Ushwahiba ulivyong’oa rais Park madarakani

15Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ushwahiba ulivyong’oa rais Park madarakani

WIKI iliyopita ilikuwa mbaya na chungu kwa Rais wa Korea Kusini, Park Geun hye, baada ya Mahakama ya Kikatiba kutoa uamuzi wa kuufikisha mwisho utawala wa Rais huyo.

Park Geun hye alishtakiwa na Bunge la nchi hiyo na ilitokana na mgogoro wa kisiasa uliolitikisa taifa hilo la Asia kiasi cha kusababisha maandamano yasiyo na kikomo.

Bunge lilimshitaki Park mwezi Desemba kwa kutumia vibaya madaraka na ufisadi baada ya mamilioni ya watu kuandamana wakimtaka rais huyo ajiuzulu kufuatia kashfa mbalimbali za ufisadi na rushwa.

Uamuzi huo uliofikiwa na jopo la majaji wanane wa Mahakama ya Kikatiba ambao hauwezi kukatiwa rufaa unamaanisha Korea Kusini itafanya uchaguzi katika kipindi cha miezi miwili ijayo kumchagua rais mpya.

Inamaanisha pia Park, mwanamke wa kwanza kuwa rais nchini humo anakuwa kiongozi wa kwanza kuondolewa madarakani baada ya kushitakiwa na Bunge, kupoteza kinga ya rais iliyokuwa ikimlinda dhidi ya kufunguliwa mashitaka.

Jaji Mkuu wa mahakama hiyo ya kikatiba Lee Jung Mi amesema vitendo vya Park vilihujumu vibaya sheria na demokrasia.

Urafiki wamchongea

Park mwenye umri wa miaka 65 alikutwa na hatia ya kuvunja sheria kwa kumruhusu rafiki yake Choi Soon Sil kuingilia masuala ya kitaifa na kukiuka sheria kuhusu shughuli za utumishi wa umma.

Park anadaiwa kuficha uingiliaji huo uliofanywa na Choi na hata kuwashutumu walioyaibua madai hayo.

Kwon Seong Dong mbunge na mwanachama wa Kamati ya Bunge ya mashitaka amesema uamuzi huo wa Mahakama unathibitisha kuwa kila mtu ni sawa mbele ya sheria, hata rais.

Park ambaye ni binti wa kiongozi wa zamani wa kiimla aliyeungwa mkono na jeshi la nchi hiyo aliingia madarakani mwaka 2012 baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa kidemokrasia.

Uamuzi waligawa taifa

Watu wawili wameripotiwa kufariki dunia katika maandamano ya umma baada ya kutangazwa kwa hukumu hiyo. Waziri Mkuu wa Korea Kusini ambaye pia ni kaimu rais Hwang Kyo ahn amefanya mkutano na Baraza la Mawaziri na kutoa wito wa utulivu na uthabiti baada ya hatma iliyomfika Park.

Lakini mfumo wake wa uongozi wa kuonekana kujitenga, kukumbwa na kashfa chungu nzima, na ugumu wa kiuchumi na kijamii ulisababisha umaarufu wake kushuka sana na mamilioni ya Wakorea Kusini waliandamana wakitaka ajiuzulu au aondolewe madarakani.

Kulingana na kura za maoni, karibu asilimia 77 ya raia wa nchi hiyo waliunga mkono kuondolewa madarakani kwa kiongozi huyo.

Aliomba radhi mara kadhaa kwa athari za kashfa hizo lakini alikanusha madai yote ya kuwa alifanya makosa alipowasilisha taarifa yake kwa mahakama mwezi uliopita.

Swahiba wake wa karibu aliyemuingiza matatani Choi Soon Sil, tayari anakabiliwa na mashitaka.

Marekani imesema inatarajia kuwa na uhusiano mzuri na kiongozi ajaye wa Korea Kusini. Ubalozi wa Marekani nchini humo umesema Korea Kusini itaendelea kuwa mshirika wa karibu na kuongeza wanaheshimu maamuzi ya nchi hiyo.

Waendesha mashitaka nchini humo wanasema wanaamini Rais Park Guen-hye alikula njama na mshirika wake mkubwa, ambaye alitumia urafiki wake huo kujipatia utajiri mkubwa usiokuwa na maelezo.

Taarifa hizo zinakuja wakati waendesha mashitaka hao wakimtia hatiani rasmi rafiki na mshirika huyo wa muda mrefu wa Rais Park, Choi Soon-sil, kwa tuhuma za kuingilia masuala ya kiserikali na kuzilazimisha kampuni kutoa mamilioni ya dola kwa mifuko aliyokuwa akiiendesha.

Mwishoni mwa mwaka jana waendesha mashitaka pia waliwatia hatiani wasaidizi wengine wawili wa zamani wa Rais Park, ambao wanashukiwa kushirikiana na Choi katika njama hizo.

Choi mwenyewe ni binti wa kiongozi wa kundi moja la kidini, ambaye kabla ya kifo chake alikuwa akimfundisha Rais Park na ambaye alikuwa akimchukulia kama "shujaa" wake.

Kiongozi huyo wa kwanza mwanamke wa Korea Kusini amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa, akidaiwa na wapinzani wake kuwa anaihujumu demokrasia.

Choi Soon-sil amefunguliwa rasmi mashitaka ya ufisadi kwa kujipatia na kuzitumia nyaraka za serikali kwa maslahi binafsi licha ya kuwa yeye hana nafasi yoyote serikalini.

Polisi inasema maandamano ya hivi karibuni yalihudhuriwa na watu 170,000 karibu na Baraza la Mji na lango kuu la kasri kwenye mji mkuu, Seoul, ingawa waandaaji wa maandamano hayo wanasema waliohudhuria ni watu 500,000.

Waandamanaji wengine walipita kwenye mitaa iliyo karibu na ofisi za rais, huku wakibeba mishumaa na kuwasha simu zao, wakipiga mayowe:

"Park Guen-hye achia madaraka" na "Mkamateni Park Guen-hye!"

Mbali na kashfa ya kujipatia na kutumia nyaraka za siri za serikali kujinufaisha binafsi, Choi anatuhumiwa pia kutumia ukaribu wake na Rais Park kuwapatia watoto wake elimu ya juu kinyume na taratibu.

Siku ya Ijumaa, Wizara ya Elimu ya nchi hiyo ilikitaka Chuo Kikuu cha Wanawake cha Ewha kumfutia usajili binti wa Choi aitwaye Yoora Chung, baada ya kugundua kuwa chuo hicho kilikiuka taratibu zake katika kumpokea binti huyo.

Hivi karibuni kabla ya hukumu kutolewa, upinzani ulitumia wingi wao bungeni kupitisha sheria ambayo inamruhusu Mwendesha Mashitaka maalumu kuchunguza kashfa zinazomuandama Rais Park na kuyaweka hadharani maovu yaliyotendwa na kiongozi huyo.

Habari Kubwa