Uzuri wa nyumba si lazima kutumia bilioni

12Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Uzuri wa nyumba si lazima kutumia bilioni

WATU wengi wanapenda nyumba zao ziwe na mvuto wa kuridhisha na kusuuza nafsi ili kuwaongezea furaha moyoni hasa ile ya kuwafanya wajisikie kuwa wako nyumbani.

Maua haya yanayotengenezwa kwa usatadi na sanaa hubadilisha uzuri wa nyumba na kuifanya mpya hata kama imechakaa. PICHA: VIVIAN MACHANGE.

Pamoja na kupenda huko lakini wanashindwa kuziridhisha nafsi hasa kutokana na sababu kubwa ya kipato kiduchu . Kiasi kidogo cha fedha walizonazo au uchumi kutokuruhusu kufikia kiwango hicho ni tatizo linalowafuatilia wengi.

Mtaalam wa masuala ya ujenzi Lucas Kwambikwa, anayeishi Mbezi Dar es Salaam, siyo suala kubwa la kuwaogopesha watu siku hizi.

Anaeleza kuwa zipo njia mbalimbali za kufikia angalau kwa kiwango fulani uzuri wa kile ambacho kinaweza kuridhisha nafsi ya mmiliki.

Mtu anaweza kuwa na nyumba nzuri ambayo ameiboresha kwa gharama ndogo na kuisha kwenye nyumba bora tena ikaonekana mujarabu kama zilivyo nyumba nyingine nzuri na za kisasa zilizozagaa mitaani.

Jambo la kwanza mtaalamu anashauri kwamba endapo unakuwa na nyumba iliyochakaa na hufurahishwi na muonekano wake, anza kwa kukwangua rangi yake na kupaka mpya.

Unaweza kutumia ile ile au ukabadilisha na kutumia nyingine.

Pamoja na hayo anashauri kupaka rangi ambazo utaridhika nazo mwenyewe na si kulazimishwa na mtu mwingine, ukiamini kuwa zitaipa nyumba muonekano mpya wa kiwango cha juu.

Anasema kwamba kupaka rangi kwenye chumba au nyumba kutasaidia kuipa hadhi, uzuri na sura mpya lakini pia inaipandisha chati na kuifanya kuwa bora zaidi.

Anasema juhudi hizo zimelenga kuboresha nyumba na kuipa muonekano mpya lakini kwa kutumia gharimu kidogo na kazi ndogo.

Jambo jingine muhimu ni kubadilisha fenicha au samani au kuongezea mapambo madogo.

"Hebu fikiria wakati unaponunua vitu vya kuuvika mwili kama nguo, viatu na pochi ambavyo mwanamke, anahitaji kuwekeza hela nyingi kwa maana ya kuwa bidhaa zenye viwango, visivyoharibika ndani ya muda mfupi. Vivyo hivyo kwa ajili ya nyumbani kwako unapoishi. Wekeza kwenye vitu vile vya thamani ambavyo vina haki ya kutumia hela yako ya nyongeza," anasema Kwambikwa.

Jambo jingine ambalo anasema linaweza kusaidia katika kuuweka upya uzuri wa nyumba yako na kuipendezesha ni kununua mahitaji ya kuweka ndani ambayo ni machache na ya muhimu.

Anasema ni muhimu kuwa na falsafa hiyo kichwani wakati unapohitaji kununua vitu kwa ajili ya nyumbani kwako.

Aidha, kiwe ni kwa matumizi au kwa kupendezesha au vyote kwa kuhakikisha kuwa kila kitu unachoweka ndani ya nyumba yako umekichagua kwa umakini na kinapaswa kuwapo.

"Tunapoondoa vile vitu ambavyo havihitajiki, tunavipa vile ambavyo ni muhimu nafasi ya kung’ara"

"Kwa mfano huna haja ya kubandika 'wallpaper' zenye maua na michoro lukuki badala yake pamba ukuta (kwa mfano ule wa nyuma ya sofa) kwa kutundika picha moja kubwa. Au pia badala ya taa nyingi nyingi weka urembo mkubwa mmoja wa kuning’inia katikati ya chumba.

Jambo jingine Kwambikwa anasema ili kutunza nyumba yako iendelee kuonekana mpya kwani kuna umuhimu wa kuondoa baadhi ya vitu ambavyo aidha vimechakaa sana au ambavyo vimenunuliwa na kuingizwa ndani ya nyumba bila kuwa na matumizi ya muhimu na vikaonekana kuchangia kuharibu mvuto wake.

"Kabla hujanunua kitu cha nyumbani iwe ni kitanda, kochi, pazia na jokofu hakikisha kuwa umepata kilicho bora na kwa bei inayokubalika, kwa mfano, gharama ya kitanda cha chuma cha ukubwa wa futi tano kwa sita ni tofauti kwa kila mtengenezaji japo bidhaa ni ile ile.

Au pia gharama inaweza kupungua kutokana na muundo wa kitu japo ukubwa unakuwa ni ule ule unaohitaji," anasema.

"Na pengine badiliko la muundo haliathiri matumizi ya bidhaa hiyo. Tukirudi kwenye Mfano huo huo wa kitanda cha chuma yawezekana muundo fulani unahitaji vyuma vingi wakati mwingine unatumia vichache, kwa hivyo moja kwa moja unakuta bei yake inakuwa chini na ukiangalia dhumuni lako la kupata kitanda cha kulalia linakuwa limetimia bila kujali muundo.Unapopendezesha nyumba yako ni vyema ukaangalia kila upande wa namna ya kupata kitu chenye ubora lakini kwa bei nafuu."

Kwambikwa anasema ili nyumba yoyote ionekane imekamilika na ni ya gharama au ya kifahari hata kama si lazima uwe umekamilisha kukarabati kila eneo unaweza kufanya yafuatayo.

Weka mapazia , mazuri katika sehemu muhimu zinazohitajika kama sebuleni, chumba cha kulia na jikoni.
Unaweza kwa kuwekeza kidogo kidogo na kwa namna hilo, nyumba nzima itafanyiwa mabadiliko na lazima ionekana imekamilika na nzuri.

Habari Kubwa