Usajili 10 ghali zaidi Man United

26Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili 10 ghali zaidi Man United

MANCHESTER United imekuwa moja ya klabu yenye mafanikio zaidi Uingereza tangu Ligi Kuu ya England ilipoundwa upya mwaka 1992, na hilo limetokana na kuwa na wachezaji wa kiwango bora kabisa waliowahi kucheza hapo.

Klabu kamwe haijawahi kuwa na woga kwenye matumizi ya fedha katika kusajili mchezaji yoyote, na hilo limewasaidia kushinda mataji 13 ya Ligi Kuu pamoja na mengine ya nyumbani na Ulaya.

Huku wakiwa na rekodi nzuri ya kuwakuza wachezaji wao vijana kutoka katika akademi yao na kupandishwa kikosi cha kwanza kama vile Ryan Giggs, Paul Scholes, David Beckham na Marcus Rashford.

Wengine ni wale muhimu ambao wamenunuliwa kwa fedha nyingi na wakafanya makubwa klabuni hapo.

Lakini pamoja na yote usajili gani wa gharama zaidi katika historia ya klabu hiyo?

Soma makala haya uweze kujua;

#10 Juan Mata – Pauni Mil 37.1

Baada ya kukosa nafasi kule Chelsea chini ya kocha, Jose Mourinho, Juan Mata alinunuliwa na David Moyes ili kuisaidia kuimarisha kiwango cha United katika msimu wake wa kwanza hapo Old Trafford.

Ameendelea kuwa hapo hadi leo, lakini hajaweza kuonyesha kiwango cha juu kama alivyofanya kule Stamford Bridge.

Hajawa na nafasi ya kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza hapo kwa mashetani wekundu na ameongezewa mkataba wa miezi 12.

#9 Nemanja Matic – Pauni Mil 40

Mashetani wekundu hao walikuwa na uhitaji mkubwa wa kiungo wa kati mwaka 2017, na Kocha Jose Mourinho akaamua kumsajili Matic kwa pauni milioni 40.

Raia huyo wa Serbia amekuwa na kiwango cha kuvutia tangu alipotua pale Old Trafford na hivi karibuni alisaini mkataba mpya ambao utamweka hapo hadi mwaka 2023.

#8 Bruno Fernandes – Pauni Mil 47

Baada ya kumwania kwa miezi kadhaa, Manchester United hatimaye wakafanikiwa kuipata saini ya Bruno Fernandes.
Man United walikamilisha usajili wa nyota huyo wa kimataifa wa Ureno Januari mkwaka 2020.

Tangu kutua kwake hapo Man United, amekuwa na mchango mzuri kwa timu na amekuwa akilinganishwa na gwiji wa zamani wa United, Eric Cantona.

#7 Fred – Pauni Mil 47

Alikuwa anawaniwa kwa udi na uvumba na majirani zao Manchester City ili kwenda kuongeza nguvu kwenye kikosi chao.

Lakini Fred mwenyewe akaamua kuichagua Man United iliyokuwa chini ya kocha Jose Mourinho na akajiunga na kikosi hicho mwaka 2018.

Alikuwa na wakati mgumu wa kuzoea mazingira katika mwaka wake wa kwanza na nusu hapo, lakini sasa ni mmoja wa viungo muhimu zaidi kwa kikosi cha kocha, Ole Gunner Solskjaer linapokuja suala la mechi kubwa.

6. Aaron Wan-Bissaka – Pauni Mil 50

Baada ya kuonesha kiwango cha kuvutia sana kwa kikosi cha Crystal Palace, huku akionesha uwezo wa hali ya juu, Man United wakalazimika kutumia kiasi cha pauni milioni 50 ili kunasa saini ya mlinzi huyo kijana.

Kiulinzi amekuwa na kiwango kizuri na amekuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho na inaonesha wazi kwamba, ana nafasi kubwa ya kuendelea kung’ara zaidi.

#5 Angel Di Maria – Pauni Mil 59.7

Baada ya kulazimika kuondoka kule Real Madrid, Di Maria alisajiliwa kwa ada ambayo wakati huo iliweka rekodi ya pauni milioni 60 na akapewa jezi namba saba.

Alianza vizuri, lakini baadaye akajikuta akiwa hana nafasi chini ya kocha, Louis Van Gaal, na haraka akaondoka kipindi cha majira ya joto kilichofuata na kuelekea jijini Paris kujiunga na PSG.

#4 Jadon Sancho – Pauni Mil 73

Hili ni dili la hivi karibuni zaidi, Manchester United wamemsajili kijana mwenye kipaji kujiunga na kikosi chao hiyo kwa mkataba wa miaka mitano, akitokea kule kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, katika klabu ya Borussia Dortmund.

Jadon Sancho mwenye umri wa miaka 21 sasa, ameigharimu kiasi cha pauni milioni 73, na anaonekana atakuwa na wakati bora zaidi katika miaka inayokuja hapo Old Trafford.

#3 Romelu Lukaku – Pauni Mil 75

Baada ya kung’ara kule Everton, Manchester United ikalipa pauni milioni 75 ili kumsajili Lukaku hapo Old Trafford wakati kocha Jose Mourinho alipokuwa anaangalia mtu wa kuziba pengo la Zlatan Ibrahimovic.

Lukaku alifunga mabao 27 katika msimu wake wa kwanza, lakini baadaye akawa sio tena chaguo la Mourinho ambaye alifukuzwa na y ye akaenda kujiunga Inter Milan kipindi cha majira ya joto kilichofuata.

#2 Harry Maguire – Pauni Mil 80

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alifanya maamuzi ya kutaka kumsajili beki, Harry Maguire hapo Old Trafford, na alikuwa tayari kufanya lolote linalowezekana.

Klabu hiyo ikatoa kiasi fedha kilichoweka rekodi ya dunia cha pauni milioni 80 kumsajili mlinzi huyo na tangu hapo amekuwa nahodha wa timu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili sasa aliyokaa hapo.

#1 Paul Pogba – Pauni Mil 89

Baada ya kuondoka kama mchezaji huru na kujiunga na Juventus, Pogba alirudi tena klabuni hapo kwa ada iliyoweka rekodi ya dunia kwenye usajili ya pauni milioni 89 mwaka 2016.

Muda wake klabu hapo umekuwa wa kupanda na kushuka kwa kipaji chake, kwani kuna wakati amekuwa na kiwango cha juu akiisaidia timu na wakati mwingine amekuwa katika kiwango kibovu na kutokuwa na msaada kwa timu.

Hivi sasa amekataa kusaini mkataba mpya, huku huu wa sasa unamalizika kipindi cha majira ya joto kinachokuja na huwenda akaondoka akiwa mchezaji huru, kama hatauzwa kipindi hiki cha majira ya joto.