Utoaji huduma hospitali za umma umulikwe

06Jun 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Utoaji huduma hospitali za umma umulikwe

WIKI iliyopita Rais Samia Suluhu Hassan, alifanya ziara ya kushtukiza maeneo manne ikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Dar es Salaam ili kujionea utoaji wa huduma.

Salome Kitomari.

Ziara hiyo ilituma salamu kwa watendaji wa umma kuwa wanapaswa kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa serikali iko macho na inafuatilia kwa karibu.

Napongeza kwa hatua hiyo ambayo huenda itasaidia kuwashtua watendaji kuwa serikali iko macho na wakati wowote Mkuu wa nchi anaweza kufika kwenye eneo lao na kujua yanayoendelea, maana yake kinachotakiwa ni uwajibikaji.

Pamoja na jitihada hizo ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa kiserikali wa ngazi nyingi, lakini bado ipo haja ya kumulika sana hospitali za umma.

Leo nitazungunzia Mwananyamala ambayo nimewahi kipeleka mgonjwa, kilichonikuta na majibu niliyopata baada ya kudodosa kwanini hali iko hivyo, na hii ni mfano halisi ikiwa ni moja kati ya wengi wanaotendewa hivi.

Nilipeleka mgonjwa ambaye alijifungua siku chache zilizopita hospitalini humo na kupata shida ya nyonga, nilivyofika nilichukua kiti cha wagonjwa na kutakiwa kumuinua mgonjwa wangu na kumkalisha.

Nilifanya hivyo kwa shida sana kwa kuwa ni mtu mzima hivyo ni ngumu kumuinua mwenyewe, nilimuomba mpita njia anisaidie katika hilo. Nilivyofika mapokezi kwanza nilikutana na majibu ilimradi na hiyo ni kutokana na ugeni wangu katika kujua wapi pa kuanzia, niliandikiwa kwenda kumuona daktari.

Nilivyofika chumba cha daktari hakuwapo nililazimika kusubiri kwa muda na alivyokuja nilijua natakiwa kuingia, lakini nilifukuzwa kwa lugha kali ya “subiri huko nje hadi nikuite” ilichukua tena muda flani hadi kuingia ndani.

Nilipoingia kwa kuwa mgonjwa wangu hakuwa anajiweza nilitakiwa kumpandisha kitandani na nilivyoona siwezi niliomba msaada wa daktari ambaye alijibu ovyo kuwa “Kama hutaki atibiwe utajua mwenyewe ila hakikisha anapanda hapo kitandani.” Na haikutosha alimtaka asimame wakati mgonjwa alikuwa hawezi hata kujisogeza mguu na aliposema hawezi kunyanyuka alimfuata na kumminya nyonga kwa nguvu (mtu mwenye hasira kali).

Tulipambana mimi na mgonjwa wangu ili kumpandisha kwenye kitanda kwa ajili ya uangalizi, baada ya hapo tulitakiwa kwenda kupiga X-Ray, ambayo katika chumba tuliwakuta vijana wenye morali na walinisaidia kumnyanyua mgonjwa na kumpandisha kitandani.

Baada ya X-Ray nilitakiwa kurudi kwa daktari na nilipofika mlangoni tu nakutana naye anatoka na kututaka turudi siku ya Jumatatu, wakati huo mgonjwa anaumwa sana hata hawezi kufanya lolote, na baada ya kulalamika tulipewa panadol za kutuliza maumivu.

Nilijiuliza sana kwamba ni wagonjwa wangapi wanakwenda hapo na kupata huduma za aina hiyo, kwamba kuanzia mapokezi kwenye kulipia lugha ni mbaya, ukifika kwa daktari naye hali hiyo hiyo na mwisho unaondoka na maumivu au ugonjwa wako.

Nikiwa hapo nilivutiwa kuuliza kwanini hali iko hivyo kwa kuwa binafsi nimezoea kutibiwa hospitali binafsi ambazo mgonjwa ni mteja hivyo wanamjali kwa kuhakikisha anapata huduma zote muhimu tena kwa ubora. Nilizungumza na kijana aliyekuwa maabara na dada mwingine aliyekuwa mapokezi, swali langu kwao ilikuwa mbona kila mfanyakazi anaonekana ana kisirani katika kuhudumia, kwani kuna shida gani.

Ndipo walipofunguka kwa nyakati tofauti kuwa dada usituone hivi kali zetu ni ngumu hakuna motisha, hakuna malipo ya muda wa ziada, tuna malimbikizo mengi, maisha yetu ni magumu, mfano daktari aliyekuhudumia huenda hata hajui nyumbani kwake watakula nini, hivyo wewe tusamehe tu ridhika na hata hii huduma uliyopata maana nasi tuna matatizo yetu mengi kubwa mishahara ni midogo sana.

Nilishtuka kwa kuwa huyo ni mmoja na daktari alinionyesha kwa vitendo hakuwa tayari kuzungumza, nilichokifanya sikurudi tena hospitalini humo badala yake nilimtafuta daktari hospitali binafsi ambaye aliniandikia dawa za kununua na mgonjwa wangu alipona kabisa.

Kwa kawaida mtu anapokuwa mgonjwa anapofika hospitalini akimuona daktari anapata tumaini la kupona kabla hajahudumiwa, hiyo inategemea na jinsi alivyompokea na kumpa huduma, inapokuwa tofauti ni kumuongezea mgonjwa matatizo.

Juzi, katika moja ya kundi letu la taaluma mmoja wa mwanataaluma ameeleza yaliyomkuta baada ya kwenda hospitalini humo akisumbuliwa na mifupa, na aliishia kufukuzwa na daktari hadi alipowasiliana na watu Wizara ya Afya ndipo akapata huduma.

Anaeleza kuwa daktari anayemhudumia siku zote ndiye huyo, lakini alimbadilikia akamjibu vibaya na kumtoa ndani ya chumba. Hii ni mifano michache kati ya mingi, wangapi wanakosa huduma au kupewa huduma ovyo kwa mazingira kama haya, mbona haya hayafanyiki kwenye hospitali binafsi, na je, nini kinafanyika kuweka morali na kuboresha utendaji kazi kwa hospitali inayohudumia mamia ya watu?

Ipo haja kwa serikali kufuatilia kwa karibu sana kero na huduma hafifu zinazotolewa, ipo haja ya kuzungumza na wafanyakazi na kuwapa morali, maana kama hospitali ya mjini hali iko hivi, vipi hospitali, vituo vya afya na zahabati huko vijijini?

Hii inatuma salamu kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuiiangalia sekta ya afya, kuangalia namna ya kuwafanya wafanyakazi wajifunze yanayofanyika sekta binafsi ili siku moja huduma kwenye hospitali za umma iwe bora zaidi ya sekta binafsi.

Mungu ibariki Tanzania

Habari Kubwa