Utumaji fedha kwa Simu na changamoto zake

17Jun 2016
Denis Maringo
Dar es Salaam
Nipashe
Utumaji fedha kwa Simu na changamoto zake

A. UTANGULIZI

MATUMIZI ya simu katika kutuma, kupokea, kuhifadhi fedha na pia kufanya manunuzi ama ulipaji wa bili mbalimbali ni jambo jipya ambalo kila kukicha linashika kasi hapa nchini.

Itakumbukwa kwanza, matumizi ya aina hii yalijaribiwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya kisha kushika kasi Afrika Mashariki yote.Kwa sasa yanasambaa kwingi kwingineko na yamewakuna wengi, akiwemo Rais Baraka Obama wa Marekani ambapo wakati alipofanya ziara yake nchini humo mwaka huu aliwasifu Wakenya waliobuni utaratibu huu kuwa wamemfanya mwafrika aheshimike zaidi na pia kubainisha kuwa hii ni moja ya fursa kubwa za kibiashara na ukuaji wa uchumi kwa watu wa Afrika Mashariki.

Kabla ya matumizi ya huduma hizi za miamala ya fedha kwa njia ya simu, dunia ilijikuta imezoea utaratibu wa tumuli na upokeaji wa fedha kwa kutumia huduma zenye chimbuko la nchi za Magharibi kama Western Union na Money Gram. Huduma hizi bado zipo na hasa pale mtumiaji na mpokeaji wanapoishi nchi ama mabara tofauti ambapo inabidi kwenda katika moja ya matawi ya makampuni haya ili wapatiwe huduma.

Tukumbuke kuwa Benki na Taasisi za fedha nazo bado zina huduma kama hizi, ingawa ambapo fedha zinaweza kuwekwa , kutumwa na kuchukuliwa baina ya akaunti mbalimbali, ndani ya nchi fulani na hata nchi na mabara tofauti. Zaidi ya hapo, matumizi ya kadi za plastiki za kuhifadhia na kuchukulia fedha (Credit Cards na Debit Cards), maarufu nchini kama kadi za ATM (mfano Visa, MasterCard na American Express) ni kielelezo kingine dhahiri kuwa ushirikiano wa wataalam na makampuni ya fedha na yale ya teknolojia umeleta mapinduzi makubwa katika sekta za fedha, biashara na uchumi

Kwa kifupi maisha yamerahisishwa sana na kitu pekee ni wewe na mimi kuzitumia fursa hizi kikamilifu. Baada ya utangulizi huu, tuangalie sasa changamoto za kisheria zilizopo kwa makampuni ya simu, mawakala wa upokeaji na utoaji fedha (kama M-Pesa, Tigo Fedha, Airtel Money na EzyNet), wateja Watumiao huduma hizi, mamlaka za udhibiti, pamoja na wadau wengineo.

B. CHANGAMOTO ZA KISHERIA
Biashara ya utumwaji wa fedha kwa njia ya simu na miamala yake ni jambo lenye changamoto zake. La kwanza lililo wazi ni kwamba sekta hii mpya inayokua kwa kasi haijawa na sheria (wala sera) maalum inayojitegemea kuidhibiti ama kuwafahamisha wadau na jamii kwa ujumla kuhusiana na mambo kadhaa ya msingi ambayo mtu wa kawaida anapaswa kuyajua pasipo kumtafuta mwanasheria au kuuliza TCRA, Benki Kuu ama Wizara ya Fedha ama ile ya Mawasiliano.

Mathalani, maswali ya harakaharaka ambayo mtu yeyote anaweza kujiuliza ni: (1) Kwa sababu utumwaji wa fedha kwa njia ya simu unahusisha teknolojia ya simu katika kufanya kazi ambazo kwa asili zimekuwa zikifanywa na benki, je ni nani hasa mwenye jukumu la kuidhibiti na kuitolea miongozo sekta hii?, Je ni Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA) ama Benki Kuu ya Tanzania (BoT); (2), Je, Ni Sheria ipi inayotawala zaidi hapa, ama pale zinapogongana sheria za kifedha na zile za mawasiliano ya mtandao, ni ipi inachukua nguvu?; (3), Je ni wakati gani Jeshi la Polisi ama Idara ya Usalama wa Taifa ‘vintages’ kujihusisha ama kuhusishwa pale wizi au uhalifu mwingine unafaponyika katika miamala ya kifedha kwa njia ya simu ama pengine kuhamishwa kwa kiasi kikubwa cha fedha na genge fulani ambalo linahatarisha usalama wa Taifa?; (4) Nafasi, haki, wajibu na mahusiano ya Kisheria baina ya Makampuni ya Simu, Mawakala wa Utoaji na Upokeaji Fedha na raia wanaotumia huduma hii, ikoje?; (5) Je, kodi zinazolipwa Serikalini katika huduma hizi ni stahiki?; (6) Je, Sheria za mahusiano ya Kazi na Ajira zinamtambua Wakala kama Mfanyakazi wa Kampuni ya Simu ama ni wakala tu, na je, malipo ya Kamisheni kwa mawakala wa Simu ni ya kiwango kinachokubalika kisheria ama kuna unyonyaji fulani? Haya, ni baadhi tu ya maswali yanayotoa taswira ya haraka kuhusiana na changamoto nyingi zilizomo katika jambo hili.

Katika haya, tukumbuke kuwa siku chache zilizopita kampuni moja kuwa ya simu huko Afrika Magharibi imeamriwa kulipa fidia ya mabilioni ya fedha kwa jambo ambalo linagusa moja kwa moja hiki tunachokiongelea leo. Ililipishwa faini hiyo baada ya kuthibitika kuwa namba ya simu iliyounganishwa na mtandao wa kampuni hiyo na ambayo haikuwa imesajiliwa rasmi ndiyo iliyotumiwa na genge la wahalifu lililokuwa limemteka aliyekuwa Waziri wa Fedha wa Nigeria ili kwamba watumiwe fedha katika namba hiyo ili wamuachilie huru.

Tukiachana na changamoto hizi, kwa mwanasheria kitu kimoja ni wazi nacho ni kwamba tumuli na upokeaji fedha kwa njia ya simu si jambo linaloweza kumuumiza mwanasheria mzuri kwa sababu huu ni kama mvinyo wa zamani ndani ya chupa mpya. Maana yake ni nini?

Maana yake ni kuwa mahusiano ya kisheria baina ya Makampuni ya simu, mawakala wao na mwananchi ama kupokea fedha ni yale yale ambayo yako katika sheria zetu, na hasa sheria ya Mikataba ya Tanzania (Sura ya 345), ambamo ndani yake imeweka bayana ni nini haki na wajibu wa kila mmoja: Kampuni ya simu itoayo huduma za kifedha, wakala unapoenda kuweka ama kuchukua fedha, na mwananchi mteja anayetumia huduma hizi.

Ndiyo kusema basi, pale unapotumia fedha halafu isikufikie basi kuna mtu ana wajibu na haki. Iwapo pia ukatuma fedha halafu ukakosea namba ya yule unayemtumia ama ya wakala na ikaenda kwa mtu asiyehusika kabisa, basi pia sheria zetu zinajitosheleza kwa kulifafanua hili. Vipi labda, ambapo ubovu wa mtandao umekusababisha upate hasara kubwa kwa kushindwa kutoa fedha wakati uliihitaji kufanikisha jambo fulani zito?

Kwa leo tuishe hapa. Alamsiki.

*Denis Maringo ni Mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. Mawasiliano: 0719.270.067; Barua-pepe: [email protected]

Habari Kubwa