Upara, nywele za kijivu ni ishara magonjwa ya moyo

05Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Upara, nywele za kijivu ni ishara magonjwa ya moyo

WANAUME wanaokuwa na upara kichwani, mbali na wale wenye nywele za rangi ya kijivu wako katika hatari kubwa ya kupatikana na magonjwa ya moyo miongoni mwa wanaume walio chini ya umri wa miaka 40, utafiti unasema.

Utafiti uliofanyiwa zaidi ya vijana 2,000 nchini India ulionyesha kuwa wengi waliokuwa na ugonjwa wa moyo walikuwa na upara na nywele za kijivu ikilinganishwa na wanaume wenye nywele kichwani.

Utafiti uliofanywa na Idara ya Magonjwa ya Moyo barani Ulaya, utasomwa katika kongamano la kila mwaka la magonjwa ya moyo nchini India.

Hata hivyo, wakfu wa Uingereza unaosimamia magonjwa ya moyo umesema kuwa pamoja na ugunduzi huu, sababu zingine hatari pia ni muhimu.

“Utafiti huu unasema kuwa miongoni mwa wanaume wenye upara na nywele za kijivu unaweza kuwagundua wale walio na hatari ya matatizo ya magonjwa ya moyo,” anasema daktari Mike Knapton alipozungumza na BBC.

Hata hivyo, hilo sio jambo ambalo linaweza kubadilishwa na watu zaidi ya kudhibiti hali ya maisha.

Tafiti za nyuma zimeonyesha kwamba magonjwa ya moyo yanaweza kusababishwa na vyanzo mbalimbali kama vile viwango vya juu vya mafuta na shinikizo la damu na kuwa hivyo ndivyo vitu muhimu zaidi kuvifuatilia.BBC