UTAFITI: Upungufu wa mbegu za kiume unahatarisha maisha

11Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
UTAFITI: Upungufu wa mbegu za kiume unahatarisha maisha

WANAUME wenye mbegu chache za kiume wako katika hatari ya kupata magonjwa kwa mujibu wa utafiti mpya.

Utafiti uliofanyiwa wanaume 5,177 ulibaini kwamba wanaume wenye mbegu chache za kiume wana mafuta mengi mwilini, shinikizo la damu na mafuta machafu katika mishipa ya damu.

Pia wana uwezo mkubwa wa viwango vidogo vya homoni za kiume.

Waanzilishi wa utafiti huo wanasema kuwa, wanaume wenye mbegu chache za kiume ni muhimu wakafanyiwa vipimo vya magonjwa mengine.

Hivi karibuni nchini Tanzania, kumeshamiri matangazo mbalimbali rasmi na yasiyo rasmi kuhusiana na dawa za asili haswa za kuongeza nguvu za kiume.

Miongoni mwa dawa hizo ni dawa ya 'Ujana' ambayo kazi yake ni kusaidia kuongeza nguvu za kiume.

Dawa zingine zikiwa Sudhi, Vatari, IH Moon na Coloidal Silver ambazo kazi yake ni kudhibiti vimelea mbalimbali.

Baraza la dawa nchini humo limesema hatua hii imekuja baada ya uchunguzi wa kina uliofanywa na kubaini kuwa dawa hizo hazina madhara kwa afya ya binadamu, hivyo hawana budi kuzikubali.

Aidha, Paul Muhame ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa dawa za asili nchini Tanzania anasema baada ya baraza kupitisha vigezo vyote vilivyohitajika kutoka katika dawa hizo, mamlaka ya dawa na chakula pia imethibitisha hilo.

“Suala la muhimu ambalo tumeliangalia zaidi ni usalama wa mtumiaji…katika upande wa kuthibitisha kuwa dawa hizo zinaponyesha au la, linabaki kwa mnunuaji na mtumiaji wa dawa hiyo,” anasema.

HATARI

Upungufu wa mbegu za kiume na matatizo ya ubora wa mbegu hizo ni masuala yanayoathiri mmoja kati ya wanandoa watatu kushika mimba kulingana na utafiti huo uliofanywa nchini Uingereza.

Lakini katika utafiti huu mpya wanasayansi walichanganua wanandoa wasioweza kupata watoto nchini Italia, kujua iwapo ubora wa mbegu hizo pia unaathiri afya ya mtu kwa jumla.

Waligundua kwamba wanaume wengi walio na mbegu chache walikuwa na matatizo kadhaa ya kiafya ikiwamo mwili ulionenepa na shinikizo la damu.

Hatua hiyo huongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya moyo na kiharusi.

Wanaume hao pia walionekana kuwa na viwango vya juu vya kuwa na homoni chache za kiume ambazo hupunguza ukubwa wa misuli na mifupa na huenda vikasababisha ugonjwa wa kudhoofika kwa mifupa.

Daktari Albert Ferlin ambaye aliongoza utafiti huo anasema:

“Wanaume wasio na rutuba hukumbwa na matatizo ya kiafya ambayo yanaweza kuhatarisha hali yao ya maisha na kupunguza kiwango cha maisha wanayoishi,” anaongeza:

“Rutuba huwapatia wanaume fursa isiyo ya kawaida ya kutathmini afya na kuzuia magonjwa.”

Hata hivyo, wamiliki wa utafiti huo wanasisitiza kuwa utafiti wao haukuthibitisha kuwa ukosefu wa mbegu za kiume za kutosha husababisha matatizo ya kimetaboliki badala yake ni vitu viwili vinavyohusiana.

Wanasema kuwa uhaba wa homoni za kiume huhusishwa na matatizo haya ya kiafya.

Dk. Ferlin anasema kuwa utafiti unaonyesha ni muhimu kwa wanaume wanaotibiwa matatizo ya ukosefu wa rutuba kuangaziwa vizuri kimatibabu.

“Wanaume walio na matatizo ya kuwapatia mimba wake zao wanafaa kukaguliwa vizuri na kufuatiliwa na wataalam wao wa rutuba kwa sababu huenda wana viwango vya juu vya kupata maradhi na vifo,” anasema.

Hata hivyo, uthibitisho wa dawa za asili nchini Tanzania umezua mjadala mkali katika vipindi vya radio nchini humo haswa kwa upande wa serikali kuthibitisha dawa za nguvu za kiume kuuzwa kihalali.

BBC iliweza kupata maoni mbalimbali kutoka kwa Watanzania kuhusiana na uthibitisho wa dawa hizo:

“Watu watazinunua lakini hakuna mtu atakuwa na uhakika kwamba dawa hizi zinatibu, sana sana atabahatisha tu,” anasema Thomas Hemed, mkazi wa jiji la Dar es Salaam na kuongeza:

“Inaweza isilete madhara, lakini huwezi kujua baadaye…kiukweli inabidi ziangaliwe kwa watu maalum kwa watu wanaouza ili mtu akidhurika ajue ataenda kwa nani.”

SABABU ZA KUKOSA NGUVU ZA KIUME

Sababu za kukosa nguvu za kiume zinaainishwa kuwa ni pamoja na magonjwa (kisukari, saratani), msongo wa mawazo na kutumia aina fulani ya dawa kwa mfano dawa za kudhibiti msukumo wa damu (BP)

Pia umri mkubwa, kukosa usingizi wa kutosha na matatizo ya kihomoni. BBC

Habari Kubwa