UTAFITI: Pesa chafu na simu za mkononi ni hatari kwa afya yako

25Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
UTAFITI: Pesa chafu na simu za mkononi ni hatari kwa afya yako

PESA chafu na simu za mkononi zinaweza kuwa hatari kubwa kwa afya yako, watafiti wanaonya.

Wanasayansi wanasema pesa hususani zile za thamani ndogo, zinasababisha magonjwa mengi ya kuhara miongoni mwa watu wanaotumia chakula kinachoandaliwa kwenye maeneo ya hoteli, migahawa na vilabu.

WANAOANDAA CHAKULA

Utafiti uliofanywa miongoni mwa waandaaji 395 wa chakula katika maeneo 15 tofauti ya Jiji la Nairobi, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Jomo Kenyatta na kile cha Teknolojia nchini Kenya (JKUAT), kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Tiba ya Kenya (Kemri), na Kitengo cha Utafiti wa Matibabu cha Jeshi la Marekani nchini humo.

Unabainisha kwamba wanaoshughulikia chakula cha umma kwa ujumla wanapaswa kuhamasishwa juu ya hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na kugawa chakula baada ya kushika pesa au simu za mkononi.

Utafiti huo unaonyesha kuwa kwa sababu pesa na simu za mkononi huwa hazisafishwi, hugeuka kuwa maficho ya vimelea wa magonjwa ambao husababisha sumu kwenye vyakula.

Baada ya kupima sarafu kuanzia shilingi moja hadi noti ya shilingi 1,000 zinazotumiwa jijini Nairobi, ripoti ilifichua kuwa sarafu za shilingi 5, 10, 20 ndizo zilizokuwa chafu zaidi, zikifuatiwa na noti za shilingi 50, 100 na 200.

“Nyingi kati ya pesa pamoja na simu zilikuwa na bakteria wanaosababisha magonjwa.”

Matokeo ya utafiti huo yaliwasilishwa kwenye mkutano wa saba wa afya na sayansi wa Afrika Mashariki, uliofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania mwezi Machi.

Na kibaya zaidi utafiti huo unasema ni kwa wahudumu wa vyakula, hususan wanaogawa vyakula kwa wateja pamoja na wapishi ambao ilibainika kuwa hawazingatii usafi na hasa baada ya kupokea simu zao za mkononi.

Wakati wa utafiti huo, washiriki 34 walipatikana na magonjwa tofauti kama vile kikohozi, kichomi na maumivu ya tumbo na utumbo (gastroenteritis).

Si kwamba magonjwa haya yanasababisha matatizo tu kwa wagonjwa, bali ni magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa mwandaaji wa chakula, anayegawa chakula au mpishi wa chakula anayeumwa.

Aidha, ilibainika kuwa asilimia 60 ya waliofanyiwa utafiti hawakuwa wamenawa mikono yao baada ya kupokea simu za mkononi.

Kwa kawaida, waandaaji wa chakula hawapaswi kupokea simu.

“Wanaoshughulikia chakula cha umma kwa ujumla hawana budi kuhamasishwa juu ya hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na kugawa chakula baada ya kushika pesa au simu za mkononi,” unaonya utafiti.

Mnamo mwaka 2009, Taasisi ya Utafiti wa Tiba nchini Kenya (Kemri), ilifanya utafiti sawa na huo jijini Nairobi na kugundua kuwa simu za mkononi zina vimelea wa magonjwa kwa kiasi kikubwa, baadhi zikiwa hata na vimelea wanaopatikana kwenye kinyesi.

MACHINJIO HATARI ZAIDI

Nyingi kati ya pesa zilizopatikana na vimelea zilikuwa ni sarafu zilizochukuliwa kutoka kwenye machinjio, zikifuatiwa na zile zilizokusanywa kutoka kwa wauzaji wa mahindi kando ya barabara na vyakula vinavyouzwa kwenye maduka madogo (vioski).

Kwa mujibu wa Dk. Richard Korir, Ofisa wa Utafiti katika Kituo cha Kitengo cha Utafiti wa Makrobailojia na mwandishi wa utafiti huo, kutofuatwa kwa kanuni ya kuosha mikono na usafi kwa ujumla kunasababisha kuhamishwa kwa vimelea hawa wa magonjwa kwenda kwenye chakula ambacho bila shaka kinaliwa.

Utafiti huo ulifanywa na kuwasilishwa na mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kilimo (JKUAT) ambaye aliangazia aina mbalimbali za bakteria wanaopatikana katika mazingira, chakula, utumbo na ngozi kwa wanyama na binadamu.

SIMU ZA MKONONI ZINA MAAMBUKIZI ZAIDI

Ingawa vimelea vingi vya bakteria hawa si hatari, baadhi wanaweza kusababisha magonjwa kama vile homa ya matumbo, sumu ya chakula na maambukizi ya ngozi.

“Shilingi 1,000 ndiyo yenye maambukizi ya chini kwa sababu hutumiwa mara chache, huku sarafu ya shilingi moja ikiwa pia haina uchafu mwingi na thamani yake imeshuka kwa hiyo haitumiwi sana,” anabainisha Dk. Korir.

Sarafu zenye thamani ya chini ndizo zilizokutwa na uchafu mwingi kuliko zile zenye thamani ya juu.

Vimelea waliopatikana zaidi walikuwa ni wa jamii ya staphylococcus, wanaofahamika kusababisha maambukizi ya ngozi, moyo na mifupa, sumu ya chakula, kichomi na sumu ya mwili wa binadamu.

Bakteria waliopatikana katika chakula pia ni jamii ya Escherichia Coli (E. coli), ambao hupatikana katika mazingira ya chakula, utumbo wa binadamu na wanyama.

Wengi kati ya vimelea hao si hatari, lakini wanaweza kukufanya uwe mgonjwa.

La kushangaza ni kwamba, Dk. Korir anasema, zikilinganishwa na sumu za pesa, simu za mkononi ndio mbaya zaidi inapokuja katika suala la maambukizi ya magonjwa.

“Watu wengi hawadhani kuwa simu ni chafu au ni chanzo cha kuambukizwa magonjwa… kwa hiyo, mara nyingi hawazingatii usafi baada ya kuzitumia,” anasema.

Simu ziligundulika kuwa na bakteria 12 baada ya kukusanywa na kuchunguzwa na zaidi bakteria aina ya Staphylococcus, ambao mara nyingi hupatikana katika nywele na ngozi.

Kutofuatwa kwa kanuni ya kuosha mikono na usafi kwa ujumla kunasababisha kuhamishwa kwa vimelea hawa wa magonjwa kwenye chakula, umebaini utafiti. BBC

Habari Kubwa