Usalama barabarani mwaka huu uje na jipya kusaidia wenye ulemavu

03Sep 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Usalama barabarani mwaka huu uje na jipya kusaidia wenye ulemavu

SEPTEMBA ni mwezi ambao masuala ya usalama barabarani hupewa kipaumbele.

Kwa mwaka huu Tanzania inapoadhimisha wiki ya usalama barabarani , ukweli uliopo ni kwamba nchi hii ni moja kati ya nchi barani Afrika inayoongoza kwa ajali kutokana na watumiaji kutozingatia sheria na alama za barabarani.

Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya watu wanaoathirika kwa ajali hizo ni wanaotembea ambao tunawaita watembea kwa miguu.

Barabara nyingi za Tanzania, zinatumiwa kwa ushirika na waendesha magari, pikipiki, bajaji, maguta, baiskeli na wanaotembea wakiwamo watoto, wazee na walemavu.

Kwa barabara zilizowekwa njia za wapita kwa miguu, wafanyabiashara ndogo ndogo wamezivamia na kueguza kuwa sehemu yao ya kufanyia biashara.

Eneo mojawapo linalotisha ni Mbezi jijini Dar es Salaam ambako hapapitiki, kila mmoja amekaa barabarani, akiuza bidhaa bila kujali kuwa kuna magari, wanaotembea na pikipiki.

Wajasiriamali wameweka migongo barabarani, hawaogopi wala kuhofia gari ama yeyote anayekuwa nyuma yao. Wiki ya usalama barabarani ishughulikie kero hizo zinazoongeza uwezekano wa vifo na ulemavu.

WALEMAVU
Watu wenye ulemavu wa viungo, wakiwamo wa kutoona, wapo kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na ajali kutokana na kukosa njia zao zitakazowawezesha kupita kwa usalama.

Idara ya watu wenye ulemavu Zanzibar ni kati ya vyama vya watu wenye ulemavu, inayotoa kilio baada ya kuona madereva wengi hawajui matumizi ya fimbo nyeupe, kwa watu wenye ulemavu wa macho na kuhatarisha usalama wa maisha yao.

Mwanasheria wa Idara hiyo, Ruwaida Shaaban Khamis, mwaka jana aliwahi kuzungumzia suala hilo akisema watu wenye ulemavu wa macho wanalazimika kutembea na wasaidizi barabarani ili kulinda usalama wao.

Wadau wa usalama barabarani mwaka huu waangalie jinsi ya kuwasaidia na kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara hasa madereva, wanapaswa kufahamu umuhimu wa fimbo nyeupe.

Watu wenye ulemavu wa macho, huwasababishia kuingia gharama ya kuwalipa wasaidizi wanao waongoza barabarani, lakini kama kungekuwa na mipango mizuri ya matumizi ya barabara, watu hao wangekuwa wanatembea bila hofu ya kugongwa.

Inaelezwa kuwa tangu magari yanayotumia gia za ‘automatic’ yalipoanza kuingia kwa wingi nchini, kila mtu amegeuka kuwa dereva na baadhi yao huanza kuingia barabarani bila kuwa na leseni ya udereva.

Kutojua sheria na alama za barabarani, kimekuwa chanzo kikubwa cha ajali za barabarani.

Watu wanaojiita madereva kwa kuendesha magari bila kwenda kwenye shule za udereva na kupata leseni, wanadaiwa kuongoza kwa kusababisha ajali za kizembe barabarani.

Wenye ulemavu wa macho walikuwa na uwezo wa kutoka nyumbani wenyewe na kwenda katika harakati za maisha bila ya kuwa na msaidizi kwa kutumia fimbo nyeupe, lakini kutokana na ongezeko la magari, maisha yao yamekuwa katika mazingira ya hatari.

Tafsiri ya ulemavu iliyo katika Sheria ya Watu wenye ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010, haitofautiani na tafsiri iliyoko kwenye mkataba wa kimataifa unaomaanisha mtu binafsi kukosa au upungufu wa fursa za kushiriki katika shughuli za kijamii katika kiwango sawa na wengine kutokana na maumbile, akili, au sababu za kijamii;

Mwanasheria huyo anasema, pamoja na Mkataba wa utoaji wa Haki kwa watu Wenye Ulemavu (2006), huduma za jamii lazima ziwe rafiki kwa watu wenye ulemavu, lakini bado majengo ya umma na barabara zinazojengwa nchini hazina huduma rafiki kwa watu wenye ulemavu na kuwapa wakati mgumu.

Wakati barabara zinapopanuliwa hasa Morogoro ujenzi uangalie namna ya kuwapa njia maalumu watu wenye ulemavu ambao ni waathirika wa kila huduma inayotolewa nchini.

Kwa mfano hawawezi kutumia vyoo kutokana miundombinu yake kutokuwa rafiki . Leo ukiingia kwenye vyoo vya umma kwenye vituo vya basi hakuna huduma kwa ajili ya kundi hili wala watoto.

Baadhi ya misingi ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za watu wenye ulemavu ni: Kuheshimu utu wa mtu, uhuru wa mtu binafsi ikiwa pamoja na uhuru wa kuchagua anachokitaka, na uhuru wa watu; Kutokubagua; Kushiriki kikamilifu na kuingizwa katika jamii;

Kuheshimu tofauti na kukubaliwa kwa watu wenye ulemavu kama sehemu ya upana wa binadamu na ubinadamu na usawa katika kupata fursa.

Licha ya baadhi ya barabara kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu, bado huduma wanaotembea na fimbo nyeupe, huishia kuzigonga biashara au kujikwaa.

Watu wenye ulemavu wa viungo pia hawajatengewa huduma yao na badala yake hulazimika kujichanganya na watu wasiokuwa na ulemavu tofauti na nchi zingine zilizoendelea, zinazozingatia haki za watu wenye ulemavu.

Baadhi ya barabara zimejengwa kwa kutozingatia vivuko vya watu wenye ulemavu, hali inayoonyesha watu hao kutengwa katika jamii.

Madereva wawapo barabarani, hata wakiona mtu mwenye ulemavu, hawatoi msaada wa kumruhusu kupita, kutokana na kutojua sheria za barabarani.

Vyombo vya usafiri wa umma nchini pia havijazingatia haki za watu wenye ulemavu kwa kuwatengea viti vyao maalumu na badala yake hupata msaada kutoka kwa wasamaria wema.

Ni jukumu la vyombo husika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa haki zao za msingi kama walivyo binadamu wengine. Kila mtu duniani ni mlemavu mtarajiwa.

Iwapo ndani ya magari yaendayo haraka waliyoyaunda wamewakumbuka walemavu na kuwatengea viti ni wakati pia kwa daladala nyingine kuweka eneo la wenye ulemavu na pia serikali kuweka miundombinu ya barabara ya kuwasaidia kwani nao wana haki na stahili ya kuwa na huduma hiyo.

Vyama vya kuwatetea wenye ulemavu viiwajibishe serikali wakati huu wa maadhimisho ya wiki ya usalama barabarani , wasingojee tena kwa sasa itoshe kusema kuwa yanahitajika mabadiliko kuwasaidia wenye ulemavu.

Habari Kubwa