Vijana 5,000 wakusanywa, waingizwa kwenye kilimo

08Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Vijana 5,000 wakusanywa, waingizwa kwenye kilimo
  • Mradi wa ubia wasomi wa Costech, Chuo Kikuu Michigan
  • Walengwa chini ya miaka 24, kundi lililosahaulika

UKOSEFU wa ajira kwa vijana wengi imekuwa tatizo kubwa nchini na dunia nzima. Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 60 ya vijana barani, Afrika hawana ajira.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha Afrika ndio inaongoza kwa kuwa na vijana wengi, huku ikitazamiwa kundi hilo kuongezeka.

 

Chuo Kikuu cha Michigan State cha nchini Marekani kwa ubia na mashirika ya Sugeco, IITA na Tume ya Sayansi na Technolojia (Costech) kupitia Kitovu cha Ubunifu cha Buni, kwa pamoja wamra,au kutekeleza mradi uitwao Agrifood Youth Lab, unaolenga kuwakwamua na kuwawezesha vijana wa nchini.

 

Ni mpango unaoenda sambamba na dira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli, kuelekea kwenye Tanzania ya Viwanda.

 

Ni mtazamo unaolenga kupunguza pengo la ukosefu wa ajira nchini kwa vijana, kupitia kinachoitwa ‘minyororo ya thamani ya sekta ya kilimo na ufugaji.’

 

Akizungumza na Nipashe, wakati wa majadiliano ya kundi lengwa yaliyowashirikisha wadau mbalimbali, zikiwemo kampuni binafsi na vijana, iliyoenda sambamba na uzinduzi wa utekelezaji wa mradi huo hapa nchini, Mshauri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Michigan, Julie Howard ana mengi ya kufafanua.

 

Julie ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa taasisi ya AG Youth Lab, anasema mradi huo umelenga vijana wenye umri kati ya miaka 18-24, ikiamini ndilo lililosahaulika katika jamii.

 

"Hili ni kundi ambalo idadi yake imekuwa ikiongezeka kwa kasi barani (Afrika), huku likiwa na mahitaji makubwa kiuchumi na limetengwa. Hii ndio sababu iliyopelekea kuligeukia kundi hili kwa kulipa kipaumbele," anasema Julie.

 

Maeneo ya mradi

 

Anauleza mradi unalenga kufanya kazi kwenye minyororo mitano ya thamani, anayoitaja kuwa ni: Ufugaji kuku, kilimo cha muhogo, ufugaji samaki, kilimo cha Mboga na matunda, na kilimo cha mbegu za mafuta.

 

Mradi unaendeshwa na Chuo Kikuu cha Michigan na washirika wake umefadhiliwa na taasisi ya MasterCard.

 

Mratibu wa mradi huo nchini,Jerry ichael ana ufafanuzi:" Mradi huu umelenga kuwafikia zaidi ya vijana 5,000 nchini na watapata mafunzo mbalimbali, ikiwa ni kwa nadharia na vitendo ili waweze kufikia fursa mbalimbali za ajira na pamoja na kujiari.

 

“Hii ni kwa sababu waajiri wengi wamekuwa wakianisha changamoto mbalimbali zinazofanya vijana wengi kukosa ajira. Lakini, vijana nao wanadai kuwa na vigezo vyote, ingawa wanashindwa kuelewa ni kwa nini wanakosa ajira.

 

“Kwa hiyo mradi unakuja kuwa daraja kati ya vijana (waajiriwa) na waajiri, pia kuwaunganisha vijana na fursa nyingine mbalimbali za kujiajiri, katika sekta ya kilimo na ufugaji hususani katika minyororo ya thamani iliyoainishwa"

 

Jerry anasema maeneo ya minyororo hiyo mitano imelenga mikoa ya Pwani na Morogoro ikishirikiana na Dar es Salaam.

 

"Hii ni kwa sababu Dar es Salaam ndipo soko lilipo, kwa hiyo hawa watakaoweza kujiajiri wataweza kupata soko la bidhaa zao kwa urahisi, kutokana na idadi kubwa ya walaji katika mkoa hauna fursa za kuajiriwa,”

Anasema, huku akiiongeza mradu unawealenga vijana wasio masomoni.

 

"Tumezoea miradi mingi ikija, tunafanya kazi na vijana ambao wengi wao wanakuwa wamemaliza vyuo vikuu na tayari wanakuwa wameshapata fursa nyingi" anaongeza Jerry.

 

Agrifood Youth Lab(AYL), katika mkakati wake, inasema wananuia kuanza na kundi la vijana wadogo ambao ni rahisi kuwabadilisha kimawazo yao na hata kuwaongoza kirahisi.

 

"Kwa ufupi mradi huu ni tofauti kabisa, si sawa na mingine, ila ni kwa vijana ambao watakuwa na utayari. Vijana watarajie mradi,” anasema.

 

Anataja vigezo kuwa ni umri wa miaka 18 hadi 24, hajaajiriwa na waliojiajiri ni wenye kipato cha wastani wa dola mbili za Marekani, sawa na Shilingi 4,400.

 

Jerry anataja sababu za kuchagua kada hiyo, kwamba ndiko inakopatikana rasilimali kwa urahisi, pia ni karibu na maeneo ya masoko.

 

"Ukiangalia Morogoro imezungukwa na Dodoma na serikali inahamia Dodoma. Hapo kutakuwa na uhitaji mkubwa wa chakula hivyo hata soko la mkoa huo litakuwa ni kubwa. Ukiangalia mkoa wa Pwani uko karibu na Dar es Salaam na wengi tunaoishi kwenye mkoa huu ni walaji na si wazalishaji wa chakula.," anafafanua.

 

Jerry, anasema tafiti zilizofanyika, zimechangia katika maamuzi ya kuufanya mradi huo katika mikoa ya Pwani na Morogoro.

 

"Tulitamani kufika kwenye sehemu nyingi, lakini ukiangalia kuna miradi mingine inayofanana na huu imeanzishwa katika maeneo hayo mengine. Hivyo hatukutaka kurudia kile kinachofanywa kwenye maeneo hayo, hivyo tutaanzia tulipo na kuendelea sehemu nyingine zenye uhitaji," anafaanua Jerry.

 

 

Kutoka kwa Wajasirimali

 

Veronica John, mjasiriamali kutoka Kibaha, ni kati ya vijana waliopata fursa ya kushiriki majadiliano ya kundi lengwa yaliyoandaliwa na mradi wa Agrifood Youth Lab, anakiri kujifunza mengi.

 

Anataja baadhi kuwa ni fursa za kilimo cha muhogo na vitu vitakavyoweza kusaidia kuwezesha kupata malighafi.

 

"Kwa kutumia zao la muhogo, unaweza kuongeza mnyororo wa thamani kwa kusindika unga wa muhogo kwa ajili ya kula na kuuza, pia unaweza kuuza mbegu," Veronica anasema.

 

Pia anataja dhana ya namna ya kujiajiri na kuajiriwa katika ujasiriamali ni sehemu ya kunufaika.

 

Veronica anawashauri wadau hao kuwaendeleza vijana katika ujasiriamali, kutokana na fursa walizozipata kupitia mafunzo katika sekta za kilimo, ufugaji, jambo litakalofungua fursa zaidi za ajira, hivyo kujiepusha na vishawishi mbalimbali vya kijamii kuligana na umri wao.

 

Juma Nyamgunda,ni mkulima na mjasiriamali kutoka kikundi cha Cassava Processor Group, cha Mkuranga mkoani Pwani, ana maoni:"Niimevutiwa sana na kujifunza mengi kutokana na majadiliano niliyoshiriki kupitia mradi huu wa Agrifood. Mengi yalikuwa ni changamoto.

 

“Miongoni mwa mambo ambayo nimejifunza, yanaonyesha kuleta mwanga na mafanikio katika utendaji baada ya mradi huu kuanza," anasema.

 

Nyamgunda anafafanua kuwa sehemu kubwa ya vijana wamepewa fursa ya mafanikio, kutokana na uwepo wa mradi huo wa miaka mitano nchini, kwa kufungua milango ya ajira.

 

Nyamgunda anakieleza kikundi chao kichojishughulisha na kilimo cha muhogo na usindikaji, kwa kuongeza thamani ya zao hilo.

 

Rai yake ni kwamba, iwapo vijana watapata elimu ya kutosha kwenye mambo hayo, wana matarajio ya kupata mafanikio makubwa zaidi.

 

Anatoa mfano wa zao la muhogo, ambalo awali lilichukuliwa kuwa chakula pekee, sasa una matumizi mengi.

 

"Kwa vijana watakaobahatika kuchaguliwa kushiriki kwenye mradi huu, kwao ni fursa muhimu sana ambayo wanapaswa kuichukua na kuichangamkia.

 

“Kwa wale wanaomaliza elimu hii ya msingi, kutawasababishia kupata ajira na kujiongezea kipato kwa maisha yao na familia zao kwa ujumla" anasema.

 

Nyamgunda, anasema "iwapo mradi utawasaidia kupitia vikundi vyetu mathalani kama kikundi chetu ambacho kinajishughulisha na mambo ya usindikaji kuna ajira mbalimbali ambazo zitakuwa zikitokea. Hizi zote ni kazi ambazo zinaweza kuwapa ajira vijana na kuweza kuongeza kipato kwenye familia zao."

 

"Hivyo, iwapo vijana hawa watapewa elimu hii na wakaiaminisha elimu hii kwa jamii kama wanavyoamini wao italeta matokeo chanya katika siku za usoni.

 

“Kwasababu kadri vijana hawa waliopata elimu ya ujasiriamali watakavyokuwa wakikuawa vizazi na vizazi vitaendelea kupata elimu na ushuhuda zaidi na watu watakuwa wakirithi. Ajira zitaongezeka na umasikini utakuwa ukipungua zaidi kwenye jamii," anaeleza.

 

Mshiriki mwingine, Abdulrazack Jumanne, kutoka Kongowe, Kibaha, ambaye ni mjasiriamali anayeuza maji,anasema alipoanza kuhudhuria mafunzo hayo, aliona vingi vipya na tofauti,

 

Anataja mojawapo kuwa ni kwamba, kilimo kinaweza kumfanya kijana kuinuka kiuchumi kutoka hatua moja hadi nyingine.

 

"Kutokana na majadiliano ya mradi huu, nimeona faida ambazo vijana tunaweza kufaidika nazo, kwani kupitia kilimo tunaweza kufanya biashara takriban kila siku.

 

“Kwa mfano kupitia zao la muhogo, huweza kutumika kuzalishia unga ambao hununulika kila siku kwa matumizi ya kupikia ugali. Hata unapoamua kuwekeza kwenye kilimo cha muhogo maisha yako yanaweza kubadilika," anafafanua.

 

Jumanne sasa anaahidi kuwa balozi wa mradi huo, kuwaelezea vijana wenzake fursa zilizopo katika kilimo, badala ya kubweteka tu.

 

"Vijana wengi hatupendi kujihusisha na kilimo kwa sababu hatupewi nafasi, hii ni kutokana na kudharaulika," anasema.

 

Ushauri wa Jumanne kwa vijana wenzake waliopata fursa ya mafunzo ya mradi wa AG Youth Lab, kufuatilia kwa makini wanayofudishwa na kisha kuwa mabalozi wazuri wa maelekezo hayo.

 

Mshiriki huyo anaeleza matarajio yake kuwa ni kujikita katika kilimo na kujitahidi kufika nacho mbali akiongeza ni mradi unaowagusa vijana wengi

 

"Kwangu hii imekuwa bahati na huwa bahati haiji mara mbili na ninaomba Mungu nilichojifunza kisipotee bure," anasema!

 

Mwamvua Mlangwa au Mwammy, ni mkulima kutoka kikundi cha Hydro-phonic farming, anaiomba asasi ya Agrifoos Youth Lab, kutanua wigo wa mafunzo ya kuwezesha vijana nchini kuifikia mikoa yote.

 

"Ninapongeza Mradi huu wa Agrifood Youth Lab kwa kuanzisha mpango huu ulioanza kwenye mikoa ya Morogoro na Pwani. Lakini, niiombe ifikirie kutanua wigo hadi kuifikia mikoa mingine nchi nzima kwani Tanzania ina idadi ya watu takribani milioni 50 na kati yao asilimia 76 ni vijana. Hivyo itapendeza zaidi kama tutaifikia mikoa mingine pia nchi nzima," anasema Mwajuma anasema.

 

Mtaalam Ushauri

 

Gloria Kavishe, ni Mtaalam Ushauri wa Maendeleo, pia binafsi anajitambulisha kuwa mfugaji kutoka kinachoitwa ‘Nuru Farm’ huko Bagamoyo.

 

Anasema anafuga samaki aina ya sato katika kundi lao wakiwa na mabwawa matatu yenye uwezo wa kila moja kufuga samaki zaidi ya 20.

 

Gloria anasema alikuwa kwenye kundi lililohusisha wafugaji wa samaki na kuku na anaongeza kuwa mradi umetoa nafasi ya kupata taarifa ni ‘nani anafanya nini’ na kuweza kupata uzoefu kwenye hizo sekta ambazo zina uzoefu wa kule mradi unakolenga.

 

"Kwa mfano, tumeweza kujifunza changamoto tunazozipata. Pia, mradi umeweza kujua kwamba ili kumsaidia kijana aweze kuingia katika miradi ambayo tunaifanya, ni hatua gani zifanyike, awezeshwe kwenye mambo yapi,” anafafanua.

 

Glora anaongeza: “Kwa hiyo, mradi umeweza kutambua wale vijana wana fursa gani, ni fursa ya kuajiriwa au ya kujiajiri na iwapo ataajiriwa, nini afanyiwe huyo kijana, awezeshwe vipi ili aweze kujiajiri, labda masuala ya ujuzi na masuala ya mtazamo na vitu kama hivyo.”

 

Anaunga mkono mradi kuchagua kundi la vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 24, kwani ni rahisi kuongozwa na kulelewa, hata baadaye wakasimama kwa uwezo wao.

 

"Tukimuacha akiwa zaidi tayari anaanza kuingiza mambo mengi, lakini tukimchukua, tunaanza kumtengeneza na kumuunda kijana ambaye mwisho wa siku anakuwa kijana anayeweza kujiajiri au anaweza kuajiri wengine au kijana mwenye ujuzi ambao ni endelevu," anasema.

 

Gloria anashauri vijana kubadilisha mtazamo, kwani vijana wengi wanapenda mambo ya haraka haraka, wanapenda mafanikio ya haraka.

 

"Sasa nashauri vyombo (vya habari) vionyeshe role models (mifano ya kuigwa) waliofanikiwa kwenye kilimo na ufugaji. Inaweza kuwa chachu ya mafanikio kwa vijana wengine.

 

“Hivyo, mradi utafute namna ya kutengeneza hao ‘role models’ sambamba na vyombo vya habari viandike na kutangaza juu ya kilimo, ili kuhamasisha vijana walio mitaani kujiunga na kilimo," mtaalam Gloria anaeleza.