UTAFITI: Pombe chanzo kikuu aina 7 za saratani

05Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
UTAFITI: Pombe chanzo kikuu aina 7 za saratani

PENGINE si habari njema kwa wanywaji pombe nchini, lakini ndiyo ukweli wa taarifa za utafiti zinavyobainisha.

Pombe imetajwa kuwa kinywaji kinachosababisha aina saba za saratani na watu wanaoitumia hata kwa kiwango kidogo, wanajiweka katika hatari ya kuugua ugonjwa huo.

Hayo yatokanayo na matokeo ya utafiti mpya, ambao ripoti yake ilitolewa mwishoni mwa mwaka jana.

Wataalamu wa afya nchini Uingereza, waliidhinisha matokeo ya utafiti huo na wakatoa ushauri kwa serikali nchini kuanzisha kampeni zaidi ya elimu kwa wananchi, kuwafungua macho jinsi pombe na saratani zinavyohusiana kwa karibu.

Aidha, utafiti umeamsha wito unaotolewa mara kwa mara, ukiwataka wahamasishwe kutumia pombe siku zisizo za kazi, au mwishoni mwa wiki.

Sambamba na hilo, kuna pendekezo kuwa chupa za pombe na vifungashio vingine vya vinywaji kuwa na tangazo lenye onyo kuhusu hatari ya unywaji pombe.

Uchambuzi mpya wa ushahidi uliokusanywa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, unaihusisha pombe na saratani ya titi, ini na zinginezo.

Utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Sayansi linalohusiana na mambo ya ulevi, unahitimisha kwamba kuna uthibitisho wa takwimu kati ya pombe na saratani.

Kwa mujibu wa Jennie Connor, kutoka Idara ya Kinga na Tiba ya Jamii, ya Chuo Kikuu cha Otago nchini New Zealand, kuna ushahidi wa kuaminika kuhitimisha kwamba, unywaji pombe ni chanzo cha moja kwa moja cha ugonjwa huo,

“Kuna ushahidi usio na shaka kwamba, pombe inasababisha saratani kwenye maeneo saba ya mwili na pengine katika maeneo mengine pia,” anasema Connor na kuongeza:

“Hata, bila ya kuwapo kwa maarifa kamili ya kibailojia ya namna pombe inavyosababisha saratani, ushahidi wa ugonjwa huo unaweza ukathibitisha matokeo yanayoonyeha kwamba, pombe inasababisha saratani ya koo, mapafu, ini, titi, utumbo na zingine.”

Connor anasema, ushahidi unaendelea kuonyesha kwamba, pombe inaaminika kuwa chanzo cha saratani ya ngozi, kibofu na kongosho.

POMBE YACHANGIA ASILIMIA NNE YA VIFO

Anasisitiza kuwa, hatari ya kupata ugonjwa huo kwa mnywaji inaongezeka kulingana na kiasi cha pombe anachokunywa, kwani kadri mtu anavyokunywa nyingi, ndio anavyokabiliwa na hatari zaidi.

Connor alifikia hitimisho hilo, baada ya kuchambua mapitio ya matokeo ya utafiti uliofanywa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na Mfuko wa Utafiti wa Saratani wa Dunia (World Cancer Research Fund).

Mfuko huo ni Wakala wa Utafiti wa Saratani, ambacho ni chombo cha Shirika la Afya Duniani (WHO), pia mbia wa mashirika mengine ya afya.

“Hatari kubwa inawahusu wanaokunywa pombe kupitiliza, ikilinganishwa na wale wanaokunywa kwa kiwango kidogo,” anasema Connor.

Hivyo anashauri kuwa, kampeni ya kupunguza unywaji pombe inapaswa kumhamasisha kila mtu kupunguza unywaji, kwani inawalenga wanywaji sugu, si njia mwafaka ya kupunguza saratani zinazosababishwa na pombe.

MGANGA MKUU
Mnamo Februari mwaka jana, Prof. Dame Sally Davies, ambaye ni Mganga Mkuu wa Uingereza, alizua taharuki alipowatahadharisha wanawake nchini humo kwamba, unywaji pombe unaweza kusababisha saratani.

Prof. Davies aliiambia Kamati ya Bunge la Uingereza kuwa:“Wanawake wanapaswa kufanya kama ninavyofanya mimi wakati ninapochukua glasi yangu ya mvinyo.”

Anafafanua:“Wanapaswa kufikiria kwanza kabla ya kunywa, ikiwa wanahitaji glasi ya mvinyo au wanahitaji kujiongezea hatari ya kukumbwa na saratani ya titi. Mimi huwa ninachukua uamuzi kila wakati ninapokunywa glasi ya mvinyo.”

Prof. Davies ametoa mchango mkubwa katika kuandaa mwongozo mpya wa serikali, kuhusu kiwango cha unywaji salama kilichochapishwa mwanzoni mwa mwaka jana.

Mwongozo huo ulipendekeza wanaume wapunguze unywaji wao wa pombe kwa wiki, kutoka uniti 21 hadi 14, kipimo ambacho wanawake wanashauriwa kutokizidisha.

WATAALAMU WA SARATANI
Ofisa Habari za Afya wa Kituo cha Saratani cha Uingereza, Dk. Jana Witt, anafafanua: “Tunajua kwamba, watu tisa kati ya 10, hawana habari za uhusiano uliopo kati ya pombe na saratani, na taarifa hii ni kumbukumbu tosha kuwa kuna ushahidi mzito unaoviunganisha vitu hivyo viwili.”

Utafiti wa hivi karibuni ulioendeshwa na Taasisi ya Saratani ya Uingereza (CRUK), uligundua kuwa pale watu walipoonyeshwa orodha ya saratani mbalimbali, ni mmoja tu kati ya watano aliyejua kwamba, saratani ya titi inaweza kusababishwa na unywaji pombe.

Hiyo ni ikiliinganishwa na watu wanne kati ya watano (Asilimia 80), walikuwa wakijua kwamba pombe inasababisha kansa ya ini.

“Kuwa na siku za kutokunywa pombe kila wiki, ni njia nzuri ya kupunguza kiwango cha pombe,” anashauri Dk. Witt na kuongeza:

“Pia, mtu ajaribu kuweka nyumbani kwake vinywaji laini ama vile vilivyo na kiwango kidogo cha kilevi, na siyo rundo la vilevi.”
Profesa wa Bailojia na Kemia kutoka Chuo Kikuu cha London, Alan Boobis, anasema, sayansi iliyoonyesha mchango wa pombe kwa ugonjwa wa saratani, imejengwa vizuri.

“Sasa ugumu mkubwa ni kuwasiliana kwa tija na umma juu ya suala hili,” anadokeza msomi huyo kuhusu changamoto iliyo mbele yake.

SIGARA NA POMBE
Utafiti wa Connor, pia uligundua kwamba watu wanaovuta na kunywa pombe kwa wakati mmoja, ndio walio katika hatari kubwa ya kuugua saratani.

Ili iligunduliwa kwamba, wanywa pombe walioacha wanakuwa kwenye usalama zaidi dhidi ya uwezekano wa kupata saratani na kuwa wanapoacha moja kwa moja, wanajiweka salama zaidi kwenye hatari hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Pombe cha Drinkaware, ambacho kinajitolea kutoa elimu husika nchini humo, Elaine
Hindal, anakiri kuwa unywaji pombe na saratani una uhusiano wa karibu sana.

“Unywaji wa mara kwa mara unaozidi mwongozo wa serikali wa kiwango kilicho salama cha pombe, unamuweka mtu kwenye hatari zaidi ya kuugua aina tofauti za saratani,” anasema.

“Aidha, unywaji wa aina hiyo unaweza kuongeza hatari ya kuugua magonjwa ya moyo na ini, kiharusi na kongosho.” Anafafanua zaidi Hindal.

Kuhusu sigara, anasema kuwa uvutaji wa sigara na unywaji pombe kwa pamoja, unaongeza hatari ya kupata saratani ya koo na mdomo na mtu anapotumia kimojawapo, madhara yake yanakuwa tofauti.

Anashauri watu wanaokunywa pombe zaidi ya mwongozo uliotolewa na serikali, wanapaswa kupunguza kiwango ili kulinda afya zao za baadaye.

Habari Kubwa