Utafiti: Usalama wa tovuti nchini ni mdogo

24May 2016
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Utafiti: Usalama wa tovuti nchini ni mdogo

TOVUTI ni mkusanyiko wa kurasa zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali za tarakilishi katika mfumo wa kieletroniki, ambazo kwa pamoja hujumuika kutoa habari, maelezo ya jambo ama suala fulani.

Programu maalum hutumika katika kusoma kurasa na kutafsiriwa kupitia mtandao na mifumo ya kisasa kwa lugha inayoeleweka kwa urahisi na wingi wake huitwa ni ‘tovuti’.

Matumizi ya tovuti ni makubwa nchini. Hii inatokana na kukua kwa kasi kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) hapa nchini.

Teknolojia hii imerahisisha mawasiliano, kutoka katika eneo moja hadi jingine kwa haraka zaidi bila kujali umbali.

Utafiti uliofanywa naTume ya Sayansi Tanzania (COSTECH) kuanzia August 2015 hadi Machi mwaka huu kuhusu ‘Hali ya Usalama kwa Tovuti za Tanzania na Athari za kuvuja kwa Taarifa’, imebanika kuwa tovuti nyingi si salama nchini.

Kati ya tovuti 258 zilizofanyiwa utafiti, 201 sawa na asilimia 77, zilibainika kuwa si salama kutokana na namna zilivyotengenezwa, kwa sababu hakuna ufuatwaji wa kanuni na kufanya ziwe dhaifu. Mtafiti katika Masuala ya Usalama wa Mawasiliano, Geofrey Kilimba anasema kuna virusi vya kijasusi vinaweza kusambazwa katika tovuti hizo.

Hali hiyo anasema kuwa, inasababisha kuibiwa kwa taarifa na kuharibu mfumo mzima katika kompyuta, kutoa siri za faragha kwa watumiaji binafsi wa tovuti, hivyo kuhatarisha usalama wa ndani ya nchi.

Anaeleza kwamba, utafiti uliofanyika kwa koindi hicho umelenga kubaini hali ya usalama mdogo katika tovuti na taarifa zilizopo katika mitandao nchini, ili kupata ufumbuzi wa haraka na kulinda mawasiliano katika tovuti. “Kwa sasa ‘cyberspace’ la Tanzania lina madhara na halina usalama na kwamba tovuti nyingi sio salama.

Zinaweza kushambuliwa muda wowote na wahalifu wa kimataifa hata kusababisha taarifa kuvuja au kudukuliwa kwa lugha nyingine,” anasema Kilimba. Kilimba anasema, kwa sasa suala la matumizi ya tovuti katika taasisi za serikali na binafsi kwa taasisi zote lina nafasi kubwa.

Kuna mfumo wa kifedha unaotumiwa pamoja na taarifa za siri katika mfumo wa kibenki na nyinginezo. “Kama tunavyofahamu hivi sasa taasisi nyingi za kibenki zinatumia mifumo hii, hata za serikali huwa zinaweka mambo kadhaa ambayo ni mawasiliano yao ya ndani, sasa yakiingiliwa mawasiliano haya, husababisha kuvuja kwa taarifa,”.

Anasema kinachotakiwa ni kubadili mfumo wa ufundishaji wa tovuti vyuoni, kwani mtaala uliopo katika vyuo vikuu upo katika tovuti, hivyo elimu itolewe namna ya kutengeneza tovuti kwa njia za kiusalama zaidi, ili kulinda mawasiliano.

Kwa nini matumizi ya tovuti?. Wataalamu wa masuala ya tovuti nchini na duniani kote wanatambua umuhimu wa matumizi ya tovuti yanayoelezwa kuwa yanarahisisha mawasiliano. Mkurugenzi wa Extreme Web Technologies, Mohsin Sumar anasema tovuti kwa upande wa matumizi ya kibiashara, hutumika kutoa taarifa kuhusu biashara ya mtu kwa muda wa saa 24 hata kama hayupo katika eneo la biashara.

Anasema tovuti ni kama ofisa mauzo asiyelala, anayekesha saa zote na wiki nzima kwa kutoa taarifa muhimu kuhusu biashara yako, inajishughulisha na nini, kazi za hivi karibuni, bidhaa zinazopatikana pamoja na maoni kutoka kwa wateja biashara kufahamika.

Pia tovuti kwa mujibu wa mtaalamu huyo humuwezesha mtumiaji kufanya mauzo na kuwasaidia wateja kumpata mfanyabiashara kwa urahisi.

“Kadri siku zinavyokwenda ndio jinsi ambavyo imekuwa rahisi kwa watu kupata taarifa mikononi mwao, kuwapo kwa simu za kisasa zinazowawezesha watu kutumia chombo cha kutafutia vitu yaani ‘search engine’,” anasema.

Anabainisha, kwa wastani wa sekunde moja watu 40,000 hufanya maulizo yao kwenye mtandao kupitia vyanzo mbalimbali vilivyo katika ‘Google’.

Anasema kwa saa 24 kuna maulizo bilioni 3.5, huku kwa mwaka ikiwa ni maulizo na trilioni 1.2, na kwamba fursa hiyo ya maulizo kutoka kwa watu mbalimbali hutumiwa na washindani kuonyesha namna wanavyozidiana na kujitangaza.

Anasema gharama za kutangaza kwa haraka zaidi kupitia tovuti ni ndogo ukilinganisha na njia nyingine za matangazo zinawashawishi washindani na kila wapaotangaza kupitia magazeti, anuani ya tovuti huwashawishi wateja kuangalia tovuti kupitia gazeti.

Habari Kubwa