Uvivu na kilio cha ajira kulivyouingiza mji Mpanda kashesheni vikundi

25Nov 2022
Neema Hussein
MPANDA
Nipashe
Uvivu na kilio cha ajira kulivyouingiza mji Mpanda kashesheni vikundi
  • Majina yao; Damu Chafu, Manyigu, Kaburi Moja, Kunguru Mweusi, Mchelemchele, Mazombi, Wafu,Mkoa waigeuza ajenda, RPC awawashia moto

JANA, ilikuwa sehemu ya kwanza ya makala hii, ikiwa na simulizi namna uongozi na wakazi walivyoshirikiana kufyeka vichaka, makazi ya wakabaji, ambao waligeuka tishio kubwa. Endelea na simulizi ya kilichojiri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, SACP, Ali Makame; ndiye kavisambaratisha vikundi. PICHA ZOTE: NEEMA HUSSEIN.

 

 

MJI wa Mpanda ulioko mkoani Katavi, mara zote

wakazi wake wengi wanajishughulisha na uchumi wa biashara na kilimo, kukiwapo mzunguko wa pesa, huku sehemu kubwa ya waajiriwa ni wa serikalini na taasisi zisizokuwa za kiserikali.

 

Ndani ya mazingira hayo, ndipo napo kuna hofu ya kuwapo makundi ya kihalifu yaliyoibuka hata kuwarudisha nyuma wananchi wanaopambana kujipatia kipato halali, maana wanawapora vitu mbalimbali kama vile pesa, simu na wengine wanavunja nyumba zao kuwaibia.

 

Makundi hayo yamejipa majina maaarufu kama Damu Chafu, Manyigu, Kaburi Moja, Kunguru Mweusi, Mchelemchele, Mazombi na Wafu na staili yao imekuwa kuvizia maeneo ya mikusanyiko ya watu, kama vile kumbi za starehe, harusini, misibani na barabarani pale wanapokutana na mtu pekee, hasa nyakati za usiku.

 

Ni hali inayowafanya wakazi wa Mpanda kufanya shughuli bila ya kuwa na amani wakilazimika kuwahi nyumbani kutoka kwenye biashara zao, wakihofu kukabwa na kuporwa.

 

Ni uporaji wa kutumia silaha za jadi kama vile mapanga, visu, nondo, bisibisi na vingine vyenye ncha kali, hata ajenda hiyo ikaifikia ngazi ya kujadiliwa katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Mkoa wa Katavi.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, SACP, Ali Makame anasema sehemu kubwa ya vijana hao ni kuanzia umri wa miaka 14 hadi 32 na tayari wameshachukua hatua kubwa kuwasaka na kuwakamata, baadhi wameshafikishwa mahakamani na operesheni inaendelea kuwakabili.

 

Jeshi hilo lilifanya msako katika mitaa mbalimbali na hivi karibuni limetoa taarifa ya kukamatwa kwa vijana wengine 11 kutoka katika mitaa ya Nsemulwa, Majengo na Kazima katika wilaya ya Mpanda

 

"Sasa hivi mbona raha mtu unatembea mpaka saa 5 saa sita usiku, wala hupati tatizo lolote kwa kweli tulipongeze jeshi la Polisi limejitahidi sana kuwakusanya hawa vijana mtaani sa hizi mtaa umetulia," anasema Juma Shabani, mkazi wa Manipsaa Mpanda.

 

Mkazi Jackson Phillipo, anaielezea Nipashe kwa kauli: “Ni vijana wadogo wadogo! Chanzo cha makundi haya kwangu mimi naona ni ushawishi unaotokea kwenye makundi rika, wengi wanaingia huko pasipokuwa na elimu yoyote ya kujua wanafanya vile kwa faida ipi au hasara ipi katika jamii.

 

"Vijana wanapomaliza shule hawajui wafanye nini, hata wazazi wao pia hawawafuatilii kabisa. Njia rahisi ya kujipatia kipato wanaona bora waingie huko, kumbe ndio wanaenda kupotea kabisa.

 

"Kitu kingine mimi nadhani vijana wengi wanataka mafanikio ya haraka yaani anahisi akifanya hivo atapata labda mali, pesa nyingi kumbe hapana. Mimi nashauri tu labda wazazi wangewasomesha watoto na elimu ya dini ili wapate hofu ya Mungu."

 

Hiyo inaendana na maoni ya Juma Shabani, kwamba:"Mimi naona tatizo kubwa ni wazazi kutokuwajibika. Tuangalie kabla ya kuwawajibisha hawa vijana, lazima tuangalie kwanza je wazazi wanatimiza wajibu wao, Kabla Jeshi la Polisi au serikali halijawahukumu?.

 

Ivo Chambala, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makanyagio, eneo mojawapo maarufu kwa uhalifu, anaisimulia Nipashe kuwa ongezeko la makundi ya kihalifu linachangiwa na serikali kunyimwa ushirikiano kutoka kwa wazazi wasiojua shughuli za watoto wao, hata wanakolala.

"Kama wiki mbili zilizopita kuna kundi la mitaa jirani kutoka kata ya Misunkumilo, Shanwe na Kigamboni walivuka huku majira ya saa mbili (usiku) kuja kuvamia na kuleta fujo ya kutaka kupora watu, lakini kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, tulilisambaratisha hilo kundi na kutoa taarifa kwa Polisi Kata wetu.

"Tulikuja kungundua ni sehemu ya vijana wengi ambao wapo majengo na kituo chao kinakuwa ni Shule ya Sekondari Mwangaza, ndio ilikuwa kituo wanachokutana mara kwa mara. Ukiwaona ni kama wameenda kwa mazoezi ya mpira kumbe wanakuwa ukingoni mwa makaburi na kupanga mipango yao ya kihalifu.

"Sasa katika vikao vyetu tulikua tunajua kabisa hilo eneo la makaburi ya Mwangaza ni eneo hatarishi hasa tukiliacha likiwa chafu sababu vitendo vyote vya kihalifu lilikuwa hilohilo chaka linawahifadhi wavuta bangi, hata mali za wizi zilikuwa zikifichwa katika hayo makaburi, anasema Chambala.”

BANGO LA RC

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amekuwa akikemea vikundi hivyo tena kwa majina, akiwasisitiza vijana kubadilika, kwa kutafuta kipato cha halali.

 

Ni mara kadhaa Nipashe imemshuhudia akitenga muda wake kukutana na vijana na kuzungumza nao, ikiwemo kusikiliza kero zao, hata kuwasaidia pale inapobidi.

 

Hivi karibuni alipozuru katika shughuli za vijana wabeba mizigo waliounda umoja wao kumiliki miradi kadhaa unaoitwa Trans Cargo, amewasisitiza vijana kuondokana na utegemezi na kuondoa umasikini uliokithiri.

 

"Mara nyingi mwili wa binadamu haukubali yaani ana afya njema, amekula ameshiba, halafu amekaa hana kitu cha kufanya, ukiona mtu yuko hivo huyo mtu ni hatari sana! Kwa sababu ni lazima kwa mujibu wa asili yetu ‘nature’ ya miili yetu, atatafuta jambo la kufanya kwa ajili ya kutumia ile nguvu yake,” anasema Mkuu wa Mkoa.

 

Mzee Charles Anthony, mwenyeji mkongwe wa mjini Mpanda, anaunga mkono kauli ya Mkuu wa Mkoa Mwanamvua, akisema: "Changamoto za vijana sasa hivi ni nyingi sana wengi wanawaza kuajiriwa tu, sasa ile inawapa shida. Zamani ilikuwa ukitoka darasa la saba la nane unapata kazi, usipopata kazi unashika jembe unalima au shughuli zingine.

 

"Sasa hivi hilo halipo! Kwanza ‘kinacho- wakosti’ (kinachowagharimu) ni mitaji, mitaji hawana. Pia, huwa nawaza wakikamatwa kwanini wanaachiwa? Watu mmeshajua ni wahalifu, mnawaachia tena wakirudi wanafanya uhalifu!”

 

Mkazi Evarist Katoto, anafafanua kupitia simulizi akisema: "Kulikuwa kuna watu hapa Mpanda Hoteli (mtaa wa kiserikali) sio watu, hao ni balaa! Si bora sasa hivi, ilikuwa hutembei kwa raha. Unaweza ukatembea, ukashangaa tu ngwala, kofi, umenyang’anywa simu, umesachiwa, umechukuliwa hela, unabaki unapiga kelele na hamna wa kukusaidia."

 

ULINGO WA MIKASA

Juvenary Deus, ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Msasani, Mpanda anaisimulia  Nipashe, kuna wakati wizi umefanyika mchana, ila sasa usalama umetawala kutokana na vikundi vingi vya kihalifu kukamatwa na mtaa wake umetulia.

Anasema, watu waliokuwa wakikabwa katika eneo hilo, zaidi ni abiria kutokana na mtaa huo kuwa karibu na stesheni, pia hata wapita njia hasa wafanyabiashara waliokuwa wakitoka kwenye biashara zao.

"Pia, hata siku za kawaida ambazo treni haipo basi wanakaa wanamvizia mtu yeyote watakayemuona labda amebeba kibegi chochote wanamuona mwonekano wake mzuri, basi wanamfuatilia nyuma mpaka sehemu fulani, halafu wanajifanya kuwa wao ni askari wapelelezi.

"Yaani mbinu wanayotumia hadi mtu, aamini wanaenda kwa wale migambo migambo wanakubali kuchukua fedha kutoka kwao wanavua zile nguo wanawapa halafu wanapiga nazo picha za paspoti wanaenda kutengeneza vitambulisho vya kuonyesha kuwa wao ni askari au mgambo.

"Sasa wakimkamata mtu wanamuonyesha hicho kitambulisho na yeye anakubali anawafuata akifika huko anawakuta na wengine kwenye kichaka ndio wanamkaba sasa hizo ndio zilikuwa mbinu zao.

"Mimi mpaka nililala ndani, ikaonekana labda nashirikiana nao maana ilionekana, baadhi ya vitu vinaingia huu mtaa vya wizi na wanafanya biashara humu humu, mazoezi ya ukabaji yanafanyika kwenye mtaa huu, lakini baada ya kufuatilia kiundani zaidi wahusika walibainika na walikamatwa na mpaka hivi sasa wako ndani,” anasema.

Anasema, kwenye kikundi cha Damu Chafu, watu wazima wakawa wanawapa watoto silaha kama nondo kwenye majira ya saa mbili na saa tatu, akiweka mfano hai, penye shule ya Sekondari Kashaulili, walikogundua watu wazima usiku wakishiriki njama na watoto wanaowaweka katika sehemu za maficho kushiriki uhalifu.

"Wakipita watu wale watoto wanaanzisha fujo, wale watu wazima wanafanya kama wanajipitisha ili waamue ule ugomvi, kumbe wao ndio wamewaagiza wale watoto, hapo wanaingilia na kumkaba mtu, wanamuumiza na kumpora.

Anasema, Polisi imechangia sana kufanikisha kukabili uhalifu huo na watuhumiwa wamekamatwa, hali iliyorejesha usalama wa mji kwa ujumla.

Taasisi mbalimbali nazo zikaingilia kati kusaidiana, ikiwamo Jeshi la Magereza kushiriki kufyeka mapori na vichaka kama vya makaburi ya Mwangaza na mapori ya Stesheni, ambako kulitumiwa  kama vituo vya kupanga na kufanya uhalifu, pia kuhifadhi silaha na mali zilizoibwa.