Ushirikiano wa Nyerere, Mao Tse Tung kuibuliwa sekta ya mawasiliano

02Sep 2016
Gwamaka Alipipi
Dar es salaam
Nipashe
Ushirikiano wa Nyerere, Mao Tse Tung kuibuliwa sekta ya mawasiliano

UHUSIANO baina ya Tanzania na China unazidi kupanuka miaka na miaka na sasa urafiki huo unazidi kusambaa na kugonga hodi katika nyanja ya habari na mawasiliano.

Ni uhusiano ulioasisiwa na marais wa kwanza wa mataifa hayo katika miaka ya 1960, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mao Tse-Tung wa China.

Hadi sasa Watanzania wanajivunia mengi, ikiwa na ujenzi wa reli ya Tazara, miradi ya viwanda kama vile cha nguo –Urafiki nk.

Urafiki wa mataifa hayo mawili, yalijikita katika sekta mbalimbali, zikiwamo biashara, ulinzi na viwanda. Lakini kwa sasa, unazidi kusambaa katika sekta nyinginezo kama vile mawasiliano.

Mnamo Agosti 9 mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo wa Tanzania, Nape Nnauye na Mkurugenzi wa Idara ya Habari China, Zhao Quizheng walipozungumza katika Kongamano la Kidiplomasia baina ya China na Afrika lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Wote walieleza mipango iliyopo baina ya mataifa hayo mawili katika kuendeleza sekta ya habari na mawasiliano.

Ni kongamano lililowakutanisha hivi karibuni maofisa mbalimbali wa kiserikali wapatao 20, kutoka nchi zaTanzania, China, Kenya, Afrika Kusini, Morocco na Nigeria.

Maofisa hao, mbali na kujadili namna ya kushirikiana katika kupanua sekta ya mawasiliano, pia walibadilishana maoni na kujadiliana kuhusu namna ya kukabiliana na fursa na changamoto zilizopo.

Katika uhusiano huo, wenye mtazamo‘Ndoto ya China’ na ‘Ndoto ya Afrika’ katika kipindi kipya cha maendeleo.

Waziri Nnauye anasema ushirikiano baina ya China na Tanzania, ulizidi kuimarika katika miaka ya 1990 na kwamba vyombo vya habari vinawajibu wa kukuza ushirikiano huo.

“Ipo haja ya kuimarisha ushirikiano wa vyombo vya habari vya China na Afrika, ili kudumisha ushirikiano uliokuwapo tangu zamani. Sisi na Wachina ni ndugu,” anasema Nnauye.

Anasema China imekubaliana na Tanzania kuleta uzoefu wao katika nyanja ya mawasiliano.

Pia, China pia inatarajia kuimarisha ushirikiano na wananchi wa Afrika, katika sekta nyinginezo kama vile afya katika kipengele cha upatikanaji dawa.

Nnauye kupitia kongamano hilo, anasema vyombo vya habari vya Afrika, vina wajibu wa kueneza mazuri yaliyopo katika bara hilona kuondoa dhana potofu iliyojengwa nabaadhi ya mataifa, kuhusu Afrika.

Nnaoe anasema kuwa, katika ushirikiano wa miaka yote kati ya China na Tanzania, nchi hizo mbili zimejifunza mengi katika kuimarisha ustawi wa wananchi wake na daima kumekuwapo utashi wa kuimarisha uhusiano huo, kuenzi jitihada za waasisi wa ushirikiano huo.

“Ni wakati mwafaka kuongeza jitihada za kuimarisha uhusiano na ushirikiano wetu kuwaenzi waasisi wa ushirikiano huu - Rais Mao Tse Tung na Mwalimu Julius Nyerere,” anasema Nnauye.

BALOZI WA CHINA

Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youqing, anasema kuwa ushirikiano wa China na Tanzania katika sekta ya mawasiliano, kutaongeza na kupanua wigo wa ufanyaji biashara na teknolojia.

Anasema ushirikiano kati ya China na Tanzania ulianza na urafiki huo ni muda wa mrefu katika masuala ya maendeleo.
Balozi Lu anasema urafiki wa China na Tanzania, siku zote umekuwa msingi mkuu wa uhusiano wa China na Afrikana ndicho kinachoongoza katika uhusiano wa China na Tanzania.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari wa China, Zhao Quizheng, anasema serikali ya China na wabia wao wa Afrika, wanapaswa kushirikiana na asasi za kiraia, ili kukuza uchumi wa nchi zao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China na Rais wa Chama cha Kidiplomasia cha Watu wa China, Li Zhaoxing, anasema katika karne ya 21, inahitaji zaidi ushirikiano wa kidiplomasia baina ya nchi na nchi.

Anasema ushirikiano wa China na nchi za Bara la Afrika kwa sasa ni muhimu katika kupanua uchumi wa nchi husika na kubadilisha maisha yao.

Anasema teknolojia ya mawasiliano katika Bara la Afrika ikikua, itasaidia upatikanaji kirahisi wa huduma nyingi.

Mkurugenzi wa Redio ya China (CRI), Hu Bangsheng, anasema kupitiaCRI, China itashirikiana na vituo vingivya redio barani Afrika, ili kubadilishana ujuzi na uzoefu.

“Baadhi ya Redio na vituo vya televisheni kutoka Bara la Afrika na China, vitaweza kushirikiana katika kubadilishana ujuzi wa msauala ya habari. Hiyo yote ni kuhakikisha undugu unakua,” anasema Bangsheng.

Katika kongamano, China ilitangaza kutoa msaada wa Sh. milioni 45 kusaidia upatikanaji madawati kwa shule za sekondari na msingi katika mkoa wa Dar es Salaam, jambo ambalo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alishukuru.

Mwezi Desemba mwaka jana, kulifanyika mkutano mkubwa kuhusu ushirikiano wa China na Tanzania, huko nchini Afrika Kusini.

Habari Kubwa