Umasikini umepungua nchini, umri wa Mtanzania kuishi umeongezeka zaidi

11Jan 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Umasikini umepungua nchini, umri wa Mtanzania kuishi umeongezeka zaidi
  • Dk. Kazungu ataja serikali ilikokanyaga, inakoelekea

MKAKATI wa serikali iliyoko madarakani hivi sasa ni kwamba inadhamiria kuijenga Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati kufikia mwaka 2025, inahitaji mkakati mzuri wa kuoanisha sera za kiuchumi na kijamii.

Wakulima wakiwa shambani. Kilimo ndio nyenzo kuu ya uchumi nchini. PICHA MTANDAO.

Katika mtazamo huo wa jumla, Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), imetoa mtazamo wake kuoanisha mambo hayo,
ESRF inasema katika mabadiliko yake kiuchumi, kunatakiwa kuboreshwa hali ya binadamu, mahitaji ya huduma za jamii na kwa watu wanaoongezeka, na lazima kupangwe na kuwekwa taratibu bora za kuimarisha tija ya kiuchumi kwa umma.

Mtiririko wa kijamii, unaonyesha idadi ya Watanzania inaongezeka kwa haraka na wanahama kutoka vijijini, kwenda mijini kunafungua milango kwa fursa nyingi.

Asasi hiyo inaeleza kuwa, ubunifu uliofanywa wa sera za kijamii na kiuchumi, inaweza kutanua mawazo katika mtawanyiko wa watu kitaifa, ili kusukuma mageuzi ya kiuchumi.

Novemba 28 mwaka huu, Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu ya Tanzania (THDR) ya mwaka 2017, imetolewa kwa mara ya pili kitaifa yenye mada kuu: ‘Sera ya kijamii katika Muktadha wa Mageuzi ya Kiuchumi Nchini Tanzania.’

Ni ripoti hiyo ilyoandaliwa na ESRF) kwa ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP),mada yake ikisudia kuendeleza dhana zilizoibuliwa na Ripoti ya Kwanza ya Mwaka 2014.

Hivi karibuni mkakati wa maeneo ya kiuchumi nchini, umeweka mkazo kwenye umuhimu wa mageuzi ya kiuchumi katika kupunguza na kuleta ustawi.

Wakati serikali inafanyia kazi ripoti ya THDR ya mwaka 2014, ikijikita katika dhana kuu kwamba, mageuzi ya kiuchumi yalete maendeleo ya binadamu, mchakato wake ni lazima uende sambamba na upatikanaji wa ajira, ongezeko la kipato na utoaji huduma za jamii.

Hivyo, ripoti ya mwaka 2017 imelenga kuendeleza fikra za ripoti tangulizi katika kuchambua nafasi ya sera ya kijamii na utoaji wa huduma za kijamii katika mchakato endelevu wa mageuzi ya kiuchumi nchini.

Maudhui yake

Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk.Tausi Kida, anasema miongoni mwa matokeo muhimu yaliyopo kwenye ripoti hiyo, ni pamoja na kuonyesha kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya binadamu, yanayothibitishwa kupitia ongezeko la kipimo cha Maendeleo ya Binadamu kwa asilimia 43.1, kutoka mwaka 1985 hadi 2015.

“Kwa kuzingatia alama za mwaka 2015, Tanzania imepanda daraja, ambalo ni zaidi ya wastani wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara,”anasema Dk. Tausi.

Hata hivyo, anasema kwa ujumla Tanzania bado inabaki kwenye kundi la nchi zenye kiwango kidogo cha maendeleo ya binadamu, ikishika nafasi ya 151 kati ya nchi 188 duniani.

UMASIKINI WAPUNGUA

Aidha, ripoti hiyo imeonyesha kwamba kiwango cha umaskini kwa kutumia kipimo cha umaskini wa vigezo mbalimbali (MPI), umaskini umepungua kutoka kiwango cha asilimia 64 mwaka 2010 hadi asilimia 47.4 mwaka 2015.

“Umaskini uliokithiri umeshuka kutoka asilimia 31.3 mwaka 2010 hadi asilimia 17.7 mwaka 2015 na mafanikio haya yametokana na ukweli kwamba Tanzania imeweza kufanya maboresho katika viashiria vyote vya MPI katika kipindi hiki,” anasema Dk. Kida

Kwa mujibu wa utafiti huo, ni mafanikio yaliyosababishwa kuboreka maisha ya Mtanzania katika maeneo mbalimbali, hususan sekta za elimu na afya.

Pia, anataja ongezeko kubwa la upatikanaji wa huduma za umeme miongoni mwa wananchi wake.

Mkurugenzi huyo anasema, ongezeko la upatikanaji umeme na miliki ya rasilimali, zikiwemo simu za mkononi, redio na pikipiki ni hoja muhimu za kuelezea kushuka kwa umaskini.

Anasema mwelekeo huo unaendana na malengo ya Taifa, kama yalivyoonyeshwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano, unaolenga kupunguza umaskini kwa asilimia 34.4, kufikia mwaka 2020/21 na hatimaye asilimia 29.2 mwaka 2025/26.

Pia, anasema tofauti za maendeleo kimkoa, zimeendelea kuwapo, akitoa mfano wa asilimia 66 ya wakazi wa mkoa Rukwa inaishi katika umaskini kwa kipimo cha asilimia 12 ya watu mkoa wa Dar es salaam.

Visiwani Zanzibar, anasema matokeo ya utafiti yanaonyesha uwiano wa kipimo cha umaskini umeshuka kutoka asilimia 43.3 ua kipimo hicho cha MPI mwaka 2010 hadi asilimia 26.3 mwaka 2015.

Vivyo hivyo, Dk. Kida anasema umaskini uliokithiri nao umeshuka kwa kiwango cha nusu kutoka asilimia 16.6 hadi 8.5 kwa kipindi hicho.

AFYA JE?

Ripoti inaonyesha kwa kipindi cha mwaka 2002 hadi 2012, umri wa kuishi umengezeka kwa takriban miaka tisa zaidi kwa wanaume kutoka miaka 51 hadi 60 na wanawake imezidi kwa miaka 13, kutoka miaka 51 hadi 64.

Majumuisho katika wastani wa umri wa kuishi kwa Tanzania Bara ni miaka 61.7 na miaka 65.7 kwa Zanzibar. Ni ongezeko linalochangiwa na uboreshaji masuala mbalimbali kama vile kupungua vifo vya watoto na vifo vitokanavyo na maradhi ya Uklimwi, maboresho ya lishe na usafi, ongezeko la upatikanaji maji safi ya kunywa, uzazi wa mpango na utoaji chanjo.

Hata hivyo, Dk. Kida anasema ripoti imeonyesha Tanzania bado ina safari ndefu kuelekea viwango vya juu vya maendeleo ya binadamu yanayokusudiwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Kauli ya serikali

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo kwa niaba ya Waziri Dk. Phillip Mpango, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Khatib Kazungu, anasema takwimu za karibuni zinaonyesha matokeo ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali.

Dk. Kazungu anasema, ni jitihada zinazogusa utoaji huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi, wastani wa umri wa Mtanzania kimeongezeka kutoka miaka 62.2 mwaka 2013 hadi miaka 64.4 mwaka 2017.

“Matazamio ya serikali ni kuendelea kuboresha huduma za jamii, ili kwamba kiwango cha wastani wa maisha ya Mtanzania yawe ni miaka 66.1 ifikapo mwaka 2020,” anasema.

Aidha, anasema Mpango wa Taifa wa Pili wa Maendeleo, umelenga katika kufanya mageuzi ya kiuchumi, ujenzi wa viwanda na kuinua maisha ya binadamu.

Anasema, mpango huo una vipaumbele vinne ambavyo ni kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa viwanda; mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; kufungamanisha maendeleo ya viwanda na binadamu; na kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango.

“Ukivitazama vipaumbele hivi vinne vya mpango huu, utagundua kuwa tayari vimezingatia dhana inayoibuliwa na ripoti hii na Tanzania kama mwanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa, imeridhia Ajenda ya Maendeleo ya Dunia ya Mwaka 2030 inayoeleza kutoa msisitizo wa kutoachwa mtu yeyote nyuma katika safari ya maendeleo,” anasema Dk. Kazungu

Anasema, kwa kuzingatia umuhimu huo wa kujenga uchumi jumuishi, kutokuacha mtu yeyote nyuma katika mchakato wa maendeleo na kufungamanisha maendeleo ya watu na mageuzi ya uchumi, serikali imetoa umuhimu mkubwa katika utoaji huduma za jamii, ili kuinua hali za watu wake.

“Utoaji huu wa huduma za jamii, unaenda sambamba na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na ujenzi wa viwanda unaoendelea nchini mwetu kwa sasa,” anaongeza.

Wito wa Naibu Mtendaji Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na Mipango, ni kwamba wadau hao wasiishie kwenye utafiti, bali waendeleze utafiti na uandaaji ripoti za ubora huo, katika siku na miaka ijayo kwa manufaa ya nchi.