Utandawazi wa lugha ni chachu ya maendeleo au la?

15Jan 2019
Michael Eneza
Dar es Salaam
Nipashe
Utandawazi wa lugha ni chachu ya maendeleo au la?

MOJA ya masuala ya kijamii yanayotofautisha nchi za Afrika na mataifa mengine duniani ni uwezo wa kuongea lugha mbili, tatu au nne kwa wakati mmoja, na wako baadhi wanazungumza lugha lukuki.

Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed Gharib Bilal (wa pili kushoto), akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya lugha ya Kichina, mmoja kati ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Jamillah Dauda, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya 'Confucius' ya Chuo Kikuu cha Dodoma, ambayo ni maalumu kwa ajili ya kufundishia lugha na tamaduni za Kichina. Kushoto ni aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma, Prof. Idris Kikula. PICHA: MTANDAO

Ni moja ya sifa za Rais Dk. John Magufuli kuweza kusalimia kwa ufasaha na hata adabu za watumiaji wa lugha mbalimbali, wakati haiwezekani kuwa amekaa miaka mitano na kila kabila kubwa au hata dogo hapa nchini.

Ni kielelezo cha mchanganyiko wa lugha na wenye vipaji vya kunasa maneno ya lugha tofauti wakiwa wadogo hawapotezi kipaji hicho maisha yao yote. Ni lugha za kujifunza barabarani au katika familia; ni mazingira ya Afrika zaidi.

Kwa kawaida taifa linajitambulisha kwa lugha inayofahamika na watu wake wote, kwa kuwa kanuni za dunia ya kuwinda mtu unayeongea naye lugha moja tayari una undugu naye, inabaki kuwapo mahusiano ya ukoo, lakini hasa kabila (lugha) tayari ni undugu.

Kwa maana hiyo kile kinachoitwa ukabila kimsingi ni undugu unaoshindana, kuwa upo undugu wa Kitanzania kwa sababu tuna lugha moja, lakini undugu wa kikabila ni wa kina zaidi na ndani ya makabila zipo koo, ambako undugu halisi unathibitishwa, kuacha ule wa kifamilia.

Siyo rahisi kuwaambia watu waache undugu huo wa msingi wa lugha moja katika jamii pana zaidi.

Ndiyo maana undugu katika nchi za Afrika unakuwa na utata kiasi fulani, kwa sababu nchi nyingi zaidi hazina lugha moja ya kitaifa ila ziko lukuki au lugha kadhaa muhimu za kikabila, halafu nchi inaunganishwa kwa lugha ya kikoloni.

Inakuwa si rahisi kusema kuna undugu halisi kati ya wananchi wa taifa kama hilo, kwa sababu lugha kuu wanayozungumza haiwatambulishi kama taifa, ni jina la nchi na mazoea ya kuishi pamoja, hivyo mashindano yao ni lugha ipi ya asili, au kundi lipi la asili litatawala.

Sasa ikitokea kama Nigeria, Sudan, Ethiopia, Afrika ya Kati, Ivory Coast na kwingineko kuwa makabila makubwa yana lugha na dini tofauti, hapo inakuwa 'balaa.'

Ila machafuko kati ya makabila hayategemei lugha kuwa tofauti au hata dini, mfano mmojawapo ni Somalia, ambako wana lugha moja inayotumika nchini kote na wana dini moja - lakini wanafahamiana kwa 'vilugha' vyao na uadui unaweza kuwa mkubwa sawa na kabila jingine.

Ina maana kuwa ufahamu wa lugha moja, mbili au zaidi siyo kielelezo cha uwezo wa kuelewana na watu wengine, kwa kuwa sababu za uelewano au mafarakano ziko kwingine na siyo katika lugha.

Hivyo Tanzania imekuwa na umoja ambao watu wengi wanasema unatokana na kutumia Kiswahili, lakini kwa nini Somalia ishindwe kuwa na umoja na wanayo lugha moja pia?

Nchini Congo (DRC) takriban kila mtu anafahamu Kilingala, ambayo zaidi ni lugha ya kijamii iliyoenea hasa eneo la jiji la Kinshasa na viunga vyake ambavyo vina watu wengi zaidi kwa kukaa pamoja na wanaotoka pande nyingine za nchi kwa haraka hujifunza lugha hiyo ili kurahisisha mawasiliano.

Hata hivyo muungano wa nchi sasa unaanza kujengwa kupitia Kiswahili, kinachowatambulisha 'Wakongomani' katika Afrika Mashariki na kwa matumizi ya lugha hiyo ikichanganyika na Kilingala halafu pia Kifaransa, wanakuwa na 'blend' au 'mkorogo' maalum wa matumizi ya lugha unaowatambulisha kitaifa. Ni vyema zaidi kuliko lugha ya ndani.

Yako maeneo ambako lugha moja kubwa ya kikabila inapoenea inakuwa nyenzo ya kufanya biashara bila matatizo, pale ambapo matumizi yake hayafuriki na kuingiliana na siasa, kwa mfano nchini Nigeria ki-Yoruba kinatumika katika biashara zaidi kwa kuwa kusini mwa nchi hiyo ndiyo maskani ya biashara na wa-Yoruba ndiyo wengi.

Upande wa Kaskazini kwa miaka mingi ulitawala jeshi, licha ya kuwa wengi wa maofisa walikuwa wasomi kutoka maeneo ya Kusini, ikachochea migawanyiko ya jinsi ya kuingilia siasa nchini humo.

Hivi sasa eneo la Kusini ni tulivu kisiasa na kidemokrasia, wakati Kaskazini majimbo hufuata sheria, kulea Boko Haram.

Unaona wazi kuwa ingawa lugha ni chombo cha mawasiliano, kuongezeka kwake miongoni mwa jamii siyo silaha au nyenzo ya kufaulu zaidi katika biashara au siasa, yaani maendeleo au utengamano nchini, iwe ni kwa kuwepo lugha moja tu, au watu wengi kufahamu lugha za wengine.

Ndiyo maana tunaposema kuwa tukienzi Kiswahili inabidi kujiuliza malengo ya kufanya hivyo, kama Kiswahili ni nyenzo halisi ya biashara au elimu, kwa kuwa kuwapo kwa lugha moja ya kutuunganisha si hoja katika maendeleo, ila kuwapo na misingi ya kuzuia mifarakano.

Ni kujua lugha za nje kunakotoa fursa, na siyo ufahamu mzuri wa lugha ya ndani, au za kikabila.

Kwa maana hiyo kukienzi Kiswahili kwa maana ya kutumia muda wa kusoma, kukariri hiki na kile katika Kiswahili, ni bora zaidi mwanafunzi atumie muda wake kusoma lugha nyingine ya kimataifa, na siyo ya kabila la jirani labda kwa ajili ya kufanya utani, mzaha wa aina fulani, kwa mfano JPM anavyosalimu watu kwa lugha takribani 20, bila kuwa na azima ya kufanya mazungumzo yoyote kwa lugha hizo.

Ila ni kipaji kilichomsaidia katika uchaguzi mkuu kwa sababu mtu anayeweza kusalimia kikwetu, tena kwa adabu zinazotakiwa, anakuwa ndugu kwa mbali.

Ni kudhihirisha kuwa anawatambua na hata kama siyo kwa upendeleo hawezi kuwapuuza.

Ina maana kuwa kujua lugha za watu wengine katika mazingira ya ndani ya nchi kunaweza kuwa msaada kwa mtu mmoja au mwingine kuchanganyika miongoni mwa kundi husika la watu hao.

Ni kile wanachoita kwa Kiswahili 'ushemeji,' kuwa mtu anapata maneno mawili au matatu ya kuokoteza katika lugha nyingine, jambo linalotakiwa litokane tu na kuwa na kipaji katika kukutana na watu na kuguswa na lugha yao, na siyo lengo la kusoma au kutafuta maendeleo.

Kusoma na kujifunza lugha kibiashara kunaendana na malengo, na hivi sasa lugha zinazoleta fursa za biashara ni lugha kongwe ya Kiingereza na Kichina kinakuja kwa kasi, siyo nyingine.

Hiyo inawezekana vijana wenye vipaji vya kuelewa lugha walenge lugha hizo na ikiwezekana zile za nchi za jirani kama wanakaa mipakani au wanaona fursa maeneo hayo, huku wakijua kuwa uwezo wa kuongea nao maneno mawili matatu hakubadili tofauti za msingi kati yao na wenyeji.

Tatizo la wageni kuchomewa vibanda vya biashara nchini Afrika Kusini siyo kushindwa kuzungumza Kiingereza au kutofahamu Kizulu, ni wivu tu na dhana kuwa uwepo wao unawanyima fursa vijana nchini humo, waliolelewa katika kulalamikia ubaguzi na siyo kuparamia fursa.

Wakiona mgeni kufaulu biashara, ana rafiki wa kike, mzuka hupanda, watwae mapanga.

Habari Kubwa