Vannesa awataka wasichana wajitambue wasiruhusu vishawishi visikatishe

08Nov 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Vannesa awataka wasichana wajitambue wasiruhusu vishawishi visikatishe

“MTOTO wa kike unapaswa kujitambua, kujikubali, kusoma kwa bidii, kutumia vizuri elimu uliyoipata, kuweka malengo huku ukijua unachokitaka kwenye maisha na daima hutayumba,”

Huo ni msimamo wa msanii Vanessa Mdee, aliutoa wakati akizungumza na wanafunzi wa shule za sekondari katika Ubalozi wa Marekani Tanzania hivi karibuni.

Vannesa alikutana na wanafunzi hao wa shule mbalimbali wakati yalifanyika majadiliano ya moja kwa moja kupitia mtandao wa ‘Skype’ na mke wa rais wa Marekani, Michelle Obama, mwigizaji na mwanaharakati, Yara Shahidi, toka Marekani.Yalifanyika ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, Oktoba 11, katika Ubalozi wa Marekani Tanzania.
 
Wanafunzi zaidi ya 50 wa shule mbalimbali Tanzania walizungumza na kumuuliza maswali Michelle Obama, kuhusu changamoto zinazowakabili watoto wa kike duniani na kuwatia moyo kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
 
Vannesa anasema mtoto wa kike wa Tanzania anahitaji elimu ya darasani na jamii ili kujitambua na kuweza kuchanganua mambo mbalimbali anayokutana nayo katika ukuaji wake na asiruhusu mtu yeyote kukatisha ndoto yake.
 
“Sikuwahi kufikiri kuwa Tanzania bado tuna ndoa au mimba za utotoni nikiamini kuwa kila mmoja ana elimu, lakini kwa kukutana na wanafunzi hawa na kusikia changamoto za wengine nimeona ni tatizo la kidunia ila linatofautiana kimuundo,” anasema.
 
Vannesa anasema anajivunia kuwa mtoto wa kike aliyejitambua mapema na kukabiliana na changamoto zote hadi kufikia kuwa mwanamuziki wa viwango vya kimataifa, huku akiendelea kuimba nyimbo mbalimbali kwa ajili ya kuwafanya wanawake na watoto wa kike wajitambue.
 
Mwanamuziki huyo ambaye anatamba na kibao cha ‘Strong girl’ kilichoshirikisha wasanii wa Afrika, Marekani na Ulaya, anasema ni lazima mtoto wa kike popote anapokuwa kuonyesha kwa kiasi gani yupo imara, mwenye kujitambua na kuweza kukabiliana na changamoto zinazomzunguka.
 
“Wasichana wa Tanzania wanastahili kupata kila fursa ili waweze kufikia upeo wa uwezo wao,” alisema Mdee na kuendelea. “ Nina hamasa kubwa  ya kusaidia elimu yao na ninashukuru kuwa sehemu ya tukio hili la kuonyesha nini Tanzania na nchi nyingine zinaweza kufanya katika kuwaandaa wasichana ili kufanikiwa shuleni na hata baada ya kuwa wamemaliza masomo yao,”alisema.
 
Anasema ni lazima wazazi wakasimama kwenye nafasi zao za kuhakikisha kuwa hawawi kikwazo cha watoto wao kupata elimu kwa tamaa ya kupata mali za haraka kama kumuozesha mtoto wa kike aliyepaswa kuwa shuleni na kutambua kuwa, ukimwelimisha mtoto wa kike umeelimisha jamii.
 
“Kuna changamoto nyingine za kudharaulika kwa mtoto wa kike au mwanamke kuwa ni dhaifu hawezi kushika nafasi za juu kiserikali au kuongoza kwenye ofisi yoyote,” anasema.
 
Vannesa anasema mazungumzo ya mke wa Rais Obama na wanafunzi hao yamekuja kwa wakati muafaka kukiwa na tatizo la ndoa za utotoni huku takwimu zikionyesha kuwa mkoa wa Shinyanga unaongoza
 
Nasra Abdallah ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Kondo- Tegeta, anasema rafiki zake wawili walijikuta wanashindwa kuendelea na masomo baada ya kubakwa wakati wakienda na kurudi shuleni. Anawatuhumu waliofanya vitendo hivyo kuwa ni vijana wa mtaani waliosababisha akapata mimba.
 
“Nimejisikia furaha sana kuongea na Michelle Obama na kumuuliza maswali ikiwamo kusikia historia yake ambayo kwa kiasi fulani, kumbe naye kapitia changamoto mbalimbali licha ya kuzaliwa na kukulia kwenye Taifa la Marekani,” anasema.
 
Katika mazungumzo yake na Michelle, Nasra alimweleza jinsi watoto wa kike hasa wa shule za kutwa wanapojikuta kwenye vishawishi vinavyochangia kukatizwa masomo yao kutokana na tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam.
 
Anasema hawakubaki kulalamika walichukua hatua kwa kushirikiana na wanafunzi wenzake wakaanzisha klabu ya kuelimisha jamii inayozunguka shule, hususan vijana kwa kumpa mimba mwanafunzi anakuwa ameharibu mtiririko wa maendeleo yake.
 
“Kampeni yetu imekuwa ya nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, lengo letu ni kuwafikia vijana wengi zaidi ambao wako mtaani na kuwavizia wanafunzi wanapokwenda au kutoka shuleni, wanakuwa kikwazo cha kuweza kufikia malengo ya kitaaluma,” anasema.
 
Veronica Frank ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Kondo-Tegeta, akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo anasema kuwa baada ya kusikia changamoto za wanafunzi wa nchi za Uingereza, Peru, Jordan na majimbo ya Paris na Washington Marekani, anasema amebaini mambo mengi ambayo yanayakiwa kuangaliwa kwa makini na kujifunza.
 
Alibainisha kuwa changamoto kwa mtoto wa kike hazipo Tanzania pekee bali duniani kwa ujumla, ila zinatofautiana muundo na namna ya kuzikabili, hivyo ni wajibu wanafunzi na watoto wa kike kwa ujumla kujitambua na kutimiza wajibu wao kikamilifu.
 
Changamoto nyingine aliibanisha kuwa elimu ni ujuzi wa kumfanya mwanadamu kujitambua wapi anastahili kuwapo na siyo lazima kuajiriwa na kwa kutumia ujuzi huo watayamudu maisha ikiwamo namna ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo.
 
Naye, mwanafunzi mwakilishi wa shirika la Plan International, Catherine Kapilima, anasema watoto wa kike watumie elimu ipasavyo katika kuvivuka viunzi wanavyokutana navyo kila siku maishani.
 
Naye, Dada mkuu wa shule hiyo, Esta Costantine, alimweleza Michelle kuwa baadhi ya changamoto za jumla kwa wanafunzi hao ni kutembea umbali mrefu kufikia vituo vya daladala na wanapofika kituoni hawapewi kipaumbele jambo ambalo huwafanya wake muda mrefu au kurubuniwa na makondakta.
 
“Ninatamani kuwa kiongozi mkubwa baadaye, kwa sasa ni dada mkuu naona kuwa nimemudu nafasi hiyo na ninaweza kuongoza. Leo nimefungua uelewa wangu kuwa siyo watoto wa Tanzania pekee tunaokumbwa na changamoto za maisha wakati tunatafuta elimu bali hata nchi zilizoendelea zina changamoto zake,” anafafanua.
 
Majadiliano hayo yaliwezeshwa na serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Shirika la Plan International, yakiwa na kichwa kisemacho “Mustakabali mwema, mjadala wa kimataifa kuhusu elimu kwa mtoto wa kike, ulioandaliwa na mradi wa jarida la Galamour, wa kuwasaidia wasichana na kuwashirikisha.
 
Takwimu
 
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo wasichana wapatao milioni moja wanatarajia kuwa wameolewa katika umri wa chini ya miaka 18 duniani kote.
 
Katika Bara la Afrika,  asilimia 42 ya wasichana wote huolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18.
 
Aidha, takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) zinataja mikoa inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni kuwa ni Shinyanga asilimia  59; Tabora 58 na  Mara 55.
 
Mingine ni Dodoma 51; Lindi 48;  Mbeya 45; Morogoro 42; Singida 42; Rukwa 40; Ruvuma 39; Mwanza 37; Kagera 36; Mtwara 35; Manyara 34; Pwani 33; Tanga 29; Arusha 27; Kilimanjaro 27; Kigoma 29; Dar es Salaam 19; na Iringa asilimia nane.
 

Habari Kubwa