuzuia uhalifu inayotekelezwa na Polisi, kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii, lengo ni kuimarisha usalama wa raia na mali zao waliko.

Hali iliyoko ni kwamba, mkakati huo wa ulinzi jirani unasaidia kuondoa kero za uhalifu wa wizi wa vitu vidogo majumbani na hata wizi wa kuvunja nyumba, pale wahusika wanapokuwa hawapo.

Pia, ni mkakati unaohamasisha watu kujenga utamaduni wa kupeana taarifa na jirani zao, kuwaangalizia mazingira ya nyumba yao, ili wahalifu wasitumie fursa ya wao kutokuwapo na kutekeleza azima yao ya kutenda uhalifu.

“Jamii inapaswa kuelewa kwamba mpango wa ulinzi jirani si wa Jeshi la Polisi, bali ni wa jamii nzima ambayo inachukia uhalifu, hivyo wanaamua kuanzisha mtandao wao wa ulinzi kwa lengo la kujihakikishia usalama wao na mali zao,” anasema DCP Msangi.

Mkakati wa ulinzi jirani, ni mpango shirikishi wa ulinzi ndani ya jamii, unaojumuisha watu na nyumba jirani, kwa ajili ya kuimarisha usalama, kwa kutengeneza mtandao wa mawasiliano baina yao, kupashana taarifa za vitendo vya uhalifu, lengo ni kutafuta ufumbuzi, ili waweze kuwa salama.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi, wana jukumu la kufanya mpango huo wa ulinzi jirani kuwa endelevu. Kufanya hivyo, kunaelezwa kutasaidia upatikanaji taarifa za vitendo vya uhalifu vinavyotokea majumbani, ikiwamo vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Ni ukweli usio na shaka kuwa, wananchi wanapoamua kuchukua hatua ya kujihakikishia usalama wao na mali zao bila ya kuvunja sheria, vitendo vya uhalifu hupungua ndani ya jamii, kwa kuwa wahalifu wanatoka katika jamii yao.

Wengi wao ni watoto na jirani zao, jamaa, hivyo ni rahisi kuwabaini, kuwafichua na kuwachukulia hatua za kisheria na kuacha tabia ya kulindana.

Jukumu la Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa mkakati huu wa ulinzi jirani, ni kuchangia utaalamu na ushauri kwa vikundi hivyo vya ulinzi, juu ya masuala ya ulinzi na usalama, kwa kutumia askari kata ambaye ndiye mtaalamu wa usalama katika kata na ana jukumu la kuhakikisha kero za kiusalama zinatatuliwa kwa wakati.

Jamii mbalimbali zinapaswa kujiunga na kushirikiana katika kupanga mipango na mikakati ya kujihakikishia ulinzi na usalama, kama wanavyopanga mipango mingine ya kijamii ndani ya jamii zao, ili kujihakikishia huduma mbalimbali katika jamii.

Ushirikiano huo wa wananchi wenyewe na Jeshi la Polisi, ndio msingi wa kufanikiwa kwa mpango mkakati wa ulinzi jirani.

Viongozi wa serikali ya mtaa na shehia kwa Zanzibar, kijiji pamoja na kitongoji, wao kama viongozi wa wananchi wenye wajibu wa kuhakikisha katika maeneo yao, kunakuwapo na hali ya amani na utulivu katika maeneo yao, wanawajibika kuwahamasisha wananchi suala zima la kuanzisha vikundi vya ulinzi jirani ili kuepukana na vitendo vya uhalifu.

Imetolewa na:Kitengo cha Uhusiano,Makao Makuu ya Polisi,Dar es Salaam.

Habari Kubwa