Vigogo Afrika wanaweza kuchomoka akaunti za siri ughaibuni?

06Apr 2016
Dar
Nipashe
Vigogo Afrika wanaweza kuchomoka akaunti za siri ughaibuni?

WAKATI nchi ikiwa kwenye taharuki kubwa kutokana na ‘kasi’ ya utumbuaji majipu unaoendelea kwenye sekta mbalimbali za umma, kambi ya upinzani haioni matokeo ya maana ya utendaji huo.

Rais Idriss Deby, wa Chad.

KATIKA kile kinachoweza kuelezwa kama ‘WikiLeakes’ namba mbili, lakini safari hii ikiwa siyo ile ya mwanzilishi wake, Julian Assange, ambaye hadi leo bado anaishi maisha ya ukimbizini kwenye ubalozi wa Ecuador jijini London, nchini Uingereza, dunia tena imejikuta katika aina nyingine ya WikiLeaks.

Lakini safari hii siyo ile ya Assange tena, bali ni ya ufichuaji wa taarifa zilizo ‘ndani ya kapeti’ kutoka chanzo kingine tofauti, zilizoibuka mwishoni mwa wiki iliyopita.

Labda kwa kukumbushana tu, WikiLeaks ni shirika la habari ambalo haliko kibiashara, lenye lengo la kuupatia umma habari muhimu ambazo wakati mwingine ni za ‘chini ya kapeti’ ama za siri kabisa.

Katika kutekeleza ufichuaji wa habari hizo zenye maslahi kwa umma, WikiLeaks hutumia njia salama na zenye ubunifu kwa vyanzo vya habari kuvujisha habari kwa waandishi wake.

Na katika moja ya habari za siri zilizotolewa na shirika hilo na kusababisha sintofahamu kubwa duniani, ni pale ilipotoa taarifa mbalimbali za siri kuanzia mwaka 2010, zikihusisha pia serikali ya Marekani.

Hali hiyo ilisababisha Assange asakwe na nchi Marekani, kabla ya kubambikiwa tuhuma ya kesi za kubaka nchini Norway, akiwa Uingereza, hali iliyosababisha akimbilie ubalozi wa Ecuador na kuomba hifadhi, anakoishi hadi sasa.

Kama ilivyoelezwa hapo juu, safari hii siyo WikiLeaks na habari zake, ila ni juu ya ufichuaji mkubwa wa akaunti za siri za watu matajiri duniani.

Hii inawagusa viongozi wa dunia, nyota wa michezo na filamu, wakiwa ni miongoni mwa matajiri kadhaa waliotajwa katika kile kinachoweza kuwa ufichuaji mkubwa zaidi wa taarifa za ndani katika historia.

Ufichuaji huo mkubwa unaohusisha nyaraka milioni 11.5 na umepewa jina la ‘Panama Leaks’.

Ufichuaji huo umeonyesha namna matajiri wanavyotumia maeneo salama ya kodi, kuficha utajiri wao na kukwepa kodi.
Uchunguzi uliofanywa na zaidi ya kampuni 100 za habari umefichua mali zilizofichwa nje zinazomilikiwa na watu mashuhuri duniani, wakiwamo wanasiasa karibu 140.

Nyaraka hizo zililifikia gazeti la kila siku nchini Ujerumani, la Süddeutsche Zeitung, na kusambazwa kwa makampuni mengine ya habari ulimwenguni.

Nyaraka hizo zilisambazwa baada ya kulifikia gazeti la Süddeutsche Zeitung na Jukwaa la Kimataifa la Waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ).

Nyaraka hizo zinazoyahusu mashirika karibu 214, 000 ya nchi za kigeni kwa muda wa karibu miaka 40, zilitoka kwa kampuni ya uwakili ya Mossack Fonseca, yenye makao yake nchini Panama, katika jiji la Panama City.
Kampuni hiyo ina ofisi kwenye zaidi ya mataifa 35 duniani.

WATU MASHUHURI
Miongoni mwa watu mashuhuri waliotajwa kuwamo kwenye kashfa hii ni pamoja na Rais Vladmir Putin wa Urusi, Rais Xi Jinping wa China na mcheza filamu mashuhuri Jackie Chan.

Rais Putin anatajwa na uchunguzi, kutokana na madai kuwa washirika wake wa karibu, walishiriki kwenye mchezo huo mchafu.

Hata hivyo, nyaraka hizo hazikumtaja yeye binafsi kushiriki kwenye mchezo huo.

Washirika wake wa karibu wanatajwa kuwa walihamisha kwa siri kiasi cha dola za Kimarekani bilioni mbili, kupitia mabenki na kampuni hewa.
Aidha, nyaraka hizo za siri zimewataja viongozi 12 walioko madarakani na wa zamani katika uchunguzi huo, wakiwamo waziri mkuu wa Pakistan, rais wa Ukraine na Mfalme wa Saudi Arabia.

Wachunguzi wamedai pia kuwa, familia ya Rais Jinping ina uhusiano na akaunti za nje, kama ilivyokuwa kwa marehemu baba wa waziri mkuu wa sasa wa Uingereza, David Cameron.

Aidha inadaiwa kwamba, waziri mkuu wa sasa wa Iceland aliwekeza kwa siri, mamilioni ya pesa kwenye benki za nchi hiyo, wakati wa mgogoro wa kifedha.

Mkurugenzi wa Jukwaa la ICIJ, Gerard Ryle, amesema kinachoshtua zaidi ni namna ulimwengu wa nje unavyotumiwa na viongozi walioko madarakani, ambao baadhi yao wamekuwa wakijitanabaisha kuwa wapinzani wakubwa wa usiri.

“Tunachopaswa kufanya hapa kama waandishi habari ni kuvunja usiri kwa sababu bidhaa pekee inayotolewa na ulimwengu wa nje ni usiri na bila hivyo basi hakutakuwa tena na bidhaa hivyo kadiri tunavyoendelea kuwafedhehesha watu, nadhani tutaona mageuzi ya kweli," alisema Ryle.

WATEJA WA MOSSACK FONSECA
Kampuni ya uwakili ya Mossack Fonseca ilifanya kazi na watu wasiopungua 33 na kampuni zilizoorodheshwa na Marekani kuwa na uhusiano wa kibiashara na magenge ya wauza dawa ya kulevya nchini Mexico, makundi ya kigaidi na mataifa sugu, likiwamo taifa la Korea Kaskazini.

Moja ya kampuni hizo ilitoa mafuta kwa ajili ya ndege za utawala wa Syria, zilizotumiwa kuwashambulia raia wake.
Wateja wa kampuni hiyo wanahusisha wawekezaji wa uongo, magwiji wa dawa za kulevya, wakwepa kodi na mfanyabiashara wa Marekani aliyetiwa hatiani, baada ya kwenda nchini Urusi kufanya ngono na watoto yatima walio chini ya umri wa miaka 18, ambaye alisaini nyaraka za kampuni ya nje akiwa gerezani.

Wadadidi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa ni vigumu kwa viongozi au wanasiasa wa Afrika kutokuwamo kwenye kashfa hiyo kutokana na kasumba ya uongozi barani humu.

Wanasema mara kadhaa, viongozi wa Afrika wamekuwa wakituhumiwa na wenzao wa Ulaya na kwingineko kwa kuiba mali za raia wao na kuzificha ughaibuni.

Zaidi ya benki 500, benki zake tanzu na matawi mbalimbali yamefanya kazi na kampuni ya Mossack Fonseca tangu miaka ya 1970, kuwasaidia wateja wao kusimamia kampuni za nje.

Hii ndiyo kashfa kubwa iliyoibuka mwishoni mwa wiki, ikihusisha akaunti za siri za matajiri wakubwa, wengine wakiwa karibu na viongozi wanaoongoza mataifa makubwa duniani.

Habari Kubwa