UTAFITI: Watu waaminifu haswa kuliko tunavyofikiria!

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
UTAFITI: Watu waaminifu haswa kuliko tunavyofikiria!

MIAKA kadhaa iliyopita, mtafiti mmoja “aligawa” vipochi 400 katika maeneo tofauti ya umma kama vile Benki, Kumbi za Sinema, hotelini, mahakamani na kwenye vituo vya polisi katika miji minane ya India.

Watu waliotumwa na mtafiti huyo, waliviwasilisha kwa walinzi wa maeneo hayo au wahudumu wanaokaribisha wageni, wakidai wameviokota njiani.

Baadhi ya vipochi havikuwa na hela na vingine vilikuwa na dola zaidi ya tatu, pesa taslimu.

Kila kipochi kilikuwa na kadi tatu zinazofanana za biashara, zilizo na jina la mwenyewe na anwani yake ya barua pepe, orodha ya vitu alivyotaka kununua na ufunguo.

Siku chache baadaye kundi la watafiti waliojidai kuwa wenye vipochi hivyo walisubiri kupigiwa simu na hao walinzi, kama sehemu ya utafiti wa kubaini kiwango cha uaminifu wao.

Vipochi hivyo vilikabidhiwa kwa wanaume 314 na wanawake 86 katika miji ya Ahmadabad, Bangalore, Coimbatore, Hyderabad, Jaipur, Kolkata, Mumbai na Delhi.

Asilimia 43 ya vipochi vilivyokuwa na pesa viliwasilishwa kwa wenyewe, lakini vile ambavyo havikuwa na hela ni kidogo sana vilivyoripotiwa kupatikana, kwamba ni asilimia 22 tu ndivyo vilivyowasilishwa kwa wenyewe.

Matokeo ya utafiti huu wa kushangaza uliochapishwa hivi karibuni katika Jarida la kisayansi, unathibitisha kuwa watu ni waaminifu kuliko vile “tunavyofikiria.”

Alain Cohn, mtaalamu wa saikolojia ya tabia katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani na ambaye pia ni mmoja wa watafiti hao anasema “Hatukutarajia tulichokiona.”

“Watu wanapojua kuwa huenda wakafaidika kutokana na tabia ya kutokuwa na uaminifu, hamu ya kuficha ukweli inaongezeka… lakini usumbufu wa kiakili unaoandamana na hisia ya kujiona mwizi huwafanya kubadili mawazo, hasa ikiwa hawajazoea kuiba kitu cha mtu,” watafiti wanasema.

Mji wa Kusini mwa India, ulikuwa na kiwango cha chini cha watu walioripoti kuokota vipochi vilivyokuwa na pesa, Bangalore (66%) na Hyderabad (28%).

Mji wa Coimbatore, uliandikisha idadi kubwa ya watu walioripoti kuokota vipochi ambavyo havikuwa na hela (58%), huku mji mkuu wa Delhi, ukiwa na kiwango cha chini cha wale waliorudisha vipochi ambavyo havikuwa na hela (12%).

Watafiti waligundua kuwa wanawake walifurahia sana kuwasilisha vipochi walivyookota, viwe na pesa au la wakilinganishwa na wanaume.

Utafiti wa “kuangusha” kipochi ama vipochi nchini India, ilikuwa sehemu ya utafiti mkubwa wa Kimataifa uliofanywa na watafiti ili kubaini tofauti kati ya uaminifu na maslahi binafsi.

Kati ya mwaka 2013 na 2016, watafiti “waliangusha” jumla ya vipochi 17,000 katika miji 355 ya nchi 40.

Baadhi ya vipochi hivyo vilikuwa na pesa, dola 13.45 za Marekani ambazo zimebadilishwa katika sarafu za nchi husika na kuongezwa kiwango chake kulingana na kiwango cha maisha cha watu wa nchi hiyo.

Miji mitano mikubwa kati ya minane ilishirikishwa katika utafiti huo.

Watafiti walikadiria kuwa watu katika mataifa 38 kati ya 40 watarudisha vipochi vilivyo na hela. (mataifa mawili ambao waleti hazikurudishwa ni Peru na Mexico.)

Lakini kiwango cha pesa kilipoongezwa mara saba zaidi katika waleti hizo na kuangushwa tena katika mataifa matatu, kiwango cha waleti zilizorudishwa kilipanda kwa 18%.

Waleti zilizokuwa na pesa nyingi zilirudishwa kwa kiwango kikubwa Denmark (82%) na kiwango cha chini kutorudishwa ilikuwa (13%).

Switzerland (73%) na China (7%) zilikuwa na kiwango cha juu na cha chini cha kurejeshwa kwa waleti ambazo ziliokotwa bila kuwa pesa ndani.

KUPIMA UAMINIFU WA

MTU NI NGUMU SANA

Utafiti huo ulibaini mambo mengi kuhusu tabia za watu tofauti.

Kwa mfano mlinzi ambaye anasimamia usalama wa jengo fulani India, alitaka ahongwe ili ashiriki utafiti huo.

“Tulifahamu baadaye kuwa hakuwasiliana na mwenye kipochi… katika sehemu nyingine mwanamume tuliyempatia kipochi hicho alisema tumwachie hiyo waleti na kwamba pesa zilikuwa ndani atazitoa kama sadaka ikiwa hatafanikiwa kumpata mwenyewe,” anasema Dk. Zünd na kuongeza:

“Nitaandika barua pepe ikiwa sitapokea mawasiliano yoyote kutoka kwa mwenyewe baada ya kumtaarifu, [Nitawapatia walio na uhitaji], bila shaka hii ni sawa na rushwa.”

Anabainisha kwamba ni jambo la kufurahisha sana kubaini kuwa watu wanakuwa waaminifu zaidi kimataifa ikiwa kitu walichookota kinahusisha pesa taslimu.

“Hilo lilijitokeza sana India na mataifa mengine ya bara Asia,” anasema Dk. Zünd.

UTAFITI HUU UNATUFUNDISHA NINI?

Matokeo ya utafiti huu yanaashiria wazi kuwa, binadamu huwajali binadamu wenzao wawe wanajuana au la.

Ndio maana wengi wao waliripoti kuwa wameokota vipochi. Cha kufurahisha ni kwamba vipochi vingi vilivyokuwa na ufunguo vilirejeshwa kuliko vile ambavyo havikuwa na ufunguo.

Zaidi ya yote, kuna “athari ya kisaikolojia” inayomfanya mtu kujiona kama mwizi.

“Ni rahisi kwa mtu kutojiona kuwa muaminifu akiamua kuchukua kipochi ambacho hakina pesa kwa sababu hajafaidika na lolote. Lakini inakuwa vigumu pesa ikihusishwa katika mjadala huo,” anasema Dk. Zünd.

Vipi wale ambao hawakutoa ripoti kuwa wameokota kipochi?

Wanauchumi wanasema huenda wakawa si watu waaminifu, lakini huenda pengine walikabwa na shughuli nyingi au kusahau kipochi chenyewe.

Uaminifu bila shaka ni sera nzuri ya maisha ya kila mwanadamu. BBC