Vibonde walivyoanza kuamka Ligi Kuu

14Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Vibonde walivyoanza kuamka Ligi Kuu

HALI ya hatari imeanza kuikumba Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya zile timu zilizokuwa zikionekana kama vibonde kuamka na kuanza kushinda kwenye mechi zao.

Wachezaji wa Alliance FC ya jijini Mwanza wakishangilia moja ya magoli yao kwenye mechi za Ligi Kuu Bara ambayo imeingia katika mzunguko wa pili. PICHA: MAKTABA

Kutokana na hali hiyo, timu zingine zilizopo juu ya timu hizo zimeshaanza kupata matumbo moto, kwa kuwa ushindi wa timu za chini umezifanya kuwa na kazi ya kuanza kuzikimbia, vinginevyo hatari ya kuteremka daraja inaweza kuwakuta, badala ya zile timu zilizokuwa zikifungwa kwenye mzunguko wa kwanza.

Hali hii itasababisha mechi za mzunguko wa pili kuwa ngumu zaidi kuliko ule wa kwanza.

Kwa matokeo hayo na msimamo jinsi ulivyo kwa sasa hakuna timu yenye uhakika ukiondoa timu za Simba, Yanga na Azam, yenye uhakika wa kubaki katika Ligi Kuu msimu ujao.

Tayari baadhi ya timu zimeshaanza kucheza mzunguko wa pili, huku zingine zikiwa bado hazijamaliza ule wa kwanza.
Hizi ndizo timu ambazo mzunguko wa kwanza hazikufanya vyema, lakini sasa zimeshtuka na kuanza kuzinduka kipindi hiki.

1. Alliance FC
Ni timu ya jijini Mwanza ambayo kwa muda mrefu wa mzunguko wa kwanza imekuwa haipati ushindi hadi pale, ilipomtimua kocha wake, Mbwana Makata na kumchukua kocha Malale Hamsini aliyekuwa akiifundisha Ndanda FC.

Awali ilionekana kama ni timu itakayoshuka daraja kirahisi na kurudi ilikotoka.

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United ya Mara, ikaichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, sare ya bao 1-1 dhidi ya Stand United, pia sare ya bila kufungana dhidi ya Mbao FC, kabla ya kuibamiza Ruvu Shooting mabao 3-0, umeifanya timu hiyo kujiondoa kwenye eneo la hatari na sasa inakamata nafasi ya 12, ikiwa na pointi 24 kwa michezo 21 ambayo imecheza mpaka sasa.

Timu hii imeonekana kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani, Nyamagana.

2. Biashara United
Pia timu hii yenye maskani yake mjini Musoma, Mara imepanda Ligi Kuu msimu huu na haikuwa kwenye hali nzuri tangu mwanzo.
Ilishinda mechi ya kwanza ya ufunguzi dhidi ya Singida United, tena ikiwa ugenini Uwanja wa Namfua bao 1-0, kila mmoja akitegemea kuwa ingefanya maajabu. Badala yake ikageuka kuwa nyanya na kugawa pointi kama njugu.

Biashara United ikacheza mechi 16 bila kushinda mechi yoyote ile.

Hata hivyo, Januari 2 mwaka huu, iliibuka baada ya kufanya marekebisho kwenye benchi lake la ufundi na kuichapa Mbeya City mabao 2-1 ikiwa nyumbani, ikishinda kwa mara ya kwanza hapo, tangu ilipopanda Ligi Kuu.

Kwa sasa bado inashika mkia ikiwa na pointi 14, ikicheza mechi 19, lakini inaonekana imeshaibuka, hivyo kuziweka timu zilizokuwa juu yake kwenye tahadhari.

3. Tanzania Prisons
Moja ya timu zinazoshangaza kwenye Ligi Kuu msimu huu ni Maafande hao wa jijini Mbeya.

Inajulikana kama ni moja kati ya timu ngumu mno kwenye Ligi Kuu, lakini msimu huu ni tofauti. Imekuwa timu dhaifu na imeshindwa kupata ushindi kwa muda mrefu.

Mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni Septemba Mosi mwaka jana, ilipoichapa Alliance mabao 2-0. Haikushinda tena mechi yoyote ile hadi Jumanne iliyopita ilipoichapa timu ngumu ya Mtibwa Sugar mabao 2-0.

Hii inaonyesha kuwa tayari wameshajua makosa yao na mzunguko wa pili timu zisitegemee mteremko wa Prisons kwa kuwa haitokubali kushuka daraja kirahisi. Inakamata nafasi ya 19 ikiwa na pointi 15, pointi ambazo huku timu zingine za juu yake zikiwa hazina idadi kubwa ya pointi ambazo zinaweza kumfanya akate tamaa.

4. African Lyon
Ilionekana ni kibonde kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu. African Lyon nayo ni moja kati ya timu zilizopanda daraja msimu huu, ingawa imekuwa na tabia ya kupanda na kushuka.

Baada ya kukaa mkiani kwa muda kadhaa, Januari 6 mwaka huu iliifumua Stand United mabao 2-0 na kuifanya kusogea hadi nafasi ya 18 ikiwa imecheza mechi 21 na pointi zake 16.

Matokeo ya mechi zake za hivi karibuni imeonyesha kuwa, imebadilika na wala si ya kuichukuliwa poa, hivyo timu zingine zilizo juu yake matumbo moto.

5. Mwadui FC
Ilipambana sana kupata ushindi katika mzunguko wa kwanza. Ilikuwa ni moja kati ya timu zenye sare nyingi kwenye Ligi Kuu.
Lakini pia ilikuwa chini-chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, baada ya kipindi cha dirisha dogo kufanya usajili, imegeuka kuwa timu tishio ghafla.

Ilitoa vipigo viwili vikali vya mabao 3-0 dhidi ya Ndanda na mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar na hivi sasa inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiondoka kabisa kwenye ukanda wa hatari, ikiwa na pointi 24 sasa kwa mechi 22 ilizocheza.

Habari Kubwa