Utekelezaji maagizo ya vita ya corona bado tatizo shuleni

06Aug 2020
Happy Severine
Bariadi
Nipashe
Utekelezaji maagizo ya vita ya corona bado tatizo shuleni
  • • Walimu hali halisi imewaelemea
  • Shida kuu ni unawaji na barakoa
  • • Elimu ‘corona nini’ imefanikiwa

JUNI 29 mwaka huu, serikali ilitangaza kufunguliwa shule na vyuo nchi nzima, baada ya kufungwa kwa miezi mitatu, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Serikali ilitoa tahadhari kuwa bado ugonjwa huo upo na lazima taasisi zote shule na vyuo vya elimu vifuate masharti yanatolewa na wataalamu wa afya, kujikinga na ugonjwa huo.

Pia, kabla vyuo na shule kufunguliwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, zilitoa miongozo ya namna ya kujikimu kiafya.

Baadhi zilihusu hatua zitakazotakiwa kuchukuliwa na asasi hizo za kielimu, kama tahadhari za kujikinga kuenea au kupata ugonjwa huo.

Waziri anayehusika na Afya, Ummy Mwalimu, katika mwongozo wa kwanza Mei, 27, 2020, alielekeza zaidi ya hatua 10 zinazotakiwa kuchukuliwa za tahadhari dhidi ya corona.

Hapo kuna suala la kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka kila wakati, wanafunzi na walimu kuvaa barakoa, kuepuka misongamano na kutolewa elimu kwa wanafunzi na walimu, jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.

Baadhi ya shule zimeweza kutekeleza maagizo hayo kwa kiwango kikubwa na kuna zingine nyingi zinazoshindwa kufanikisha utekelezaji wa kanuni hizo na hasa zilizoko vijijini.

Nipashe ilitembelea baadhi ya shule katika mkoa wa Simiyu, kutathmini uhalisia uliopo.

Miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa katika ukaguzi huo ni pamoja na unawaji mikono kila mara kwa sabuni na maji tiririka, uvaaji barakoa na ukaaji umbali wa mita moja kati ya mtu na mwingine.

Mengine yanatajwa ni kufuatilia kutekelezwa kanuni zinazoonekana kuwa vikwazo kuvitekeleza kwa shule nyingi.

UVAAJI BARAKOA

Maelekezo ya Wizara ya Afya, inazitaka wizara zinazohusika na elimu kuhakikisha zinatoa maelekezo kwa shule na vyuo, walimu na wanafunzi wanavaa barakoa wakiwa kwenye msongamano, isipokuwa wakati wa mapumziko.

Ni kanuni inayoonekana kushindwa kutekelezeka katika baadhi ya shule na hasa zilizopo vijijini, kwa walimu hata kwa wanafunzi, changamoto imegundulika ni upatikanaji wake, pia uwezo wa kuzinunua.

Katika Shule ya Msingi Mahaha iliyoko Halmashauri ya Mji Bariadi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Charles Yamungu, anasema mbali na upatikanaji wake kuwa mgumu, pia ufuatiliaji kuhakikisha wanafunzi wanavaa barako kila wakati, imekuwa ni ngumu.

“Kama ambavyo tunawajua wanafunzi kuwasimamia kuna kazi ngumu kweli, hasa wale wadogo, ukizingatia ni wengi. Lakini unahitaji muda kuwafuatilia mara kwa mara, kuhakikisha muda wote wawe wamevaa,” anasema Yamungu.

Mwalimu Mkuu huyo anasema, kutokana na mazingira ya shule na wanafunzi kujazana kwenye chumba kimoja kwa sababu ya ukosefu wa madarasa ya kutosha, kunakuwapo msongamano, hali inayotoa umuhimu kwa maagizo ya wataalamu wa afya kuhusu uvaaji barakoa.

“Mfano darasa la tano wapo wanafunzi zaidi ya 200 na wanakaa chumba kimoja. Kwa maagizo ya serikali, lazima wavae barakoa, sasa katika kuhakikisha wote wanavaa, inakuwa ngumu wengine utakuta wamevua, wanabadilishana na kuzichezea,” anaeleza Mwalimu Yamungu.

Hata hivyo, walimu wanasema tatizo linajitokeza zaidi katika kuwafuatilia wanafunzi kuhakikisha wanavaa barakoa, pindi wanapokusanyika hata darasani, kwani wengi huzichezea, kuchangiana au hata kuibiana.

KUNAWA MIKONO

Maagizo ya kiafya kutoka serikalini ni kwamba, shule na chuo kuhakikisha wanafunzi wao wananawa mikono kwa sabuni kwa maji tiririka kabla ya kuingia darasani, kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Ni kanuni inayoonekana kuwa ngumu kuitekeleza katika shule za msingi vijijini, huku za mjini zinajitahidi, kwa sababu ya mazingira bora walio nayo.

Adalbert Chambia, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Gamondo ‘A’ anasema shida kuu kwao ni upatikanaji majisafi, kwa sababu hawana huduma nzuri.

“Huku asilimia kubwa maji ambayo yanapatikana ni yale ambayo yapo kwenye madimbwi, ambayo siyo safi.

“Ukitaka kupata safi, lazima kuchimba kwenye mto ambao uko umbali wa kilomita tano kutoka hapa shuleni,” anaeleza Mwalimu Chambia, huku akitaja idadi ya wanafunzi wote shuleni ni zaidi ya 2000.

“Ukiangalia hapa wanafunzi walivyo wengi utaona tabu ambayo tunaipata. Pia, wanafunzi kuwasimamia ili watumie vizuri maji, nalo ni tatizo maana ni wengi, ingawa sabuni ipo ya kutosha na tumenunua matanki ya kutosha,” anasema.

SHULE MIJINI

Katika Shule ya Msingi Kidinda, iliyoko katikati ya mji Bariadi, wanalalamika shida yao ni upatikanaji maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Mazingira Bariadi (BARUWASA).

Mwalimu Mkuu, Robert Mathias, anasema hawana shida ya maji, bali tatizo lao ni namna ya kuwasimamia wanafunzi kuhakikisha wananawa mikono kila wakati, pindi wanapotaka kuingia darasani.

“Wanafunzi hapa ni wengi sana, kuwasimamia kila wakati wanawe mikono ni kazi ngumu, ingawa tunawaelimisha kila wakati. Wengi wao wanafuata maelekezo, ila baadhi wale wadogo wanajisahau,” anaeleza.

MSONGAMANO

Suala la wanafunzi kukaa mita moja kati ya mmoja na mwingine utekelezaji wake unadaiwa kuwa mgumu kwa shule zote za msingi, mjini na vijijini.

Hapo Nipashe imebaini shida kuu ni idadi kubwa ya wanafunzi kuzidi uwezo wa vyumba vya madarasa na madawati yake.

Katika Shule ya Msingi Gamondo ‘A’ yenye wanafunzi 2,505 inahitaji madawati 835 na vyumba vya madarasa 56, ili kukidhi kanuni hiyo ya kukaa umbali wa mita moja kati mwanafunzi na mwingine.

Mwalimu Mkuu Chambia, anasema shule ina vyumba vya madarasa 17 ikiwa na madawati 719, hivyo wanafunzi wanakaa kwa kubanana na kwenye dawati moja wamejaribu kupunguza idadi ya wanafunzi wanakaa watatu.

Anaendelea: “Zamani wanafunzi walikuwa wakikaa wanne hadi watano kwenye dawati moja ambalo uwezo wake ni wanafunzi wawili, kwa sasa baada ya hali hii, tumejaribu kupunguza wanakaa watatu, lakini bado.”

ELIMU YA CORONA

Utolewaji elimu kila mara kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huo na madhara yake kwa wanafunzi, Nipashe imegundua kwa kiwango kikubwa inatelezwa, walimu wamekuwa wakitumia wastani wa dakika 10 kabla ya kufundisha, kuelimisha jambo hilo.

“Kabla ya shule kufunguliwa walimu tulipewa elimu ya ugonjwa huu na jinsi gani tutaweza kuwafundisha wanafunzi na tumekuwa tukiwaelimisha mara kwa mara kabla ya kuanza kupindi,” anaeleza Mwalimu Mukama Mukama.

Habari Kubwa