Usuluhishi, maridhiano muarobaini mlundikano kesi mahakamani

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Usuluhishi, maridhiano muarobaini mlundikano kesi mahakamani

NI wakati wa Watanzania pamoja na mawakili kubadilika ili kukuza na kuendeleza usuluhishi badala ya kung’ang’ania utaratibu wa kawaida wa kusikilizwa mashauri mahakamani hadi kumalizika hata itachukua miongo mingi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi (Mediation Centre), Rose Teemba.

Ni ushauri wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi (Mediation Centre), Rose Teemba, katika mahojiano jijini Dar es Salaam hivi karibu na kuonya kuwa utaratibu wa kusikiliza kesi mwanzo hadi mwisho unawapotosha wananchi kwa kuona kuwa haufai.

Anasisitiza kuwa mawakili wanatakiwa kubadili mtazamo na kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa usuluhishi kwani una faida nyingi, gharama ndogo na huokoa muda.

FAIDA
Anasema unapofanikiwa ndiyo mwisho wa shauri na Jaji msuluhushi huandaa tunzo ‘decree’ ambayo ina hadhi kama ile inayotokana na utaratibu wa usikilizaji wa shauri la madai na wahusika hupewa nakala ya tunzo.

Aidha anabainisha kuwa husaidia kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani, hujenga mahusiano mazuri baina ya wadaawa kwa kuwa Wadaawa hao wanakuwa wametengeneza hukumu yao wenyewe.

“Usuluhishi hupunguza gharama za uendeshaji wa kesi za madai na vilevile huokoa muda. Badala ya wadaawa kufika mahakamani kila wakati na kwa muda mrefu kusikiliza kesi, usuluhishi huchukua saa au siku chache mpaka kufikia mwafaka” anafafanua Jaji Teemba.

“Suala la usuluhishi ni takwa la katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107A, inayosomeka, katika kutoa maamuzi ya mashauri ya madai, kwa kuzingatia sheria, mahakama zitafuata kanuni …kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro.’

USULUHISHI NI NINI?
Ni hatua mojawapo katika mwenendo wa kesi za madai ambapo wahusika katika kesi chini ya usaidizi wa usuluhishi Jaji au Hakimu Msuluhishi, wanajadiliana kukubaliana, kuafikiana na kumaliza mgogoro wa shauri lao kwa namna wanavyoona inafaa bila ya kulazimika kuingia kwenye uendeshaji wa kesi hiyo ya madai kwa kutoa ushahidi mahakamani.

Au ni mchakato wa majadiliano ya kujaribu kumaliza mgogoro wa madai kwa maafikiano ya ridhaa ya kila mdaawa.

“Katika kutekeleza ibara hiyo ya katiba, Mahakama ya Tanzania imeanzisha kituo maalum, na kwa kuanza hushughulikia mashauri yanayoanzia Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, ambayo ina kesi nyingi za madai” anasema .

Dar es Salaam ilichaguliwa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya kesi na kwamba Kituo cha Usuluhishi kinashughulika na usuluhishi wa mashauri ya madai yanayohusika na ambayo yapo tayari kwa usuluhishi.

“Baada ya hati za madai kukamilika kuwasilishwa mahakamani, shauri linatakiwa lipelekwe kwa msuluhishi kuwasuluhisha wadaawa na kwa kawaida usuluhishi unatakiwa ndani ya siku 60,” anafafanua Jaji Teemba.

Katika usuluhishi wahusika wa shauri husika au wadaawa, mawakili wao kama wapo, Jaji Msuluhishi hutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wahusika wanaafiki kufikia suluhu timilifu.

Moja ya mbinu wanazotumia ni pamoja na kuwaweka wadaawa katika vyumba maalum ‘Break out Rooms’ kila upande peke yake kwa ajili ya tafakuri ya kina kuhusu majadiliano ili kufikia suluhu.

Anaongeza kuwa wadaawa wanapofikia suluhu, hupatiwa nakala ya makubaliano yao kwa pamoja ambayo husainiwa na pande zote za mgogoro au kesi pamoja na mawakili wao kama wapo na mwishoni inasainiwa na Jaji Msuluhishi.

Pia, Jaji huandaa tunzo inayoendana na makubaliano yaliyofikiwa pamoja na utekelezaji wake ambao huwapatia wenye kesi na mawakili wao kama wapo. Endapo usuluhishi ukishindikana unakuwa mwisho wa shauri lenyewe.

“Usuluhishi ukikamilika na kufaulu wadaawa hupatiwa hati ambayo lazima ionyeshe tarehe ya makubaliano, mhuri wa kituo cha usuluhishi ikionyesha namba ya shauri na majina ya wahusika na mambo yote waliyokubaliana, makubaliano hayo yataonyesha maeneo yote ya maafikiano na utekelezaji wa makubaliano,” anafafanua Jaji Teemba.

Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi Saidi Ding’ohi, anasema licha ya kituo hiki kuanzishwa, usuluhishi pia hufanyika katika Mahakama Kuu, za Wilaya na za Mahakimu Wakazi.

Tofauti ni kwamba kwenye mahakama nyingine hakuna jaji au hakimu mahususi anayeshughulika na usuluhishi pekee, jaji au hakimu msuluhishi anakuwa na mashauri mengine ya kusikiliza.

Ding’ohi anasema kituo hiki kina jukumu la kupambana na mlundikano wa mashauri kwa kasi kama ilivyo katika mahakama nyingine za ngazi mbalimbali na kwamba baada ya kikao cha Majaji Wafawidhi kilichofanyika Arusha Septemba 2017 iliazimiwa kuwa kusikiliza na kumaliza kesi zote za muda mrefu kiwe kipaumbele.

Kituo hiki pia kilitekeleza agizo hilo na kuweka mikakati ya kushughulikia mashauri yaliyowasilishwa kwa ajili ya usuluhishi kwa haraka zaidi. Kwa mujibu wa Naibu Msajili usuluhishi ukifanyika mapema huondoa kukwamisha hatua nyingine za usikilizaji mashauri kupunguza mlundikano.

Ding’ohi anaongeza kuwa katika vikao hivyo mashauri 34 yalipangwa kwa ajili ya kusuluhishwa.“Lengo tulilo nalo ni kuhakikisha kuwa yote 34 yaliyokuwepo yawe yamefanyiwa usuluhishi hadi kufikia Novemba 22 sambasamba na yale yatakayokuwa yanaingia. Kipaumbele kuondoa ,” anasisitiza Ding’ohi.

Naibu Msajili anasema hadi Oktoba, 2017 mashauri 170 yalipokelewa kwa ajili ya usuluhishi kati ya hayo 37 yalifaulu kusuluhika.

Akitoa takwimu za kesi zilizowasilishwa kituoni hapo tangu kuanzishwa kwake Julai 2015 mpaka Oktoba 2017, Ding’ohi anasema jumla ya mashauri 504 yalipokelewa kutoka Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam. Yaliyosuluhishwa kati ya hayo ni 485 ambayo ni asilimia 96 ya mashauri yote yaliyopokelewa.

“Kati ya mashauri 485 yaliyosuluhishwa, 112 usuluhishi wake ulifanikiwa ambayo ni sawa na asilimia 23 ” anaongeza na kwamba yaliyofaulu kwa kiwango fulani (partly successful) yalikuwa ni sita kwa kipindi hicho hicho ambayo ni asilimia moja na ambayo usuluhishi ulishindikana yalikuwa 367 sawa na asilimia 76.

“Kufikia Oktoba, 2017 yalibaki mashauri 19 sawa na asilimia nne na kwamba yanayoshindikana kusuluhishika hurudishwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ili kuendelea na utaratibu wa kawaida wa usikilizaji wa kesi,” anaeleza Ding’ohi.

Akiongelea kwa undani kuhusu Kituo cha Usuluhishi, Ding’ohi anasema kilianzishwa Julai 1, 2015 ili kufanya shughuli zote za usuluhishi katika mashauri ya madai. Lengo ni kuwa na jaji mahususi ambaye jukumu lake ni kuendesha usuluhishi pekee.

“Kituo kinafanya usuluhishi kwa mashauri yanayoanzia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam pekee. Ufanisi wa kituo hiki unaweza kusambaa huduma za kituo kwa Mahakama Kuu nchi nzima, ingawa usuluhishi unaendelea kufanyika katika mahakama zetu zote.”

Nancy Mosha, wakili wa kujitegemea, anasema usuluhishi ni muhimu katika mustakabali mzima wa kuhakikisha kupungua kwa mlundikano wa kesi mahakamani na vilevile husaidia kupunguza muda wa kusikiliza kesi kwa pande zote.

“Usuluhishi ni mzuri kwa sababu hufanyika kirafiki na maridhiano yanayofikiwa yanakubalika na pande zote mbili bila kinyongo,” anasema Mosha na kuongeza kwamba ni njia sahihi ya kumaliza migogoro baina ya wadaawa, hivyo kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa umma ili utambue faida zake.

Mohamed Hamis Mtulia, amehusika kwenye utaratibu wa maridhiano anasema ni mzuri na uboreshwe na kuongeza kuwa jukumu la maridhiano ni la pande zote mbili.

“Binafsi nasema kwamba chombo hiki ni kizuri kwani maamuzi yanafikiwa kwa maridhiano ya pamoja hivyo ni muhimu kuheshimu usuluhishi, tusiogope maridhiano,” anaeleza Mtulia.

Mdaawa mwenza waliokuwa na kesi na Mtulia, Charles Mallya anasema kuwa usuluhishi unasaidia kupunguza muda wa kwenda mahakamani kufuatilia kesi hivyo kuna haja ya kuelimisha umma juu ya kituo hicho ili wananchi wakitumie ipasavyo.