Vibandaumiza: Watoto waacha masomo kisa? Ngono, kandanda vibandani

24Mar 2020
Elizaberth Zaya
Mkuranga
Nipashe
Vibandaumiza: Watoto waacha masomo kisa? Ngono, kandanda vibandani

KATIKA kata ya Kimanzichana mkoani Pwani, kilio cha wananchi kwa sasa pamoja kuogopa kusambaa kwa virusi vya korona, wanatatizwa na kuanzishwa kwa utitiri wa vibanda vya video mitaani, vinavyoonyesha burudani lakini pia picha za ngono kwa watoto wadogo na wanafunzi.

Wanafunzi kusoma kwenye madarasa yasiyo na kiwango ni moja ya changamoto zinazowafanya kutoroka shuleni na kukimbilia kwenye mabanda ya video mitaani.
PICHA ZOTE: MTANDAO.

Sehemu hizo za burudani maarufu kama vibanda umiza pamoja na kuonyesha kandanda na tamthilia, vinaelezwa kuwa vimegeuka hatarishi kwa maisha ya watoto baada ya baadhi kukimbia shule na kushinda vibandani wanapojifunza mambo mengi yakiwamo masuala ya ngono.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wakati ilipotembelea Kimanzichana, wakazi hao wanasema pamoja na lengo zuri la ujio wa vibanda hivyo ni janga kwa watoto ambao hawazingatii shule.

Sihota Mchonjo, mjumbe wa serikali ya mtaa wa Lisimalike anaeleza kwamba katika siku za hivi karibuni kumeibuka kundi la watoto ambao wengine ni wanafunzi wanaoshinda katika vibanda vya video na hivyo kushindwa kusoma.

Mchonjo pia anasema mbali na kuonyesha burudani ikiwamo mpira, lakini vibanda hivyo vimekuwa vikionyesha picha za ngono ambazo hazifai kwani hupoteza watoto wadogo.

“Kwa kweli tunaomba serikali itusaidie , watoto wetu ni wadogo kushinda katika vibanda ‘umiza’ yaani kuanzia saa 4:00 asubuhi unakuta wamefungua na watoto wamejaa tele wengine ni wanafunzi tena tunawafahamu, hii si sawa kimalezi na kwa maendeleo ya taifa.”anasema Mchonjo.

“Wanatudanganya kwamba wanaonyesha mpira na tamthilia tu, lakini ni waongo, wanaweka hata picha za ngono na watoto nao wanaangalia. Kwa mfano kama mpira ni saa 10 jioni, wanachofanya kabla ya muda huo, wanaanza kuonyesha vitu vingine. Kwa hiyo mpaka mtoto atoke humo anakuwa ameangalia vitu vingi vya ajabu na tunawaona watoto wanabadilika kidogo kidogo kila siku,” anasema mjumbe huyo.

Diwani wa Kata ya Kimanzichana, Ally Kassim Ndipitipi, anasema baada ya kubaini tatizo hilo la watoto kushinda katika vibanda hivyo na wengine wakiwa wanafunzi alitoa taarifa katika Ofisi ya Mtendaji.

“Tatizo hili lipo hapa tunahitaji kulikomesha kwa sababu bila kufanya hivyo tunaharibu watoto wetu na tunazalisha kizazi cha ajabu,”anaonya Ndipitipi.

UTORO SHULENI

Nipashe lilifika katika shule moja ya msingi katika kata ya Kimanzichana na kuzungumza na mkuu wa shule hiyo, Adrian Tete, anayekiri baadhi ya wanafunzi hutoroka na kwenda katika vibanda hivyo na kwamba tayari walisharipoti suala hilo katika ofisi ya kijiji na ya mtendaji kata.

“Baadhi ya wanafunzi wakati mwingine kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, hulazimika kusubiriana nyakati za kuingia darasani, kwa hiyo katika kipindi hicho unakuta wametoroka na kwenda kwenye vibanda hivyo vya video,”anasema Tete na kuongeza:

“Tatizo hili lilianza kuwa kubwa na ikabidi tutoe taarifa kwenye mamlaka zinazohusika ikwamo ofisi za kijiji na za mtendaji, mpaka sasa hali imepungua japokuwa bado kuna wachache wanaoendelea kutoroka ambao tunapambana nao na baadhi yao tumewaita walezi na wazazi wao.”

Anaeleza kuwa wenye video wanafanya shughuli hizo kihalali, lakini inabidi mamlaka zinazohusika ziliangalie suala hili la kuruhusu watoto kuingia humo hasa nyakati ambazo wanatakiwa kuwa darasani kusoma.

WATOTO WANABETI

Mwenyekiti wa kamati ya shule iliyotembelewa ,Mohamed Mazoea, anasema taarifa hiyo ilifika hadi katika vikao vya kamati ya shule na tayari walilizungumzia suala hilo na kuripoti katika mamlaka zinazohusika.

“Huku kwetu tunalia sana na wazazi na walezi, kweli wanashindwa kuwalea watoto wao vizuri, kuna kipindi tulipata hadi kesi ya wanafunzi kutoroka kwenda kwenye hivi vibanda vinavyotumia katika michezo ya kubeti au kubashiri, ilituchanganya kweli na ilibidi tutumie nguvu kubwa sana kumpambana nao mpaka tumefanikiwa na sasa wameondoka,”anasema Mazoea.

UKAGUZI KUSHTUKIZA

Mtendaji wa Kata ya Kimanzichana, Said Abdalah Said, anasema baada ya suala hilo kufikishwa katika ofisi yake waliitisha kikao cha kamati ya shule pamoja na kushirikisha baadhi ya viongozi wa kata hiyo pamoja na kulifikisha katika kituo cha polisi cha Kimanzichana.

“Na Jeshi la Polisi lilichukua hatua kadhaa ikiwamo kuanza kufanya ukaguzi wa kushtukiza ambush ‘ambush’ katika vibanda mbalimbali,”anasema Said.

Anaeleza kuwa hawawezi kuwazuia wenye vibanda wasifanye biashara kwa sababu nao wanafanya uwekezaji huo kisheria, lakini wanachotaka wazingatie sheria, siyo kwenda kinyume na vibali vyao.

MAONI YA WANAFUNZI

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanakiri kuwapo kwa baadhi yao kutoroka na kwenda kwenye vibanda hivyo.

“Ni kweli kuna baadhi ya wanafunzi wanatoroka kwenda kwenye hivyo vibanda vya video na hulipia Sh.100 kwa muda wote wanaokaa humo,”anasema mwanafunzi mmoja wa darasa la saba katika shule hiyo ambayo jina linahifadhiwa.

Anaongeza: “Nina wadogo zangu ambao wanasoma hapahapa ambao hutoroka na wanakwenda huko, na mama yangu ameongea mpaka amechoka, kila siku anawakataza lakini hawasikii na wakirudi wanasimulia kila kitu wanachokiona huko na vingine wanavyoviangalia kwenye vibanda ni vya aibu.”

Mwanfunzi huyo anasema kuna siku aliwafuata watoto hao baada ya giza kuingia na alipoingia alikuta wanaonyesha picha za ngono, akawabeba na akawasemea kwa wazazi wao.

SHULE NYINGINE

Mkuu wa Shule, Victor Marisha, mwalimu katika shule jirani, anasema tatizo la watoto kutoroka na kwenda katika vibanda vya video ni miongoni mwa matatizo yanayowatesa.

“Hili linatutesa sana katika shule yetu, tumelazimika kuunda timu ya wanafunzi wenye nidhamu ambao wamekuwa wakishirikiana na mwalimu wa nidhamu kwenda kuwafuatilia wanafunzi wanaotoroka kwenye vibanda hivyo, na tumesharipoti kwenye uongozi wakijiji,”anasema Marisha.

USTAWI WA JAMII

Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mkuranga, Foibe Peter, anasema watoto kushinda kwenye vibanda vya video katika halmashauri hiyo ni kubwa na wamekuwa wakipambana nalo mara nyingi.

“Hilo tatizo haliko sehemu moja tu, karibu kila sehemu ya Mkuranga kuna shida hiyo na linatutesa sana huku, na limechangia kwa kiwango kikubwa kuharibu watoto kwa sababu huko ndiko wanajifunza mambo ya ajabu kweli kweli,”anasema Peter.

Anaongeza kuwa watoto wanajifunza mambo mabaya na kupotoka kwenye vibanda umiza na tatizo kubwa hata wanapotoa elimu kwa jitihada zote wazazi nao hawatekelezi wajibu wao hivyo kuwapa walimu mzigo mkubwa.

Anasema tatizo jingine linalochangia watoto katika eneo hilo kujifunza mambo mabaya ni pamoja na wazazi kutengana na kukosa malezi ya pamoja, watoto kuishi na bibi zao ambao wengi wao hawana nguvu ya kuwafuatilia.

WENYE VIBANDA

Mmiliki wa kibanda cha video au kibanda umiza katika eneo la Kimanzichana ambaye alikataa kutaja jina lake, anasema hawawalazimishi watoto kuingia katika vibanda hivyo, isipokuwa wenyewe ndiyo hulazimisha kuruhusiwa kuingia na kutizama picha.

“Sisi tunafahamu masharti tuliyopewa ya kufanya biashara hii, hatuwezi kulazimisha watoto waingie isipokuwa watoto wenyewe ndiyo wabishi. Unakutana na katoto kanakuja kanalazimisha, ukikakataza kanakwambia mbona mama ameniruhusu na amenipa hela ya kuingilia wewe ni nani unanikataza? Wengine wanakuja na mzazi kwa hiyo ongeeni na wazazi wao wawakataze na siyo kutulaumu sisi,”anasema.

OFISI YA UTAMADUNI

Ofisa Utamaduni Halmashauri ya Mkuranga, Boppe Kyungu, anasema sheria ya utamaduni inawataka wamiliki wa vibanda vya video kuonyeshwa kuanzia saa 10 jioni.

“Hakuna sheria inayoruhusu vibanda vya video kufunguliwa kabla ya saa 10 jioni, lakini pia sheria ndogo ya halmashauri hairuhusu watoto chini ya umri wa miaka 18 kuingia kwenye vibanda hivyo, wanakiuka utaratibu kwa sababu hata vibali walivyopewa havionyeshi hivyo,”anasema Kyungu.

Habari Kubwa