Vigogo wa afya DSM lini mtafanya kitu roho inapenda ?

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Vigogo wa afya DSM lini mtafanya kitu roho inapenda ?

BILA kuwa na mipango ya maendeleo isiyohofu kuudhi au kukasirisha watu fulani kutokana na kuchukua hatua au kuamua kufanya suala linalolinda maslahi ya umma, ni wazi kuwa taifa haliwezi kuendelea kwa kasi na viwango vinavyotakiwa.

Ulaji na uuzaji wa vyakula jijini Dar es Salaam usiozingatia sheria za mtu ni afya wala kuhofu magonjwa.

Tunaafikiana kuwa umaskini ni tatizo lakini pia hatukubaliani kuwa kwa vile kuna ufukara basi kila mtu afanye apendavyo ili apate riziki.

Tukubaliane kuwa kila mmoja akifanya apendavyo gharama inakuwa kubwa kuwasaidia hao walioathirika na ulegevu wa sheria ama maamuzi ambayo yalifanywa na watu waliokuwa na hofu.

KULA VYAKULA VISIVYORIDHISHA

Nizungumzie ulaji na uuzaji wa vyakula jijini Dar es Salaam usiozingatia sheria za mtu ni afya wala kuhofu magonjwa. Hivi ni kwanini kila mtu ni mama , baba lishe kwenye mji huu?

Hofu pengine inakuwa mamlaka zikiwafukuza ama kuwakataza zitachukiwa na wananchi, hali inayohofiwa itatishia ustawi wa kisiasa kweli?

Ukifika katikati ya jiji utakutana na wanawake wanauza vyakula chini ya miti kwenye kituo cha Posta mpya. Hili ni eneo lenye vumbi, harufu ya maji taka hasa kwenye msimu wa mvua. Vitafunwa huwekwa juu ya ndoo na magazeti. Vingine viko ndani ya mabeseni. Wengine huuza samaki wa kukaanga chakula kinachoalika inzi.

Daladala zinapofunga breki zinanyunyiza vumbi jingi kwenye vitafunwa na pia moshi wa injini unazidi kukoleza athari kwa afya za walaji. Vumbi hili limejaa mayai ya minyoo na hata vimelea vya magonjwa. Linapotua kwenye chapati, maandazi, samaki , vitumbua na kila kinachouzwa eneo hilo, naamini haliwaachi walaji hao salama.

Hivi huko ndiko kuwafanya wananchi wakubaliane na sera za nchi za kujiajiri? Ofisa Afya wa Jiji tukubaliane kuwa unatakiwa kuchapakazi vya kutosha kama ulivyofanya wakati wa ujio wa kigogo fulani miaka kadhaa iliyopita. Kama una majibu kwanini wakati ule uliwaondoa wafanyabiashara hao tuambie. Unadhani walikuwa hawafai ama ilionekana biashara ile ni ya aibu isiyozingitia ustaarabu na haistahili kuonekana na watu wa mataifa makubwa? Au ilikuwa ni kwa sababu wako chini ya mti na mazingira ni machafu?

Lakini tafiti zinazofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na taasisi za tiba za binadamu mbona hazijaibua vyanzo vya maradhi hasa ya tumbo- minyoo, homa ya tumbo, kuhara , kutapika, kuhara damu kuwa ni mazingira machafu na kula vyakula duni magengeni, kuuza matunda kwenye makarai na mabeseni?

Maofisa afya wa Jiji fanyakazi kwani kuwaachia watu kufanyabiashara za vyakula wanavyotaka ili kumudu maisha yao kunarejesha tena ugumu wa kupata huduma za afya mahospitalini ambazo kama usafi wa vyakula ungezingatiwa maradhi hayo na haja ya kutibiwa isingekuwapo.

 

JUISI YA MIWA

 

Hivi haiwezekani kuzizuia biashara holela za kuuza juisi za miwa michafu, isiyooshwa bali kukwanguliwa kidogo kuondoa rangi nyekundu licha ya kutupwa chini kwenye madimbwi ya maji taka Tandale?  Hivi haikustahili kuoshwa? Ofisa afya hujawahi kuona kuwa juisi ya miwa ni chafu, imejaa inzi, tena inashikwa na mikono michafu kila miwa inapokamuliwa?

Jamani ni kero pweza wanaonuka huuzwa kila mahali.Tena hupangwa juu ya meza mbovu na chafu. Ni aibu.

Jiji hebu jaribuni kulinda afya za walaji wekeni viwango.Inakuwaje vyakula vinapikwa na kuliwa popote ? Jengeni basi migahawa ya muda ya kisasa na kuweka maelezo kuwa ili mtu afanye biashara  eneo hilo anatakiwa kulipia kiasi fulani.

Wekeni bango na mgambo wa jiji lenye maandishi “ili uuze chakula hapa changia kwanza Sh. 50,000 zifanikishe kukodisha eneo la mgahawa la kutoa huduma za mama lishe .Jaribuni pengine wajasiriamali hao wakichangia itawezekana kupata fedha za kukodi moja ya ukumbi kubwa kwenye maghofa ya kisasa yanayojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ili kuboresha maisha ya wanawake hawa na Watanzania ambao ni wateja wao wakubwa hasa madereva,makondakta , wapiga debe wa daladala na wamachinga wanaozurura mjini kufanyabiashara.

Lakini, uchafu wa vyakula unaonekana pia kwenye viwanda vya mikate. Bi na Bwana Afya wa Jiji angalieni vitafunio wanavyokula wananchi wenu.

Hizo bekari ni chafu ukiingia mlangoni unakutana na kinyesi cha mbwa cha wiki nzima. Hivi kama wanakanyaga kinyesi wakiingia kiwandani mna uhakika gani na mikate yao?

Tena chunguzeni mikate inawekwa ndani ya mifuko myepesi ya nailoni inayotupwa chini.Huko wenye viatu vichafu hupita na hakuna anayezingatia usafi na afya.

Vyoo kwenye hizi bekari ni vichafu kama ambavyo choo cha wateja kwenye baa nyingi za mji huu na migahawa mingi hapa Dar es Salaam.

Wakala wa Usalama mahali pa kazi (OSHA) fanya ukaguzi usiwaachie watu wengine kufanya biashara kujipatia kipato kwa kuwaumiza walaji.Hapa tunamaanisha maradhi.

Bibi/Bwana afya wa Jiji katika eneo ambalo linawafanya wakazi wengi wa Dar es Salaam kulalamika ni kuachilia vyakula kuuzwa barabarani, sehemu zisizo na vyoo kuruhusu watu hao kujiaminisha kuwa kila mahali ni jikoni bila kuwa na choo cha wateja na maji kwa ajili ya kufanya usafi.

Hawa wazee wa afya wa jiji wanajua kuwa maduka yanayouza bia mitaani wateja wanatumia vyoo vya familia? Tukabaline kuwa hamfanyi ukaguzi wala kusimamia usafi wa chakula ipasavyo pasi kupata kushinikizwa la vigogo kutoka juu.

Jamani changamkeni hivi hamuwezi kuwaagiza wanaouza juisi na kahawa kutumia glasi‘dispozabo’ na kila mteja anayetumia huduma aombe kupewa glasi dispozabo tena safi?

Mabwana na mabibi afya hakikisheni wajasiriamali wanawajibika kwenye biashara zao ili kulinda afya za walaji.

 

NYAMA YA MAGOGO

Nawaulizeni tena hivi tutaendelea kula nyama zinazokatwa juu ya magogo mpaka lini?

Duka la nyama lina msumeno lakini pembeni kuna magogo kadhaa yaliyojaza  mabucha badala ya majokofu ya kutunzia nyama , tunawauliza hili ni mpaka lini?

 Lile agizo la kukata nyama na msumeno limetekelezwa lakini magogo yanatumika sana na ukiuliza utaambiwa msumeno umekorofisha. Kumbe si lolote.

Tuambieni tutakula nyama za magogo hadi lini? Waambieni watoe magogo mabuchani. Tukiingia duka lina msumeno lakini wanakatia magogo ukihoji unaambiwa ni mashine ni mbovu.

Hivi tunavyotaka mrekebishe ni kidogo kuna mengi mengineyo hebu mbadilike mtakuwa mkifanyakazi hivi mpakalini?

Tuna mengi kuanzia uchafu wa huduma ya vyoo vya kulipia, machinjio yasiyofaa kutumiwa kuandaa kitoweo na msururu mrefu wa mambo yanayoleta kero.

Tunawaomba mfanyekazi mbona mnaweza. Heri ya mwaka mpya 2019.

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa