Umeme wa vijijini wachochea kasi ya maendeleo Morogoro

09Aug 2016
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Umeme wa vijijini wachochea kasi ya maendeleo Morogoro

WANANCHI wa vijiji vilivyofikiwa na mradi wa umeme vijijini (REA) wametakiwa kuupokea na kuutumia vyema kwa sababu ya gharama zake kuwa nafuu huku manufaa yake ni makubwa katika kuboresha maisha na kukuza uchumi.

Mhandisi wa Ujenzi wa miradi kwa wateja wadogo wadogo wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) David Chisoto anasema kuwa, gharama hizo ndogo ni za uingizaji umeme kwenye nyumba zao. Umeme wa kawaida kijijini hulipiwa shilingi 177,000 .

Kwa kawaida umeme mkubwa wa njia tatu hulipiwa gharama ya sh. laki tisa. REA hulipia gharama hizo na mteja huachiwa kulipa gharama za kodi ya VAT pekee kuwa sh. 139,000.

Ameipongeza Serikali kwa kuboresha juhudi za kufikisha nishati ya umeme hasa vijijini kwa kutumia miradi ya REA I na II na kuwezesha wateja 1,306 kuunganishiwa huduma hiyo kati ya wateja 5,662 waliopo vijiji 64 kwenye wilaya za Morogoro vijijini, Mvomero, Gairo, Kilombero na Ulanga.

Chisoto anasema, mradi huo wa REA II ulipaswa kukamilika mwezi Septemba 2015 hata hivyo ulilazimika kuongezewa muda ili uweze kukamilika kufuatia maeneo mengi yaliyokusudiwa bado hayajafikia hivyo unatarajia kukamilika mwaka huu.

Anasema, licha ya mradi kupendeleza kutoa umeme katika maeneo hayo ya vijiji, lakini maeneo mengine hayana wingi wa watu na kusababisha TANESCO kuchukua muda mrefu kufikisha huduma hiyo kufuatia kukabiliana na changamoto inayokinzana na utaratibu wao wa kuweka umeme, huzingatia idadi kubwa ya watu waliopo kwenye eneo na ubora wa nyumba zinazotakiwa kuwekwa umeme huo.

Kufuatia kuwepo kwa mradi huo anasema kuwa, shirika hilo limefanikiwa kukusanya Sh. 37,982,000 kutokana na malipo ya huduma ya umeme wa REA II kati ya hizo Sh. 33,534,000 zimetokana na huduma ya umeme wa njia moja na Sh. 4,448,000 zimetokana na umeme wa njia tatu.

Naye Mkandarasi wa Kampuni ya kusimamia ujenzi wa umeme wa REA II, MBH-Power Limited, Vinay Kumar anasema tayari kilometa 270 za msongo mkubwa zimekamilika kati ya kilometa 376 za msongo mkubwa zilizopo na kilometa 130 za msongo mdogo kati ya km 170 zilizopangwa tayari zimekamilika sawa na asilimia 70 ya utendaji wa shughuli hiyo, huku transfoma 50 kati ya 70 zikiwa zimeshafungwa kwenye maeneo husika na kuwashwa tayari kwa matumizi ya umeme vijijini.

Kumar anasema, kufuatia changamoto mbalimbali wameshindwa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.Miongoni mwa changamoto hizo ni mabadiliko ya hali ya hewa na mvua, wafanyakazi na mawakala wadogo kufanya kazi kwa muda na kuacha kazi bila taarifa maalum.

Meneja wa TANESCO mkoani Morogoro Mhandisi John Bandiye amesema, REA imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha umeme kwa wanavijiji kwa kuongeza kilometa 376.5 za umeme wa kati na kilometa 180 za umeme mdogo kwa watumiaji wa umeme katika mkoa mzima na kwamba mradi huo uliosimamiwa na Serikali, umeweza kufikisha huduma ya umeme katika maeneo ambayo Tanesco peke yao wasingeweza kufika kwa wakati, kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ubovu wa miundombinu hasa ya barabara.

Mhandisi Bandiye anasema, katika kutekeleza shughuli za kuingiza umeme kwenye vijiji, hivyo wameweza kukumbana na changamoto nyingine ambayo ni kuzuiliwa kukata miti ili kupitisha mradi kwenye mashamba ya wanavijiji, hali iliyofanya wakati mwingine mradi kuchukua muda mrefu kukamilika kwa kuogopa kusababisha hasara na athari kwa wananchi matawi ya miti yatakapogusa kwenye nyaya za umeme.

Anasema, viongozi wa vijiji wanapaswa kutumia nafasi yao vyema kwa kusimamia suala la miradi ya REA kwenye maeneo yao, kwa kuwashawishi wananchi waruhusu umeme kupita kwenye mashamba na maeneo yao ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo.

Katika kutekeleza mradi huo, wananchi wa vijiji kadhaa kikiwemo kijiji cha Doma kata ya Melela wilayani Mvomero mkoani hapa wameipongeza Serikali kwa kutayarisha mradi huo, huku wakidai kukumbwa na changamoto mbalimbali kabla ya kufikishiwa kwa mradi huo.

Hidaya Polinda mkazi wa kijiji cha Mangae, anaiomba Serikali kusimamia na kukamilisha huduma hiyo mapema vijijini ili kuwaondolea usumbufu baadhi ya wanavijiji wanaolazimika kufuata huduma mbalimbali muhimu ikiwemo ya matibabu mkoani Morogoro, hali inayotishia uhai wa watoto na kina mama, hasa wajawazito wanapotaka msaada wakati wa kujifungua.

Anasema kuwa wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 45 kufika Hospitali ya Rufaa Mkoa Morogoro ili kupata matibabu na kwamba walitumia umeme wa Solar ambao hauna nguvu ya kuweza kufanya mambo mengi zaidi ya kupata mwanga nyakati za usiku pekee.

Hidaya anasema, kukosekana kwa umeme kwenye kijiji chao kuliwafanya watumie gharama kubwa kununua mafuta ya taa kila siku ili waweze kupata mwanga hasa nyakati za usiku.

Naye Imani Magenda mkazi wa kijiji cha Mangae kata ya Melela anasema, suala la kuingiza umeme kijijini hapo, limewasaidia kupiga hatua katika suala zima la maendeleo na hatimaye kuweza kukuza uchumi wao walioukosa kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme wa uhakika kijijini hapo.

Anasema kwa sasa wameweza kufungua biashara zinazowawezesha kukuza uchumi wao ikiwemo kuanzisha maduka, huduma za vinywaji na machapisho ya makaratasi na kutegemea kupata wateja kufuatia kuwepo kwa huduma ya umeme.

“wakazi wa Mangae hasa vijana tulikuwa na nia ya kujituma muda sana ili kuleta maendeleo yetu, sasa umeme umefika tutaweza kufungua huduma za machapisho ya makaratasi, kuboresha baa zetu na hata kuhifadhi vyakula kwa muda mrefu kwenye mafriji mambo ambayo kwetu imekuwa ni ndoto” alisema Magenda.