UTAFITI WA MADAKTARI BINGWA: Nusu ya mimba zisizopangwa Kanda ya Ziwa

07Apr 2016
Elizaberth Zaya
Dar
Nipashe
UTAFITI WA MADAKTARI BINGWA: Nusu ya mimba zisizopangwa Kanda ya Ziwa

Kwa mwanamke mkazi yeyote, dhana ya kupata mimba ni ya kawaida sana.

Mimba si ya kawaida, iwapo imepatikana katika mazingira yasiyo kawaida, kama vile umri mdogo au haikupangwa. Hapo ndipo inapoelezwa ‘mimba isiyotarajiwa.’

Ili kukabiliana nayo, kuna njia nyingi zinazopendekezwa ambazo zimepewa jina la uzazi wa mpango. Hizo ni pamoja na kufunga uzazi kupitia njia nyingi na kutuimia kinga katika tendo la ndoa.

Suala hilo la kukabiliana na uzazi wa mpango ni mtambuka na linashikiliwa kwa kiasi kikubwa na mambo kadhaa, kama vile utashi wa wahusika, elimu, mazingira, utamaduni na upatikanaji wa huduma husika.

Hiyo ndiyo inayotawala kiwango cha athari katika maeneo husika, jamii moja ikionekana kuwa na kiwango kikubwa cha athari kulinganisha na kingine.

HALI ILIVYO TANZANIA
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi ya Guttmacher, Tanzania iko katika kiwango cha juu kimataifa katika vifo vya wajawazito ambao ni 410 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa.

“Utoaji mimba usio salama unachangia zaidi ya theluthi mbili ya wanaolazwa hospitalini kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba na takriban robo moja ya vifo vya uzazi,” inaeleza taarifa hiyo.

Taasisi hiyo inalaumu sheria nchini, kwamba Sheria ya Makosa ya Jinai inaidhinisha utoaji mimba katika kuokoa maisha ya mwanamke, lakini haijaweka wazi namna ya kulinda afya ya mwanamke huyo.

UTAFITI WAIBUA MAMBO
Utafiti uliofanywa kwa ubia na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu(NIMR), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili(Muhas) na Taasisi ya Kimarekani iitwayo Guttmacher, mwaka 2013 ulibaini Kanda ya Ziwa inaongoza kwa utoaji mimba zisizo salama nchini.

Takwimu za utafiti wa Guttmacher, zinafafanua kwamba Kanda ya Ziwa inaongoza kwa asilimia 51 ambayo ni sawa na matukio 120,857 ya mimba.

Sababu za kuwepo kiwango hicho kikubwa cha utoaji mimba, inalezwa kuwa kuna kiwango kidogo sana kitaifa katika matumizi ya uzazi wa mpango, huku kukiwapo mahitaji makubwa ya ngono katika jamii hiyo.

Nyanda za Juu Kusini, ndiyo inayofuata kwa kuwa na matukio ya mimba 68,910 zilizotolewa, ambazo ni sawa na asilimia 47 ya mimba zote.

Kanda ya Magharibi ina asilimia 44 ya matukio hayo yenye mimba 59,565; Kanda ya Kaskazini ina mimba 51,965 ambayo ni sawa na asilimia 31.

Pia, Kanda ya Kati kuna matukio ya mimba 23,465 ambazo ni sawa na asilimia 28; Kanda ya Kusini mimba 21,923 ambayo ni sawa na asilimia 27; Mashariki mimba 54,655 sawa na asilimia 24,
Zanzibar ndiko kwenye kiwango kidogo kitaifa kwa kuwa na asilimia 11 pekee, ikihusisha mimba 3,714.

Sababu inayotajwa na asasi ya Guttmacher ni kwamba wanawake wa Zanzibar wanaanza kushiriki ngono wakiwa na umri mkubwa na wameolewa.

Mtafiti Profesa Andrea Pembe, kutoka Muhas anasema utafiti huo imebaini kila mwaka mwaka kuna mimba zisizotarajiwa moja na kati yao, mimba 405,000 ambazo ni sawa na asilimia 39 hutolewa katika mazingira yasiyo salama na kwa usiri.

Anasema takriban theluthi mbili ya mimba hizo zinazotolewa huendana na madhara ya kiafya kwa kukosa matibabu sahihi, inayoendana na vifo vya wanawake 1,500.

Profesa Pembe anasema Chama cha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake(Agota) wamekuwa wakikumbana na matukio mengi ya namna hiyo.

Anasema katika majukumu yao, ama mtu mmoja mmoja au Agota kama chama, wamekuwa wakikumbana na matukio mengi ya wanawake kutoa mimba katika mazingira hatarishi.

MAPENDEKEZO
Profesa Pembe anasema chama chake kinapendekeza serikali iwe na mkakati maalum wa kuwapatia matibabu ya haraka kinamama, ili kupunguza vifo vitokanavyo na mimba batili.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Neema Rusibamayila, anakiri udhaifu katika njia zinazopendekezwa katika uzazi wa mpango
Guttmacher yenyewe ina mapendekezo yake ya kutaka kuwerpo makundi yenye mahitaji maalum ya kuzui mimba, akitaja wenye umri kati ya miaka 15 na 49.

“Takriban mwanamke mmoja kati ya watano wenye umri kati ya miaka 15 – 49 nchini Tanzania wanataka kucheleweshwa au kusitisha kuwa na watoto, lakini hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango.

“Kundi hili la wanawake huchukuliwa kama lenye mahitaji yasiyofikiwa na uzazi wa mpango,” inasema Guttmacher katika taarifa yake inayobainisha kuwa mwaka 2013, asilimia 15 ya mimba zote nchini zilitolewa.

“Kwa kutambua utoaji mimba usiokuwa salama ni chanzo kikuu cha vifo vya wajawazito. Serikali ya Tanzania imepanua wigo wa upatakanaji wa huduma baada ya mimba kuharibika katiika muongo mmoja uliopita, lakini mapungufu makubwa bado yapo na wanawake wengi hawapati huduma wanazohitaji,” anasema Mtafiti Mwandamizi wa Guttmacher, Sarah Keogh.

Anaongeza: “Utafiti huu unabainisha mapungufu hayo. Inakusudia kuunda mikakati ya kuhakikisha mwanamke wa Kitanzania anayehitaji, anaweza kupata huduma baada ya kuharibika mimba.”
ends

Habari Kubwa