Uraibu huu ni tatizo Usifiche, ongea utibiwe’

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Uraibu huu ni tatizo Usifiche, ongea utibiwe’
  • SAIKOLOJIA

SIKU moja nikiwa kwenye moja ya hoteli iliyo jirani na nyumbani kwangu nikipitia makabrasha yenye taarifa za saikolojia, simu yangu ilipokea ujumbe mfupi kwenye Watsapp uliosomeka.

Baadhi ya kinadada wakitafuta wateja mitaani usiku ili kuuza ngono. Biashara hii kuuza mwili ni uraibu ambao unahusishwa na matatizo ya akili. PICHA :MTANDAO.

“Shikamoo dokta, naitwa Shubuli (si jina halisi) nina miaka 23, Mkongo lakini naishi nchini Kuwait, nina matatizo nahitaji msaada wako”.

Sikustuka kwa sababu kila siku napokea meseji nyingi kutoka kwa wasomaji wa safu hii na wanaonifuatilia kwenye vipindi vya redio na runinga mbalimbali. Tena ninapokea taarifa kutoka kwa watu wenye matatizo ya kisaikolojia. Hivyo ni kitu cha kawaida ila cha msingi ni lazima niwasiliane na mhusika kujua shida yake kwa kina. Hivyo nilianza kumdodosa kwa kina aliyetuma ujumbe huo kujua ni matatizo yapi yanayomkabili na kuhitaji msaada wangu wa kitaaluma.

Tulifanya mazungumzo marefu na Shubuli huku nikimuuliza maswali mengi ili kujua kwa kina kinachomsumbua. Alinieleza mengi lakini kwa kifupi ni kuwa ana tatizo la kujichezea sehemu za siri au kujichua ili kujiridhisha kingono. Aniambia huu ni mwaka wake wa pili akiwa na tabia hiyo.

Kwenye maelezo ya Shubuli anasema tabia hiyo ya kujichezea ameianza mara alipofika nchini Kuwait ambapo alikwenda kwa ajili ya kufanya kazi kwenye moja ya mashirika nchini humo.

Anasema kazi yake hiyo ni ya mkataba wa miaka miwili huku akitakiwa kuishi nchini humo mpaka mkataba unapofikia mwisho ndipo anatakiwa kurudi Congo.

Kwenye simulizi yake hiyo alisisitiza kuwa hakuwa na tabia hiyo ya kujichua alipokuwa nyumbani ila amejifunza baada ya kufika ugenini alipokwenda kufanya kazi.

Anasema mazingira ya kazi anayofanya yanambana na watu wengine wote kiasi cha kukosa nafasi ya kujichanganya na jinsia tofauti zaidi ya wao kwa wao ama kufikia mazingira mapya. Anafanyakazi na kinadada na jukumu lake hilo linamchanganya.

Shubuli kwenye kuvuta kumbukumbu ya namna alivyoangukia kwenye tatizo hilo la kisaikolojia anasema siku moja usiku baada ya kumaliza kazi rafiki yake wa kike wa karibu alimshawishi kula , kulala na kuoga pamoja kama njia ya kuondoa upweke waliokuwa nao.

Na kwa sababu za kimazingira takribani kila mtu katika nyumba waliyokuwa wanaishi alikabiliwa na hali ya upweke na kadri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele, hali ya kila mmoja ilizidi kuwa mbaya.

Baada ya kumshawishi yule dada akubali kulala naye bila kujua kuwa alikuwa na dhamira tofauti ambayo aliigundua baadaye. Shubuli anakumbuka kuwa walipoanza kulala pamoja alikuwa anamtomasa tomasa kama vile wanandoa wa jinsia tofauti wanavyokuwa faraghani.

Anasema hakupendezwa na hali hiyo, ilimchukiza, akamwambia hapendi na kumkanya, katika kukazia maamuzi yake alihama chumba na kulala peke yake kwenye chumba kingine ili kumkwepa yule dada ambaye hata hivyo hakumsumbua kwa sababu alimwambia ukweli wa kuchukizwa na tabia hiyo hivyo alimwacha aendelee na maisha yake.

Anasema alistahimili hali hiyo ila ilifika hatua aliona anashindwa kujizuia kwani alikuwa mpweke mno huku hamu na kufanya tendo la ndoa ikiwa juu tena kila wakati ikizidi kuongezeka kwa kasi kubwa.

Baada ya kuona hivyo ilibidi aombe ushauri wa namna ya kukabiliana na hali hiyo kwa dada mmoja aliyekuwa akifanya naye kazi. Alimwendea kwa kuwa aliheshimika na alionekana ni mstaarabu kwenye lile kundi lao ikilinganisha na wale wengine. Alimsimulia hali yake na jinsi anavyojisikia.

Mara baada ya kumaliza kumsikiliza huyo dada akamwambia Shubuli hapa watu wengi wanaishi pamoja kama mke na mume, kama yeye hawezi hali hiyo basi akanunue vifaa maalum awe anajifanyia mwenyewe masuala ya ngono au awe anajichezea sehemu za siri anapopata hamu ya tendo la ndoa.

Kwa msisitizo akamweleza huyo dada kuwa hayuko tayari kukaa na mtu yeyote kinyumba wala kujichezea au kujichua sehemu za siri.

Baada ya kushauriwa hivyo alikaa kwa muda huku akijipa moyo kwamba atavumilia lakini ilifikia hatua alishindwa ila hakutafuta hivyo vifaa vya kujifanyisha tendo la ndoa mwenyewe kama alivyoshauriwa bali alianza kujichezea sehemu za siri kwa kutumia mikono yake, akijiambia kuwa ataacha siku moja.

Anasema hali ilikuwa mbaya hadi kufikia hatua ya kuwa teja na kwamba hajimudu tena na anajiona ameathirika sana.

Shubuli ananiomba ushauri kwa sababu anakaribia kurudi nyumbani Kongo na hataki kwenda na tabia hizo akitamani iishie huku huku alipoipatia.

NI MARADHI

Simulizi ya Shubuli inaonyesha kwamba ana tatizo kujichua ili kujiridhisha. Tendo la kujichua limezoeleka mno kwa wanaume wakati wanawake hawatajwi kwenye tabia hiyo.

Kwa yule ambaye anajiuliza kujiridhisha ni nini, hiki ni kitendo cha mtu aidha mwanaume au mwanamke kujichezea huku akivuta hisia za kujamiiana hadi anapofikia kilele.

Ingawa namna ya ufanywaji wake inategemea zaidi na jinsi ya mazoea ya muhusika au namna alivyoingia kwenye mazoea hayo. Wapo wanaotumia vifaa bandia, huku wengine wakijichezea kwa kutumia vifaa halisi kama aina mbalimbali za matunda ambazo zinafanana na kile wanachokilenga ili kutimiza lengo.

Kitendo hiki cha kujichua kipo kwenye kundi la maradhi ya uraibu wa ngono au sex addiction, ambao kundi hilo linajumuisha maradhi mengine yanayofanana na ugonjwa huu ambayo ni kuuza mwili au kufanya kazi za uchangudoa au dada na kaka poa.

Wengine hufanya mapenzi ya usiku mmoja (one night stand), kuangalia picha au video za ngono na kupiga chabo. Mtu yeyote aliye na hali kati ya hizo anaangukia kwenye kundi la uraibu wa kingono. Taarifa mbaya zaidi kwa watu wenye tabia hii ni kwamba kwanza wakishaanza kujihusisha na mazoea haya inakuwa vigumu sana kuacha.

Pia kwenye maradhi yoyote yale ya uraibu, aidha yawe ya ngono au mihadarati mtu anapoanza huwa haamini kama itafika hatua ya kuwa mteja au mtumwa wa hali.

Wengi wao hudhani wanavyoanza kwa urahisi basi huamini itafika muda akichoka kujihusisha na tabia hiyo ataacha, kitu ambacho si kweli sababu ni ngumu mno kuacha na kurudi kwenye tabia yako ya kawaida.

HISIA ZA FEDHEHA

Kingine ni kwamba jamii inachukulia maradhi haya au uraibu huu kuwa ni jambo la aibu lisiloelezeka kwa uwazi hata kumdokeza rafiki yako juu ya mchezo huo.

Mtu anaona ni fedheha kutokana na hilo sasa kinachotokea ni kwamba ‘waamini’ wa mchezo huu wanaendelea kuwa watumwa wa siri hiyo na mwenendo huo kwa maisha yao yote.

Mfano wa simulizi ya Shubuli ni kesi ya mfano inayotuongoza kuangalia tabia ya kujichua kwa wanawake ingawa wanaume wanachukuliwa kuwa ni vinara wa tabia hiyo.

KUTORIDHISHWA

Utafiti uliofanywa nchini Marekani unaonyesha kuwa asilimia 39 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 60 wanaripotiwa kuwa wanajichua ukilinganisha na asilimia 61 ya wanaume .

Kwa mujibu wa utafiti watu wa rika lote wanajihusisha kwa kiasi kikubwa na tabia hiyo lakini vijana ndiyo wahusika wakuu ila kwa wale wenye umri mkubwa au wa kati, huanza tabia hii baada ya kujiingiza kwenye  mchezo wa kuangalia picha za ngono wakiwa peke yao.

Kwa sababu wanachotazama kinahusisha msisimko wa kingono bila kutarajia hujikuta tayari wameshatumbukia katika tabia hiyo.

Sababu nyingine ni kunyimwa, kukosa au kutotoshelezwa wakati wa kujamiiana na  mwenza wao.Ukiangalia sababu hii ndiyo iliyomfanya Shubuli aangukie katika tabia ya kujichua mpaka kufikia hatua ya kuwa  mraibu wa ngono.

Shubuli alikosa kushiriki tendo la ndoa kwa muda mrefu ndiyo maana alitumia njia hiyo.

Vilevile hali hii ndiyo sababu kubwa inayowagusa wanawake wengi walio ndani ya ndoa ambao hawaridhishwi na wenza wao.

Kumekuwa na mazoea na usiri ndani ya ndoa nyingi huku suala la wenza kuridhishana likiwa la upande mmoja tu  wa mwanaume hivyo wanawake wengi kwa muda wamebaki na malalamiko ya kimya kimya ya kutoridhishwa na wenza wao.

Mpaka kufikia hatua ya mwanawake kuamua kuanza kujichua ni ili kutafuta mbadala na kunusuru ndoa zao kwa kuona bora ajichue kuliko kuchepuka au kuomba talaka.

TIBA IPO

 Unapaswa kufahamu kuwa, kujichua kunakufanya uone kuwa umeshapata ‘mteremko’ wa kutimiza haja zako.Ukishafika kwenye hatua hiyo akilini unaanza kupunguza nafasi ya jinsia nyingine katika kutengeneza uhusiano wa kujamiiana.

Kujichua kama maradhi ya uraibu yana matibabu kwenye huduma ya kisaikolojia hivyo kama upo kwenye sintofahamu hiyo hakikisha unakutana na mtaalam na mtaanza matibabu maalum.