Ushirika mpya unavyokomboa uchumi Wanashinyanga, Geita na pamba yao

30Jul 2021
Shaban Njia
Dar es Salaam
Nipashe
Ushirika mpya unavyokomboa uchumi Wanashinyanga, Geita na pamba yao
  • Mazao yanauzwa bei juu, kiwanda chafufuka

VYAMA vya ushirika nchini hadi kufikia miaka ya 1990, vilionekana kunawiri kiuchumi, hata kubeba haiba ya baadhi ya nchi kuja kujifunza Tanzania, kuihusi namna ya kuviendesha.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Emmanuel Charahani, akizungumza kabla ya kukabidhi malipo ya pili kwa wakulima wa zao la pamba kutoka halmashauri za Ushetu, Msalala, Nyang’hwale na Kishapu. PICHA: SHABAN NJIA.

Katika orodha ya vyama vigogo nyakati hizo, inajumuisha Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (NYANZA), Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera (BCU), Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) na Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Kahama (KACU).
 
Hivyo, ni baadhi ya vyama vya ushirika vilivyoonekana kukua kwa kasi kipindi hicho, ikiwa ni zao la ubora katika wa uongozi wa vyama hivyo, kwa maslahi ya wakulima wake na hivyo kuwainua kiuchumi kupitia mazao waliyouza.
 
Mkoani Kagera, Chama Kikuu cha Ushirika (BCU) kilikuwa kikifanya kazi kwa karibu sana na wakulima wa ndizi, pamoja na wa Kahawa waliokuwapo katika maeneo hayo, huku mkoani Kilimanjaro.

Pia, Kanda ya Ziwa, KACU ilikuwa na wakulima wa Tumbaku na Pamba, kama ilivyo kwa SHIRECU.

Kuwapo kwa vyama hivyo, kulijenga uaminifu mkubwa kwa wakulima katika eneo husika, walioviamini vyama vyao wakuza mazao yao katika eneo hilo husika, hata ikaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakulima.

MWANZO KUFILISIKA
 
Kadri siku zinavyosonga, vyama vya ushirika viliisha nguvu kutokana na viongozi wengi kutokuwa waadilifu, hata kuelekea hatua ya kufilisika.
 
Ulifika wakati viongozi wa vyama hivyo, nao walipata mwanya kujilimbikizia mali kupitia mazao yaliyolimwa na vyama husika vilididimia kwa kiasi kikubwa wakikosa uaminifu wa kuuza tena mazao yao kupitia ushirika.
 
Hata hivyo, serikali katika awamu iliyopita ikaanza tena kuona umuhimu wa kuufufua ushirika, ulioonekana kukosa nguvu baada ya wakulima kutosa imani na viongozi wake, waliokuwa wakijali nafsi zao.
 
Ni namna iliyosababisha baadhi ya vyama vya hivyo vya ushirika vikubwa na vingine vikiangukia madeni makubwa na ndio tatizo kubwa kwa vyama hivyo ikachukua nafasi.
 
Serikali baada ya kuona ushirika unaelekea kuanguka, mathalan mkoani Shinyanga na jirani yale Mkoa wa Geita, iliamua kuelekeza nguvu kufufua baadhi ya viwanda vya pamba vilivyokufa.

Marejeo hai ni katika Kiwanda cha kuchakata Pamba cha KACU cha mjini Kahama na MBCU kilichohudumia wakulima wa Wilaya za Mbogwe na Bukombe, mkoani Geita.
 
MWENYEKITI KACU

Emmanuel Charahani, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilayani Kahama (KACU), anasema chama hicho kwa sasa kimejidhatiti kuhakikisha kinarudia zama zake, kwa kununua pamba za wakulima na kisha wanazichakata.
 
Anasema, KACU ilichaguliwa kama eneo la majaribio kwa ajili ya kuunua pamba na mbegu kutoka kwa wakulima, inaichambua katika kiwanda chao kilichopo katika ofisi zake, Mhongolo, katika Manispaa ya Kahama.
 
Anasema, kiwanda hicho kilisimamisha uzalishaji  kwa muda mrefu  tangu mwaka 2013, sasa serikali ndio imeamua kufufua viwanda  vya ushirika na ndipo kiwanda hicho kikachaguliwa kuwa eneo la mfano wa majaribio kwa msimu wa mwaka 2019/2020.
 
Anasema katika ufufuaji huo, KACU ilikopa Sh. bilioni 4.6 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na katika fedha hizo, walitumia Sh. bilioni 3.1 kwa ajili ya kukarabati   mitambo na majengo, pia gharama za ununuzi na uchakataji pamba.
 
Charahani anasema, kwa masimu wa mwaka 2019/2020 wamefanikiwa kununua kilo za pamba milioni 2.2, mbegu zenye thamani ya Sh. bilioni 2.049, kutoka kwa wakulima wa Halmashuri za Ushetu, Msalala, Kahama Mji, Nyang’wale na Kishapu.
  
Anaendelea kusema kuwa jumla ya kilo milioni moja za mbegu zenye thamani ya Sh. milioni 550 ziliuzwa kwa kampuni na kilo 311,200 zenye thamani ya Sh. milioni 171.1 ziliuzwa kwa Bodi ya Pamba, jumla ya na kufanya jumla ya mauzo ya mbegu  kuwa Sh.Milioni 721.1.
 
Charahani anasema kuwa, ushirika huo ulilipa fedha zote kwa benki TADB  nakufanya  KACU kumaliza deni kwa asilimia 100.
 
MAFANIKIO/CHANGAMOTO
 
Kuhusu mafanikio ya chama, Charahani anasema wamekarabati na kufufua shughuli za kiwanda zilizokuwa zimesimama kwa miaka saba.

Pia, ni hatua iliioinua bei ya pamba kutoka kwa mkulima, Sh.810 iliyolipwa na kampuni binafsi, hadi kufikia Sh. 920 za sasa.
 
Anasema, kuna baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni pamoja na uchache wa mbegu ya pamba iliyozalishwa hasa wilayani Kahama anaongeza, ni hali inayotokana na  kuwapo mvua nyingi katika, kuzidi mahitaji ya zao pamba shambani.
 
Charahani anasema, kutokana na hali nzuri ya uzalishaji wa kiwanda hicho mali ya ushirika, imeweza chake imesababisha chama hicho kutoa malipo ya pili kama bonasi kwa wakulima wake Sh. milioni 90.9 waliogawiwa wakulima katika Halmashauri za Ushetu. Kishapu, Kahama Manispaa, za Mslala na Nyang’wale, mkoani Geita.
 
MKAGUZI MKUU
 
Mkaguzi Mkuu wa Vyama vya ushirika Mkoa wa Shinyanga lodrick Kilemile anasema kuwa, Chama cha KACU kimekuwa kikifanya kazi zake vizuri na kwamba kutoa malipo ya pili kama Bonas kwa wakulima wake ni jambo la kuigwa na vyama vingine kwani haijawahi tokea.
 
Anasema ushirika zamani ulikuwa na sura ya ‘kunufaisha matumbo ya watu’ hali ambayo kwa sasa ina mabadiliko makubwa, kwani mkulima sasa anaona faida ya kuwapo chombo hicho.
 
Kilemile anasema busara ya kimenejimenti ni kwamba, inapaswa kuwaeleza mapato na matumizi wakulima katika katika maeneo ili wanachama hao kuwa na imani na ushirika wao.
 
DC NA BODI PAMBA
 
Michael Ntunga, ni Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, anashauri ni bora kujiunga na vyama vya ushirika ili kuongeza mnyororo wa thamani wa pamba yao wanayouza katika vyama vya ushirika,
 
Anasema kuna wakulima wameuza pamba yao katika vyama vya ushirika, lakini wao binafsi hawapo katika unachama wa ushirika, hali ambayo kwa sasa inapaswa kubadilika wajiunga katika vikundi hivyo cha uchumi na maendeleo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyamaganda Taraba, anasema Wilaya ya Kishapu ni sehemu isiyo na viwanda katika Mkoa wa Shinyanga na anamuomba Mwenyekiti wa KACU kuona umuhimu wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata pamba mahali hapo, ili kuinua uchumi wao.
 
Anapasifu kuwa pana miundombinu bora ya barabara, hali ya hewa nzuri inayofaa kilimo cha pamba na anaongeza kwamba wakati umefika sasa kwa Wilaya ya Kishapu kubadilika kupitia zao hilo, ambalo ndilo dhahabu nyeupe ya Kanda ya Ziwa.