Unajua wakulima wadogo ndio wanaoilisha dunia siku zote?

30Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Unajua wakulima wadogo ndio wanaoilisha dunia siku zote?

WAKULIMA wadogo mara zote wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kujenga mifumo endelevu ya chakula, iwapo tu watakuwa katika mustakabali sahihi kimaisha, ikiwamo amani na mazingira bora.

Mkulima mdogo akiwajibika shambani. PICHA: DW.

Sabrina Elba, Balozi wa Hisani wa Mfumo wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, anasema akiwa na mume wake miaka miwili iliyopita, walienda nchini Sierra Leone ambako walikokutana na watu anaotawataja kuwa majasiri.

Hao ni kinamama na kinababa walioweza kuhimili misukosuko ya vita viliyvoikumba nchi yao, pia athari za janga la ugonjwa Ebola, lakini bado walisonga mbele na maisha yao kama kawaida.

Matumaini yalionekana wazi na mustakabal ulikuwa wa matarajio makubwa. Kabla ya hapo, hakuna aliyekuwa anajua kwamba janga jingine lilikuwa njiani linawanyemelea, wimbo wa leo ‘maambukizi ya virusi vya corona.’

Hata hivyo, ukweli unabaki kwamba hata kabla ya janga hilo kuibuka, nchi nyingi za Afrika kwa miezi mingi zilikuwa zinakabiliwa na matatizo makubwa.

Hapo panatajwa nchi za Zimbabwe zilikuwa zinapambana na athari za ukame mbaya kuwahi kutokana na mahali hapo katika kipindi cha miongo kadhaa iliyovuka. 

Nchi za eneo la Mashariki mwa Afrika, nazo zilikumbwa na baa la nzige walioteketeza mazao. Hali hiyo ilikuwa haijatokea mahali hapo kwa kipindi cha miaka 70. Baa la nzige lilizidisha umasikini wa jamii mahali hapo na likahatarisha mfumo wa upatikanaji chakula kwenye eneo hilo.

Ziara ya Sierra Leone, ikamfungulia balozi huyo na mumewe darasa kwamba binadamu wanaweza kuhimili shida katika sura ya taifa: Iwe ni vita, majanga ya asili au maambukizi ya virusi, binadamu wanaweza kuzikabili shida hizo, ili mradi tu wanapatiwa msaada stahiki.

Sabrina anaufanyia kazi Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, katika ziara hiyo aliweza kujifunza yahusuyo ya nguvu ya kilimo, jinsi kinavyoelekeza maendeleo kijamii kwa jumla.

Anajivunia kwamba, aliwezeshwa kutambua kwamba, ikiwa mtu anataka kuwawezesha kina mama na vijana, pia kujali umuhimu wa ardhi na dunia, mtu anapaswa kuwathamini wanaopanda mazao, yaani wakulima wadogo, kwani wao ndiyo walinzi wa dunia.

Wakulima hao wadogo ndio wanaotoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa chakula wa uhakika. Wanazalisha asilimia 30 ya chakula chote duniani.

Dhima yao kuu ni zaidi katika nchi za Kusini mwa Janga la Sahara, ambako wanazalisha asilimia 80 ya chakula chote kinachopatikana kwenye eneo hilo.

UNDANI WAKE

Duniani kote mashamba milioni 500 ya wakulima wadogo yanazalisha chakula kwa ajili ya watu zaidi ya bilioni mbili .Mashamba ni madogo lakini manufaa yake makubwa.

Hata hivyo, wakulima hao wanaelezwa wanaishi kwenye maeneo yaliyo katika hatari kubwa kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Inaelezwa kitaalamu kwamba, ikiwa kundi hilo halitapatiwa msaada, maafa yanaweza kuwa makubwa kwenye jumuiya zao na katika mfumo wa chakula duniani, kwa kutilia maanani wao ndiyo nguzo ya mfumo huo.

Wakulima wadogo wanakabiliwa na magumu kadha wa kadhaa, yanayojumuisha jukumu la kukidhi mahitaji ya binadamu wanaoongezeka kila kukicha.

Pia, wana tatizo la kupungua mazao wanayozalisha kutokana na kuharibika ardhi inayoweza kulimika, sambamba na tatizo la kuongezeka joto linalosababisha kupungua kwa robo ya mazao ambayo ni asilimia 25 kwa lugha ya kitaalamu
Ni mtazamo unaosisitiza ulazima wa kuwawezesha wakulima walioko katika makazi ya mashambani, wakapewa mbinu za kukabili hali zao ngumu, zinazochangiwa na kutetereka hali ya hewa.

Ni kwa njia hiyo kwamba, itawezekana kuhakikisha uthabiti wa maendeleo barani Afrika, ambako kuna uwezo wa kuilisha dunia, ikiwa msaada stahiki utapatikana.

Maendeleo ya kilimo Afrika bado yanaelezwa kutia moyo, kwani uzalishaji umeongezeka kwa asilimia 160 katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, hivyo kuvuka  kiwango cha wastani wa dunia.

Hata hivyo, bado kuna haja ya maboresho zaidi. Hadi sasa ni asilimia 1.7 tu ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya dharura za tabianchi zimeenda kwa wakulima wadogo katika eneo tajwa. 

Maoni ya wataalamu yanasisitiza kwamba, ikiwa nchi zitachukua hatua sasa na kutekeleza ahadi zilizotoa za msaada wa fedha kwa ajili ya juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, zitakuwa zinawekeza katika maendeleo ya siku za usoni.

Kwa mujibu wa DW