Umasikini unavyoleta simulizi nzito kuhusu hedhi ya mabinti

16Jun 2016
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Umasikini unavyoleta simulizi nzito kuhusu hedhi ya mabinti

AFYA bora ni jambo la msingi kwa mtu yoyote, kwani mtu akiandamwa na magonjwa mara kwa mara, ni wazi hata shughuli za uzalishaji zitasimama.

Mkurugenzi wa taasisi ya Binti yetu, Rose Urio wa kwanza kulia akiwa pamoja na wanafunzi wa shule ya Msingi Saku iliyopo Chamanzi Wilayani Temeke.

Serikali ina jukumu la kuhakikisha linawalinda watu wake kwa kutoa huduma bora ya afya kupitia vituo vya afya na hospitali, sambamba na upatikanaji wa bidhaa bora na dawa.

Hivi sasa wanafunzi wengi wa kike wanaofikia umri wa kupevuka, wanashindwa kuhudhuria masomo yake ipasavyo kwa zaidi ya siku tatu hadi tano kwa mwezi. Hiyo ni kutokana na hofu anapokuwa katika kipindi cha hedhi.

Kwa mujibu wa utafiti mbalimbali uliofanywa na taasisi mbalimbali, ikiwemo Haki Elimu mwaka 2013, kutokana na kutohudhuria masomo kikamilifu kila mwezi, jambo hilo humfanya mwanafunzi kukosa masomo kila mwezi na kwa kiasi kikubwa linalozorotesha ufaulu wake darasani.

Baadhi ya wanafunzi hushindwa kuhudhuria vipindi vyote vya masomo wakiwa katika hedhi, ni kwa sababu wengi wanaogopa kuchafua sare zao za shule, jambo linalowajengea hofu ya kuchekwa na kutaniwa na wanafunzi wa kiume na walio chini kiumri.

Mei 28 mwaka huu, Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Hedhi Salama Duniani na taasisi mbalimbali zinazoshughulika na masuala ya watoto wa kike, ikiwamo Taasisi ya Binti Yetu, waliadhimisha siku hiyo kwa kuvunja ukimya na kuzungumzia suala zima la hedhi salama.

Nchini Tanzania, bado kitendawili cha hedhi salama kwa wasichana na ni changamoto walio wengi, hususan wanaoishi vijijini.

Pamoja na mambo mnengine, bado elimu ya kuhusiana na hedhi salama inahitajika kutolewa kwa ukamilifu, hasa matumizi ya vifaa salama, wakati wa hedhi, ili kuwaepusha wasichana na magonjwa yanayoambatana na hedhi.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa salama vya kutumiwa na watoto wa kike na wanawake wawapo katika hedhi.

Matumizi ya vitu visivyo salama, yanaweza kusababisha hatari ya maambukizi ya magonjwa kwa wahusika.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Binti Yetu, Rose Urio, anasema kukosekana elimu ya hedhi salama na matumzi ya vifaa sahihi kama taulo za kike, huweza kupelekea msichana kupata magonjwa ya ngozi, saratani na maambukizi mengine kwenye njia ya uzazi.

Urio anasema utafiti uliofanywa na taasisi yake vijijini, umebaini wasichana wengi wanatumia vifaa mbadala wa taulo za kike. Hiyo ni kutokana na kukosa pesa za kununua vifaa vya kisasa, ambavyo hutupwa baada ya matumizi.

“Yaani maeneo ya vijijini hasa kutoka jamii za wafugaji hutumia ngozi za wanyama, makapi ya miwa, magazeti, pamoja na makaratasi kwa kukosa fedha za kununua taulo za kike,” anasema.

Hivyo, anawaomba wadau hususan wanawake, kutoa mchango kwa watoto wa kike, angalau kwa kuwawezesha kupata taulo jozi pakiti moja kwa kila mwezi, jambo lisilohitaji kiasi kikubwa cha pesa kwa mwezi, ili kumuweka binti salama.

Anasema ipo haja ya wanawake wanaharakati na wasio wanaharakati, kuungana kutoa elimu katika shule za mijini na za vijijini, ili kuwajengea ufahamu na kuona hedhi ni jambo la kawaida kwao.

“Serikali inapaswa kutuunga mkono kwa juhudi zetu ambazo tumezianzisha sambamba na taasisi na mashirika binafsi, ili kutusaidia upatikanaji wa taulo za kike unaoendana na kutoa elimu ya hedhi shuleni, kupunguza utoro kwa wanafunzi,” anasema

TAULO ZA KIKE MBADALA

Urio, anasema kuwa mbali na elimu sababu kubwa inayosababisha kuwepo na matumizi mbadala ya taulo za kike ni ukosefu wa fedha.

Anasema wasichana ambao wanatumia njia mbadala ama taulo za kike za bei ndogo ambazo zina madhara kwa ngozi zao ni changamoto ya kipato na elimu.

Anaongeza kuwa wanawake wanaotumia njia hizo ni vizuri wakaacha mara moja ili kulinda afya zao, hata hivyo ameiomba serikali kuangalia jinsi ya kuwasaidia watoto wa kike walioko mashuleni kupata taulo hizo.

UBORA WA TAULO ZA KIKE

Urio anasema kuwa serikali kupitia mamlaka zake, inapaswa kuweka utaratibu wa kuzikagua taulo za kike ambazo zinaingizwa nchini, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuingizwa taulo feki.

Anasema watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya ngozi kutokana na uhalisi wa ngozi zao wanapotumia taulo za kike ambazo hazina ubora.

“Japo hakuna utafiti ambazo zimefanywa kuhusu matumizi ya taulo za kike kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, lakini ni wazi kuwa umakini wa hali ya juu unatakiwa ili kukabiliana na matatizo ambayo yanaweza kuwakumba watu wenye ulemavu wa ngozi,” anasema

KAULI YA SERIKALI

Katika maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani, serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Tekniolojia na Mafunzo ya Ufundi, inasema ipo katika mchakato wa kutafuta wafadhili kusaidia kutoa huduma za taulo za kike kwenye shule, ili kuwawezesha wanafunzi wasikose masomo wanapokuwa katika kipindi hicho.

Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa Huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira, kutoka wizara hiyo, Theresia Kuiwite, anayesisitiza kuwa, elimu bure isiishie kwenye ada pekee.

Anasema hata taulo za kike, ili waweze kupatiwa na ndio maana wanatafuta wahisani watakaokubali kujitolea katika kuisaidia serikali, kusambaza bidhaa hiyo kwa ajili ya wanafunzi.

Hata hivyo, anasema kwa sasa wizara yake inafanya utafiti wa mahitaji ya taulo za kike zinazotakiwa kwa shule zote za msingi na sekondari, hasa zile za serikali ili waje na mkakati wa mahitaji yao.

WAZALISHAJI TAULO

Urio anasema taasisi yake imefanya mazungumzo na serikali, kwa ajali ya kufungua kiwanda cha kutengeneza taulo za kike, kwani malighafi zinapatikana kwa wingi nchini.

Anasema kuna haja ya kuanzishwa kiwanda cha kutengeneza taulo za kike nchini, kwani bidhaa hizo zinazotumika kwa wingi ni za kigeni na hazina ubora stahiki.

“Kama Tanzania tungekuwa na viwanda vya taulo za kike nina imani wasichana wangeacha kutumia ngozi za wanyama na makapi ya miwa wakati wa hedhi, kwani tungetengeneza na kuuza kwa bei rahisi, tofauti na hizi zianazoingia kutoka nje ya nchini,” anasema

Urio anasema ameshawsiliana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini, (SIDO) ili kuwapatia wataalamu na kuwapa ushauri jinsi ya kuanzisha kiwanda kitakachopunguza gharama za taulo hizo.

Anasema kuwa malighafi za kutengenza taulo hizo, zipo nchini na kinachotakiwa sasa ni kwa mamalaka husika ni kutoa ushirikiano katika mchakato wa kuanzishwa kiwanda hicho, ili wasichana wapate kifaa hicho na kuendelea kulinda afya zao.

WAFANYABISHARA
Mmoja wa wafanyabishara wa duka la bidhaa za kike na watoto, lililopo Kimara jijini Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake liliandikwa gazetini, anasema taulo za kike zinazonunuliwa kwa wingi ni zile ambazo ni za gharama nafuu.

“Nimekuwa nikipata malalamiko kutoka kwa wateja zangu kuwa taulo ambazo zina gharama ndogo, zimekuwa zikiwasababishia muwasho wakati wa kutumia kutokana na ubora wake kuwa mdogo,”a anasimulia.

Anaongeza kuwa, zipo taulo zenye gharama ya juu na ni salama kwa watumiaji, kwani hajawahi kupokea malalamiko katika matumizi yake.

Habari Kubwa