Viazi lishe vyamnyanua kiuchumi

08Sep 2017
Beatrice Philemon
Nipashe
Viazi lishe vyamnyanua kiuchumi
  • .Ataka watu wachangamkie fursa

VIJANA wametakiwa kujikita kwenye kilimo kilicho na tija cha viazi lishe chenye mafanikio makubwa kuliko kukaa vijiweni huku wakati mwingine wakiitwa majambazi pasipo sababu.

Wito huo umetolewa na Yonathan Piason Sehaba, mkulima kutoka Kijiji cha Kiegeya, wilaya Kilosa, mkoani Morogoro ambaye anaweka wazi kwamba kilimo hicho kitawakwamua kiuchumi kwa kupambana na umasikini na kuacha kuwa tegemezi kwa wazazi wao.

“Ukizungumzia kilimo hiki, siyo vijana wote wanakifahamu, kilimo hiki ni kizuri na chenye tija kama mkulima au kijana atafuata kanuni bora za kilimo,” anasema.

Akizungumza na Nipashe Sehaba, mkulima mwenye watoto wawili katika kijiji hicho anasema kuwa kwa muda mrefu vijana wengi wamekuwa wakisaka ajira katika mashirika na makampuni mbalimbali bila mafanikio.

Anabainisha kuwa sasa kuwa kutokana na tatizo la ajira, ni bora vijana wakajikita katika kilimo cha viazi lishe chenye tija ambacho kitawasaidia kiuchumi.

“Na hii ni kwa sababu, kwa hivi sasa taasisi nyingi zimeanza kujitokeza kufundisha wakulima maeneo ya vijijini ili kuboresha kilimo chao kutoka kile cha kienyeji kiwe cha kisasa,” anasema.

Anafafanua kwamba kupitia kilimo cha viazi lishe, kijana anaweza kulima zao hili akauza viazi, mbegu zake au kuviongezea thamani kwa kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali na bado akaendelea kupata fedha zaidi.

“Kwa mkulima au kijana anayehitaji elimu ya kilimo bora cha zao hili anaweza kuwasiliana na mimi kwa sababu tayari nimepata mafunzo ya mbinu bora za kilimo kutoka Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO), Morogoro.

Sehaba anasema kabla ya kujikita katika kilimo cha viazi lishe, alikuwa analima mahindi, viazi vitamu na mbaazi toka akiwa na umri wa miaka 18 mwaka 1980.

“Nililima mazao hayo hadi mwaka 2015 nilipoamua kuacha kilimo cha viazi vya kawaida (viazi vitamu) na kuendelea kulima mahindi na mbaazi.” Anasema

Anasema mpaka sasa analima zao la mahindi kwa ajili ya chakula na mbaazi kama zao la biashara.

Mkulima huyo anasema aliacha kulima viazi vitamu kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mbegu bora na wateja kutaka kuvinunua kwa bei ndogo ambayo haina maslahi.

“Aidha, vilianza kutostawi vizuri kutokana na ardhi kuanza kuchoka kiasi kwamba nikilima niliishia kupata gunia chache sana,”anasema.

Lakini anasema kwa hivi sasa, baada ya kupata elimu ya kilimo bora cha kisasa ameendelea kujikita katika kilimo cha mahindi, mbaazi na viazi lishe.

“Kabla ya kupata elimu ya kilimo bora, nilikuwa nazalisha gunia 25 zenye ujazo Kg 200 kutoka kwenye eka moja na bei ilikuwa inaanzia shilingi 18,000/- hadi 25,000/- kwa gunia kiasi ambacho ni kidogo sana kwa kulinganisha na nguvu nilizotumia katika uzalishaji,” anasema na kuongeza:

“Hapa nilikuwa napata hela tu ya kujikimu na ndiyo maana wakulima wengi waliacha kulima zao hili la viazi vitamu nikiwemo mimi mwenyewe.”

Sehaba anasema kwa upande wa kilimo cha mahindi aliendelea kulima kwa matumizi ya nyumbani na kwamba kwa mwaka huu alifanikiwa kuvuna gunia 20 katika eneo la ekari tatu na nusu.

Kwa upande wa mbaazi, katika msimu wa mavuno wa mwaka huu anatarajia kuvuna gunia 10 za mbaazi.

Anasema kwa mwaka huu anatarajia soko litakuwa zuri na bei itakuwa nzuri kwa sababu ukanda wa juu katika mikoa ya Dodoma, Singida na Kondoa, zao la mbaazi halikuzalishwa kwa kiwango cha kutosha kutokana na hali ya ukame, kwani mvua hazikunyesha kiasi cha kutosha katika mikoa hiyo.

“Mpaka sasa watu wameanza kuwekeza fedha tayari kwa wakulima kwa bei ya Sh. 30,000/- hadi 40,000/- kwa debe lenye kilo 20, na sisi kama wakulima wa kijiji hiki tunaona kwa mwaka huu mbaazi ina kipato,” anasema.

BIDHAA
Mbali na mazao hayo, baada ya kupata mafunzo ya kilimo bora cha kisasa Sehaba anasema ameanza kujikita katika kilimo cha viazi lishe baada kuona pia lina uwezo wa kutengeneza bidhaa zingine.

Bidhaa za aina mbalimbali kama vile juisi, biskuti, maandazi na unga wa lishe ambao una Vitamin A kwa wingi na majani yake yanaongeza damu kwa wingi kwa mtu anayetumia, lakini pia inamsaidia mkulima kujiongezea kipato.

KILIMO CHA KISASA
Mkulima huyo anasema vilevile kuwa katika kijiji chao hali imebadilika sana, kwani wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa na wameanza kulima na kupanda kitaalamu viazi lishe na mazao mengine.

Mbegu wamepata kutoka Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO).

WATEJA
Sehaba anasema kupitia kilimo hiki ameweza kupata wateja wengi kutoka mikoa ya Iringa, Kigoma na Dar es Salaam baada ya kujua faida ya viazi hivyo.

“Kwa mfano wakati wa maonyesho ya nanenane ambayo nilifadhiliwa na SUGECO kwenda kuonyesha Watanzania umuhimu wa viazi lishe na kujiongezea kipato, niliweza kupata wateja wengi sana na nilifanikiwa kuuza kilo 963 za viazi lishe vyenye thamani ya Sh. 481,500,” anasema

Anasema alifanikiwa kuvuna gunia nane kutoka kwenye nusu ekari ambayo ilikuwa na matuta 50 na zote alifanikiwa kuziuza wakati wa maoyesho ya nane nane.

“Nikiwa kama mkulima, nimefurahi kwa sababu viazi hivi vinauzika sana na wateja wengi wanavipenda kwa sababu vina lishe bora na vina uwezo wa kutengeneza juisi, biskuti, maandazi na unga lishe ambao una Vitamin A kwa wingi.” anasema.

MATARAJIO
Mwaka ujao anatarajia kulima ekari tatu ya viazi lishe kwa wingi na ametoa wito kwa wakulima wengine kuanza kutafuta mbegu kwenye wilaya ya kilosa ili waweze kujipatia vitamin A kwa afya zao na kujiongezea kipato kwa sababu vina soko zuri.

Anasema anategemea kujenga nyumba ya kisasa, kusomesha watoto wake katika shule nzuri zaidi, kuandaa kilimo chenye tija mwakani na pia kuweka akiba kwenye mifuko ya pensheni ili baadae aweze kupata msaada akiwa mzee.

“Natarajia kuanza kulipia PPF yangu mara baada ya kuvuna mbaazi zangu mwezi wa tisa na kuziuza,” anasema

WITO KWA RAIS
Ameiomba serikali ipeleke mizani kwenye vijiji ili kuondoa usumbufu kwa wakulima na wafanyabiashara ili wapate kipato chenye tija katika uchumi wa kati wa viwanda.