Umuhimu wa jina la Kampuni au Biashara

23Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Umuhimu wa jina la Kampuni au Biashara

Moja ya mambo yawezayo kumsaidia mjasiriamali au mfanyabiashara kuifanya biashara yake kwa mafanikio ni kutambua fursa za kisheria zilizopo kabla na baada ya kuwekeza muda na raslimali katika biashara husika.

Kwa kifupi tu kulingana na ufinyu wa nafasi katika safu hii, tutayataja mambo muhimu ambayo siku zote unapaswa uyazingatie kabla na wakati wowote unapochagua jina la biashara au kampuni unayotaka ikuinue katika harakati zako za kujikwamua kimaisha.

Biashara au kitegauchumi chochote ili kifanikiwe inabidi kuandaliwa na kuendeshwa katika misingi iwezayo kumsaidia mwenye biashara husika kupata thamani halisi ya kile alichokiwekeza
‘Kampuni’(company) na pia ‘Jina la Biashara’ (Business name) ni maneno yanayotumika kila siku katika jamii tunamoishi. Yawezekana hujui yana maana gani, lakini ni lazima umepata kuyasikia ama kama hujapata kuyasikia basi unahusika nayo moja kwa moja, kila siku inayopita.

‘Kampuni’na ‘jina la biashara’ni misamiati miwili iliyo na maana tofauti na pia athari tofauti si tu kisheria, pia katika masuala mengine muhimu ya ki-biashara na uwekezaji.

Kwa hapa Tanzania BRELA ndiye Wakala wa Serikali mwenye mamlaka pekee kuhusiana na mambo yote ya usajili wa makampuni na majina ya biashara.

Chukulia mfano unapita dukani kununua sabuni au mkate basi ujue mwenye duka hilo anaendesha biashara yake kwa jina la biashara au kampuni aliyoisajili kuendeshea biashara hiyo. Majina haya huja kwa namna na katika lugha yoyote kutegemeana na utashi wa yule aliyelichagua.

Laweza kuwa jina la kimombo, Kiswahili, Kilugha ama mchanganyiko wowote. Majina kama ‘Uwanja wa Fisi Shop’, ‘Kivulini Bar’, ‘Kinyozi Mtanashati’, ‘Elimu Duka la Vitabu’, na kadhalika.

Pamoja na uhuru huu, yapo mambo kadhaa ya msingi sana kwa mfanyabiashara anayopaswa kuyazingatia ili jina la biashara au kampuni anayoianzisha liwe na maana na faida kwake. Ni vizuri kwanza, tuelimishane kidogo maana na tofauti zilizopo kati ya neno ‘kampuni’ na neno ‘jina la biashara’ kwa kadri yatumikavyo.

Ingawa maneno haya mawili ni ya kibiashara, uelewa wake unapaswa kufafanuliwa kisheria na hivi ndivyo tunavyofanya hapa. Katika kufanya hivi tunaongozwa na sheria mbalimbali za biashara, sheria yetu ya majina ya biashara, sheria ya makampuni ya mwaka 2002, pamoja na maamuzi muhimu ya kimahakama yaliyofafanua masuala haya, na hususan kesi maarufu ya Salomon v. Salomon ambayo kwa miaka mingi imenukuliwa sana katika haya tunayojadili humu,
‘Jina la biashara’ ama ‘business name’ kwa kimombo ni jina ambalo mjasiria-mali, mfanyabiashara au mwekezaji analibuni ama kulichagua miongoni mwa majina kadhaa na hatimaye kuchukua uamuzi wa kulisajili kama jina linaloitambulisha rasmi biashara anayoifanya au ile anayokusudia kuifanya katika siku za usoni.

Kuna tofauti kubwa kisheria baina ya kampuni na jina la biashara. Kwa kifupi tu ni kwamba kila kampuni ni jina la biashara pia ingawa si kila jina la biashara ni kampuni.

Hata hivyo, haitoshi tu kukaa chini na kuchagua jina fulani na kukimbilia kulisajili. Lazima ukidhi vigezo kadhaa na ufahamu hatua zinazofuata baada ya hapo.
Mosi, unapaswa uzingatie matakwa ya sheria na matakwa ya utambulishaji biashara kuletako manufaa ya kung’ara katika soko lenye ushindani (branding) zaidi ya matakwa yako binafsi.

Ndiyo kusema, inawezekana kabisa ukalipenda jina fulani na pengine likavutia hasa kibiashara lakini hili pekee halitoshi. Nina maana gani hapa?
Jina laweza kuwa jema fikrani mwako na hata katika macho yako pale unapoliandika katika karatasi au mchanga. Lakini jina hili lazima pia likubalike kisheria.

Kuna vikwazo vichache vya kisheria unavyopaswa kuvikidhi ili jina hilo lipate baraka zinazoweza kumruhusu Msajili wa majina ya Biashara alibariki na alipitishe kwa kuuweka wino wake katika hati rasmi ya kulisajili. Vikwazo viko kadhaa lakini vilivyo muhimu zaidi ni pamoja na kwamba jina husika halipaswi kufanana kabisa na jina jingine la aina hiyo lililosajiliwa na linaloendelea kutumika.

Vinginevyo utapaswa uthibitishe kwamba jina hilo japo liliwahi kusajiliwa awali halitumiki tena ama limeshapoteza haki ya kulindwa kisheria kama jina la biashara. Katika hili hatutaweza kwenda kwa undani kwa sababu lina mitego mingi yenye kuhitaji upate ushauri mahsusi wa kisheria.

Kikwazo cha pili kinachoweza jina fulani likwame na hivyo likataliwe kusajili ni iwapo jina hilo, japo halijasajiliwa lakini sheria imekataza lisisajiliwe kwa vile ni msamiati ama jina lililozoeleka na linalotumika sana.

Mfano, itakuwia vigumu sana kumshawishi Wakala wa Kusajili wa makampuni au majina ya ya biashara (BRELA) akusajilie kampuni au jina la biashara itakayoitwa ‘Serikali’, ‘Kinyesi’ na kadhalika.

Hata majina kama ‘Maji’ au ‘mgahawa’ pekee ni vigumu kupitishwa kama yalivyo, kwa sababu ni misamiati iliyozoeleka mno na ambao haiwezi kuhodhiwa na mtu mmoja. Unaweza kuyatumia kwa kuyaunganisha na majina au maneno mengine kama vile ‘maji ladha barafu’, ‘Kata Kiu Pure Drinking Water’ ama ‘Mapochopocho Misosi Restaurant’.

Jina fulani laweza kukakataliwa kusajiliwa iwapo pia halikubaliki kisheria ama ni kinyume na sera za nchi au misingi ya ustaarabu ama linahusika na biashara ambayo imekatazwa kufanyika kama ukahaba au mihadarati.

Kwa hivyo mjasiriamali makini na mwenye kutii sheria hawezi hata siku moja kuwazia aiite biashara au kampuni yake majina kama ‘Mihadarati Mateja Store’, ‘bangi nibangue Shop’ ama ‘Makahaba Lodge’.

Halafu tena jina fulani linaweza kupita na kusajiliwa kama kampuni ama jina la biashara lakini je, ndiyo utachagua jina lolote tu? La hasha. Zipo kanuni za uchaguzi wa majina yenye manufaa na katika hili unaweza kulifanya mwenyewe kwa umakini au kuomba ushauri wa wataalam waliobobea katika fani ya utambulishaji biashara ambapo jina la biashara husika inaweza kutambulika kirahisi miongoni mwa nyingi katika soko lenye ushindani (Branding).

Katika hili utapaswa uchague jina, nembo (logo), motto (kauli-mbiu) na vionjo vingine vya kibiashara. Jina kama PEPSI na nembo kama zile za SONY, CNN ama FedEX ni ushahidi mzuri katika kuthibitisha ni jinsi gani unapaswa kuwekeza maarifa na muda katika kuchagua jina la biashara na nembo. Sambamba na hili kuna matumizi ya kauli-mbiu (motto) kama ‘IPP Cares for You’ ama ‘Konyagi: The Sprit of the Nation’ au hata msisitizo kama ile ya ‘Sidanganyiki’ ama ‘Tuko wangapi?’.

Makampuni makubwa, maarufu na yaliyofanikiwa zaidi duniani na hapa nchini mengi yana majina mafupi tu na rahisi kuyakumbuka na tena ni yale yenye maneno ambayo hayana maana yoyote katika kamusi au matumizi ya kawaida ya lugha.

Tazama majina haya: GOOGLE, YAHOO, SONY, COCA-COLA, FACEBOOK, TWEETER, eBAY, HAKIELIMU, TWAWEZA, KONYAGI, DOMPO. Unajifunza nini katika kuchagua jina la biashara, kampuni au bidhaa?

Habari Kubwa