Upinzani na hatma ya Uchaguzi Mkuu katika jumuiya ya EAC

15May 2019
Mashaka Mgeta
DAR ES SALAAM
Nipashe
Upinzani na hatma ya Uchaguzi Mkuu katika jumuiya ya EAC

KWA takribani miaka minne mfululizo kuanzia mwakani, nchi tano zilizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zitakuwa na Uchaguzi Mkuu wa marais na wabunge.

Tanzania na Burundi zitafanya uchaguzi huo mwakani, wakati Uganda itakuwa mwaka mmoja baadaye (2021), Kenya (2022) na Rwanda (2024).

Pamoja na changamoto za Uchaguzi Mkuu kutofautiana kati ya nchi moja hadi nyingine, lakini ‘tishio’ la nguvu za upinzani limekuwa kubwa kwa muda mrefu, kiasi cha kutishia ‘uhai’ wa utawala kwa mataifa hayo.

Hata hivyo, wakati mataifa hayo yakijiandaa kwa uchaguzi huo, mazingira ya kisiasa yanaonyesha kupungua kwa nguvu za upinzani kunakotokana na mikakati tofauti ya kisiasa inayoundwa na kutekelezwa na viongozi waliopo madarakani.

Mwanaharakati ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchaguzi, Thomas Munanka, anasema ingawa kuna tofauti ya mfumo na ushiriki wa wananchi katika siasa na uchaguzi, mazingira ya jumla yanadhihirisha kuwapo kazi kubwa kwa wapinzani kushindana na watawala.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga.

“Ukiona matukio mengi ya kisiasa yanayotokea kama kule Kenya ambapo Rais Uhuru Kenyatta alishikana mkono wa amani na mpinzani mkubwa wa siasa nchini humo, Raila Odinga na hapa kwetu ukiona kurejea kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wapinzani akiwamo Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, ni dhahiri kwamba kunapunguza nguvu za wapinzani,” anasema.

Munanka anasema kabla ya kushikana mkono kwa Rais Kenyatta na Odinga, palikuwa na uhasama wa kisiasa uliochagiza vuguvugu la mageuzi kuwapo nchini humo, lakini hivi sasa ni kama Wakenya wanaongea lugha moja.

 

“Kwa wafuasi wa Odinga, ilikuwa mshtuko sana pale kiongozi wao alipojitokeza hadharani na kushikana mkono na Rais Kenyatta, kwa maana waliamini na wengine bado wanaamini kwamba Odinga alistahili kuwa mtawala lakini akaibiwa kura,” anasema.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.PICHA: MTANDAO

Katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, mwaka juzi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya ilimtangaza Rais Kenyatta kushinda katika awamu ya pili ya utawala kwa tofauti ya kura milioni 1.4 dhidi ya Odinga, lakini wapinzani walikwenda Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kupinga ushindi huo.

 

Septemba Mosi, mwaka juzi, Jaji David Maraga aliyafuta matokeo kufuatia shauri lililofunguliwa na wapinzani hususani Odinga, na kuamuru kufanyika uchaguzi wa marudio ambao hata hivyo, Odinga aliususia.

 

IEBC ilitangaza uchaguzi wa marudio kufanyika Oktoba 26, mwaka juzi ambapo Rais Kenyatta alishinda kwa asilimia 98, ingawa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilitajwa kupungua kwa takribani asilimia 40.

 

Matokeo hayo yaliibua ghasia nchini Kenya huku upinzani ukimtangaza na kumuapisha Odinga kuwa Rais wa Wananchi.

 

Hata hivyo, vurugu hizo ‘zilizimwa ghafla’ Machi 9, mwaka jana wakati Rais Kenyatta alipopeana mkono na Odinga, kisha ‘wakawekeana ahadi’ ya kushirikiana kuwaunganisha Wakenya na kushiriki shughuli za maendeleo ya taifa hasa zinazokuza uchumi na ustawi wa wananchi.

 

Pamoja na Wakenya kushtushwa na tukio hilo na baadaye kulipokea kwa namna tofauti, wapo ambao hawakulifurahia.

Miongoni mwa mwanaotajwa ni wanasiasa wa chama cha Jubilee kilichoanzishwa Septembe 8, 2016, wanaomuunga mkono Naibu Rais, William Ruto kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

 

Pia, kushikana mkono kwa Rais Kenyatta na Odinga, kuliwaleta pamoja wanasiasa hao wanaotoka kwenye `familia rafiki’ za wapigania uhuru wa taifa hilo, Jaramogi Oginga Odinga na Rais wa kwanza wa taifa hilo, Jomo Kenyatta. Wote hao wamefariki.

 

Kuwa pamoja kwa Rais Kenyatta na Odinga kunatanua wigo wa kutofautiana kati ya mtawala huyo (Kenyatta) na Naibu wake (Ruto) huku Odinga na washirika wake wakidaiwa kupewa fursa nyingi zinazowafanya washiriki kampeni zisizo rasmi za kumsaidia Odinga dhidi ya Ruto anayeonekana kuwa na nguvu kubwa za kisiasa.

 

Mwanasiasa kijana nchini, Sophia Shamte, anasema tathmini ya hali hiyo inaonyesha kumuathiri Odinga, kwa vile wafuasi wake wengi waliokuwa wanamtegemea, wanaweza ‘kumuona’ kuwa msaliti mwenye kujali maslahi yake zaidi ya watu wengine.

 

“Unajua Odinga ana wafuasi wengi, sasa kama ikitokea kule kupeana mkono na hizi fursa anazozipata, na Wakenya wanasema nyingine ni nyingi zaidi ya zile za Ruto, basi tafsiri rahisi ni kwamba anaweza kuonekana msaliti, hivyo wasimwamini sana kama awali,” anasema.

 

Kwa namna itakavyokuwa, Odinga bado atakuwa na ushindani mkubwa dhidi ya Ruto kutokana na ukweli kwamba Rais Kenyatta atakuwa anamaliza utawala wake, hivyo kutotumia nguvu kubwa kumuunga mkono mgombea urais yeyote kati ya watakaojitokeza, hasa wawili hao.

 

WAPINZANI KUMUUNGA MKONO MAGUFULI

 

Nchini Tanzania, kasi ya waliokuwa wapinzani katika ngazi tofauti hasa za uwakilishi wa wananchi kurudi ama kujiunga CCM ili kuunga mkono jitihada za serikali ya Rais John Magufuli, kunaelezwa kufifisha nguvu za upinzani.

 

Kuporomoka kwa wabunge na madiwani wanaojiondoa kwenye vyama vya upinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni chama kikuu cha upinzani na Chama cha Wananchi (CUF), kunaakisi kufifia kwa nguvu za kambi hiyo dhidi ya chama tawala katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

 

Kujiunga katika CCM kwa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema mwaka 2015, akiungwa mkono na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, kunaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya watu watakaowachagua (wapinzani) na ikiaminika kwamba mwanasiasa huyo ana wafuasi wengi wanaomuunga mkono.

 

Pia kuna ‘kusambaratika’ kwa CUF kulikotokana na mgogoro wa uongozi uliodumu muda mrefu kati ya pande mbili zilizomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipuma (Mwenyekiti aliyekuwa akitambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa) na ile ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

 

Hata hivyo, kambi ya Maalim Seif ilijiondoa CUF na kujiunga Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), hatua ambayo inatafsiriwa na baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa kwamba inaweza kurudisha nyuma jitihada za ‘kujipanga’ kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

 

Mbali na hayo, Mhadhiri mmoja wa sayansi ya siasa ambaye hataki jina lake kuandikwa gazetini, anasema mazingira yaliyopo sasa hayatoi fursa pana kwa wanasiasa wa upinzani kuwafikia wananchi ama sauti zao kusikika, hivyo kuweza kuwa sababu ya kutofanya vizuri katika uchaguzi huo.

 

KAGAME NA MSAMAHA WA WAFUNGWA WA KISIASA

Ingawa hatua ya Rais Paul Kagame kuongezewa muda wa utawala kufika mwaka 2034 iliwachukiza baadhi ya raia wa nchi hiyo, lakini ‘machozi yao yalifutwa’ na tamko la msamaha wa waliokuwa wafungwa wa kisiasa 2140.

 

Msamaha huo uliotolewa mwaka jana, uliwahusisha watu tofauti wakiwamo waliohukumiwa kwa makosa mbalimbali.

Miongoni mwa waliokuwa wafungwa hao ni Mwenyekiti wa chama cha Force Democratique Unies du Rwanda (FDI) Victorie Ingabire ambaye pamoja na mwanamuziki Kizito Mihigo, walihukumiwa mwaka 2010.

Ingabire alifungwa baada ya kupatikana na hatia ya kuchochea raia kuiasi serikali, kuunda makundi ya silaha ili kuivuruga nchi na kupuuza mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi.

 

 

Lakini kwa sehemu kubwa, hatua ya Mahakama nchini humo kumuachia huru mpinzani mkuu wa Rais Kagame, Diana Rwigara, Desemba mwaka jana, kuliibua hisia mpya za upinzani kupata nguvu nchini humo.

 

Mwanasiasa huyo (Rwigara) alihukumiwa kifungo cha miaka 22 jela baada ya kuzuiwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita nchini humo, akitajwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais Kagame

 

Itaendelea Jumatano ijayo…..

 

Mwandishi wa makala haya anapatikana kupitia simu namba 0754691540 ama barua pepe:[email protected].

Habari Kubwa