Usajili wa ndani Ligi Kuu Bara 2019/20

24Jun 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Usajili wa ndani Ligi Kuu Bara 2019/20

HARAKATI za usajili kwa klabu za Tanzania zimepamba moto kwa sasa, huku kila klabu ikipita huku na huko kuangalia wachezaji ambao wanaweza kuwafaa kwenye klabu zao kwa msimu ujao wa Ligi Kuu 2019/20 na michuano mingine mbalimbali, ikiwamo ya kimataifa.

Kwa timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kama vile Simba, Yanga, Azam na KMC usajili wa kimataifa ulianza Juni Mosi na unatarajiwa kumalizika Juni 30, huku kukiwa na wiki mbili za ziada ambazo zitakuwa na faini, wiki ya kwanza ikiwa na faini yake na ya pili faini yake ikiwa juu zaidi, lakini pia ikiwa ni ya mwisho kabla ya dirisha kufungwa.

Kwa upande wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), dirisha lao la usajili lilinza Juni 15 na linatarajia kumalizika Julai 15.

Tayari sura mpya zimeanza kuonekana, baadhi ya wachezaji wakianza kutambulishwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu, wengine wakiwa ni Watanzania, baadhi kutoka nje ya nchi, huku wengine wakiwa wageni, lakini wakiwa wanacheza Ligi Kuu nchini Tanzania.

Kwenye makala haya, tutaorodhesha wachezaji wa Ligi Kuu ya Tanzania tu haijalishi wa kigeni au Kibongo ambao wametoka klabu moja kwenda nyingine, lakini zikiwa ni za humu humu ndani. Hawa ni wachezaji tu ambao wametangaza na kutambulishwa rasmi na klabu zilizowasainisha. Wachezaji walioongeza mikataba na klabu zao hawahusiki na orodha hii, sasa shuka nayo...

1. Birigimana Blaise- Namungo FC, kutoka Alliance FC

Usajili wa kwanza kabisa wa ndani kutangazwa rasmi ulikuwa ni wa Bigirama Blaise ambaye ni raia wa Burundi. Sraika huyo ambaye alimaliza ligi msimu uliomalizika akiwa na Aliiance FC, amesaini kuichezea Namungo FC ambayo imepanda daraja msimu huu na itaanza kwa mara ya kwanza kucheza Ligi Kuu.

Klabu hiyo imetangaza kumpa mkataba wa mwaka mmoja straika huyo ambaye amemaliza ligi akiwa na mabao tisa. Matano aliyafunga akiwa na Alliance ambayo alijiunga nayo kwenye kipindi cha dirisha dogo, huku manne akiyafunga akiwa Stand United aliyoichezea hadi katikati ya msimu.

2. Idd Suleiman 'Nado'- Azam FC, kutoka Mbeya City

Mchezaji huyo zao la Ndondo Cup misimu miwili iliyopita akiichezea Manzese United, amejiunga na Azam FC akitokea Mbeya City.

Idd Suleiman maarufu kama Nado ana uwezo wa kucheza kama kiungo mchezeshaji, lakini pia kama winga wa kulia na kushoto. Kwenye Ligi Kuu msimu uliomalizika akifanikiwa kutupia jumla ya mabao manane, na hiyo ikawa ni usajili mwingine wa klabu ya ndani kwenda klabu ya ndani nchini.

 

3. Emmanuel Mvuyekure- Azam FC, kutoka KMC

Azam iliingia tena kwenye soko la ndani la usajili na kumpata straika mmoja matata Emmanuel Mvuyekure raia wa Burundi. Mchezaji huyo alikuwa akiichezea KMC kwenye ligi iliyomalizika na akafunga mabao saba kwa msimu, amepewa mkataba wa mwaka mmoja kwa matumaini ya kuisaidia timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa inayoikabili timu hiyo msimu ujao.

4. Benno Kakolanya- Simba, kutoka Yanga

Kakolanya ni golikipa wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars ambaye kwa muda mrefu alikuwa na mgogoro na klabu yake kiasi cha kutocheza kwa muda mrefu hali iliyosababisha kushindwa kuitwa Stars. Hatimaye Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilimtangaza kuwa yuko huru baada ya Ligi Kuu kumalizika na usajili ulipoanza, Simba ilitoa taarifa ya kumsajili kipa huyo kwa miaka miwili kusaidiana na kina Aishi Manula na Deogratius Munishi 'Dida'.

5. Abdulaziz Makame- Yanga, kutoka Mafunzo

Huyu ni kiungo mkabaji kutoka Mafunzo ya Zanzibar ambaye naye amesainishwa na Yanga kwa ajili kuitumikia klabu hiyo kwa msimu ujao kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa na michuano mingine mbalimbali.

Abdulaziz Makame ni mmoja wa viungo waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar kwenye ligi iliyomalizika.

6. Kennedy Juma- Simba, kutoka Singida United

Msimu uliomalizika alikuwa ndiye nahodha wa Kikosi cha Singida United. Msimu huu amesajiliwa na Klabu ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili. Ni beki wa kati akiwa na uwezo wa kucheza namba nne na tano. Tayari ameshaanza kuitumikia timu hiyo kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Gwambina, mechi iliyochezwa Ijumaa iliyopita. Alimaliza ligi akiwa ameifungia Singida United bao moja.

 

7. Ally Ally- Yanga, kutoka KMC

Klabu ya Yanga imemnasa beki wa kati kutoka KMC ya Kinondoni anaitwa Ally Ally. Ni beki ambaye kabla ya timu hiyo alikuwa akiichezea Stand United.

Alizua gumzo kubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika alipojifunga bao katika namna iliyoshangaza wengi, Yanga ikicheza dhidi ya KMC. Beki huyo amesaini mkataba wa miaka miwili.

8. Mapinduzi Balama- Yanga, kutoka Alliance FC

Ni kiungo maridadi aliyekuwa akiichezea Alliance FC msimu uliomalizika. Alikuwa kwenye msimu mzuri kiasi cha kuwavutia viongozi wa Yanga na kuamua kumpa mkataba wa miaka mitatu kuichezea timu hiyo. Kiungo huyo anamudu kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, mwenye kasi, chenga na uwezo mkubwa wa kutoa pasi za mwisho.

9. Paul Ngalema- Namungo, kutoka Lipuli FC

Katika kuonyesha kuwa imedhamiria kuonyesha makubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, timu ya Namungo imenasa saini ya beki mzoefu Paul Ngalema. Ngalema msimu huu aliichezea timu ya Lipuli, alishawahi kuzichezea Klabu za Ndanda na Simba na zingine kabla ya kujiunga na Lipuli ya Iringa ambayo aliisaidia kufanya vema msimu uliomalizika kwa kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la FA, na nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

10. Miraji Athumani- Simba, kutoka Lipuli FC

Huyu ndiye mchezaji pekee ambaye bado hajatambulishwa na viongozi wa klabu kama wenzake wote, lakini amejitangaza mwenyewe.

Kabla viongozi wa Simba hawajamtambulishwa rasmi, mwenyewe akafunguka na kusema tayari ameshamalizana na klabu hiyo, akitokea Lipuli FC.

"Mpaka nimeamua kusaini Simba, ina maana nimeshamalizana na Lipuli na majina makubwa ya wachezaji wa klabu hiyo hayanitii hofu, nitapambana kwa sababu hakuna ambako hakuna changamoto." Alisema winga huyo ambaye alitokea kwenye kikosi cha pili cha Simba.

Na katika kuthibitisha hilo, Ijumaa iliyopita alicheza mechi yake dhidi ya Gwambina FC tangu ajiunge na Simba.

Habari Kubwa