Unajua kwanini ‘sunzua’ huota kwenye ngozi?

12May 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Unajua kwanini ‘sunzua’ huota kwenye ngozi?

BAADHI ya vinyama au vidoti vinavyojitokeza kwenye ngozi ya binadamu humfanya mtu kuona ni tatizo kubwa, lakini alama hizo kwa kawaida hazina madhara.

Vinayama hivyo ambavyo baadhi huviita sunzua vinakuwa kama alama na vijinyama hivyo vinapoota kwenye ngozi huwa laini na hutofautiana kwa rangi: Kawaida huwa na rangi inayofanana na ngozi ya mtu, vinaweza kuwa rangi ya kahawia lakini mara nyingi hufuata rangi ya mtu aliyonayo.

 

Baadhi ya vinyama hivyo wakati mwingine hubadilika rangi na kuwa vyekundu au vyeusi kama mtu aliyenavyo ataamua kuviminya minya.

 

Vinyama au alama hizo aghalabu huwezi kuviona kwa urahisi bila kutumia kifaa maalumu (Microscopic), vingine hukua mpaka kufikia urefu wa milimita tano au zaidi.

 

Mtu anaweza kuota kinyama kimoja au zaidi sehemu moja, iwapo mahali kinapoota itakuwa imejificha au imejikunja kama vile chini ya matiti, pembeni au mgongoni ambako sio rahisi kuviona au asijue kama ameota vinyama hivyo mpaka awe mara kwa mara anapooga anajisugua sehemu zote za mwili au kwa kujiangalia kwenye kioo kwa makini.

 

Lakini watu wengine huvigundua kwa sababu huwa vinawasha vinapogusana na nguo.

 

“Vinyama kwenye ngozi havina madhara, hata hivyo vinaweza kusababisha maumivu kutokana na muwasho na msuguano unaotakana na nguo au vito kama hereni, bangili au mkufu,” anafafanua Daktari Nkanyezi Ferguson, ambaye ni Profesa na mtaalamu wa magonjwa ya ngozi kutoka Chuo Kikuu cha Uuguzi, Iowa.

 

SABABU ZA UOTAJI

Vinyama hivi huota karibu nusu ya watu wenye umri mkubwa, hupendelea kuota zaidi kwa watu wanaoelekea kuwa wazee.

 

Vinyama hivi huota kwa kurithi. Kama kwenye familia yako kuna mtu mwenye vinyama hivyo, mwingine anaweza kuvipata. “Wanaume na wanawake huathirika sawa sawa,” anasema Dk. Ferguson.

 

Watu wanene sana wako kwenye nafasi kubwa ya kupata vinyama hivyo kwa sababu ya kuwa na ngozi iliyojikunja kunja.

 

Lakini kuna sababu nyingine ukiwa mnene sana kupata vinyama hivi, kwa sababu unakuwa kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari (type 2 diabetes) na utafiti umegundua kuwa mtu mwenye aina hiyo ya kisukari anapata vinyama vingi, kama ilivyo kwa watu wenye sukari ya juu sana.

 

Kutokana na hali hiyo kuna uhusiano kati ya vinyama kwenye ngozi na insulini ambayo inadhibiti kiwango cha sukari kwenye damu.

 

“Watu wanene sana wenye kisukari wako kwenye uwezekano wa kuota vinyama kwa sababu ya kiwango kikubwa cha insulini,” anaeleza Daktari Robert Courgi, kutoka Hospitali ya Long Island, New York.

 

“Insulini inachochea ukuaji na kusababisha seli ya ngozi kubadilika. Hali hii kufanya vinyama kuendelea kuongezeka ambayo ni dalili ya kisukari,” anaongeza Dk. Courgi.

 

UNAWEZA KUVIONDOA

 

Vinyama hivi vinaweza kuondoka vyenyewe. Lakini kwa kawaida, mara vinapojitokeza, huwa na kawaida ya kubaki kwenye ngozi.

 

Inafahamika kuwa mtu anaweza kutaka kuviondoa, fikiri kwanza kwa sababu hakuna sababu za kiafya zinazoeleza viondolewe.

 

“Hakuna sababu za kitabibu zinazolazimisha kuondoa vinyama, ni sawa tu kama utaviacha,” anasema Dk. Ferguson. “Unaweza kuviondoa kama vitakuwa vinasumbua.”

 

NJIA SALAMA KUVIONDOA

 

Unapotaka kuviondoa vinyama kumbuka kuwa vimegusa mwili, lazima uwe muangalifu, usifikiri kuwa unaweza kuvikata kwa mkasi kirahisi, vinaweza kusababisha maumivu, kuvuja damu na uwezekano wa kupata maambukizi.

 

Mtu inambidi amuone mtaalamu wa magonjwa ya ngozi kuhakikisha anaondolewa kwa njia salama na daktari.