Vijana ajira ‘nje nje’ mtayafanya hayo…

16Mar 2019
Moshi Lusonzo
Dar es Salaam
Nipashe
Vijana ajira ‘nje nje’ mtayafanya hayo…

KWA taifa ambalo kuna idadi kubwa ya vijana wasio na ajira kama Tanzania, vijana wanatakiwa kubadilika na kuja na mikakati mipya ya kutatua changamoto hiyo inayoongezeka kila mwaka.

Mazingira na wakati yanawalazimisha kubadilika na la muhimu ni kuwa wabunifu zaidi, wagunduzi na wenye mawazo na taratibu mpya za kujiajiri au kuajiriwa ili kuwa na maisha bora, kwa kuwa inaelezwa kuwa uvivu wa kufikiri, matumizi mabaya ya lugha na ukosefu wa ubunifu ni baadhi ya mambo yanayochangia kundi hili kupoteza sifa katika soko la ajira.

Hayo ni baadhi ya mambo yanayoibuliwa jijini Dar es Salaam katika kongamano la wanafunzi 200 kutoka mikoa mbalimbali walioibuka kidedea kwenye mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.

Kongamano hilo lenye madhumuni ya kuwandaa wanafunzi hao kuingia katika elimu ya juu na kubaini mbinu mbalimbali za kupata ajira liliandaliwa na Taasisi ya An Nahl Trust Fund ya Dar es Salaam.

Akizungumza na vijana hao Mkurugenzi wa Kampuni ya Sahara Ventures inayoshughulika na teknolojia ya masuala ya kielektroniki na kompyuta, Jumanne Mtambalike, anawaambia washiriki hao kuwa, ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa vijana 900,000 nchini wanaingia katika soko la ajira kila mwaka, lakini ni asilimia 10 pekee karibu watu 90, 000 ndiyo wanaopata nafasi za kazi.

Hata hivyo takwimu hizo ni za muda mrefu na idadi inaweza kuwa imeongezeka zaidi.

Anasema sababu kubwa zinazowakosesha vijana kazi kama ambavyo zinaelezwa na waajiri ni wengi kutokuwa wabunifu, uvivu wa kufikiri na matumizi mabaya ya lugha jambo linalosababisha wakwame kwenye kuandika barua za maombi ya ajira na usahili.

Mtambalike anasema misingi ya kijana kujiamini na kukubalika inaanzia katika elimu ya sekondari ambako huko anaandaliwa kuwa na ujasiri wa kupambana na maisha yake.

KUKOSA UBUNIFU

Akizungumzia ukosefu wa ubunifu, Mtambalike anasema wanafunzi wengi wanaamini mchepuo pekee wa masomo anayosoma ndivyo vitakavyomwezesha kupata kazi nzuri. Mawazo hayo yanasababisha kushindwa kutanua akili zao kwa kusoma mambo mbalimbali ambayo yangemsaidia kupata ujuzi na nafasi zaidi za kujiajiri au kuajiriwa.

“Vijana wengi wanakosa ubunifu licha ya kuishi katika mazingira ya teknolojia, badala yake wanadhani michepuo pekee ya masomo itawasaidia kupata ajira wanazotaka. Huo ni uongo ni lazima kutambua kwamba bila nguvu ya ziada nafasi za kazi ni ngumu,” anaeleza Mtambalike.

Anasema ni muhimu kwa wanafunzi kusoma na kutafuta elimu mbadala nje ya masomo ili kujiongezea nafasi pale anapomaliza masomo yake.

“Kwa mfano unaposoma masomo ya sayansi, kijana ana nafasi kubwa ya kuwa daktari, muuguzi au mfamasia, lakini unapoongeza masomo ya ziada nje ya fani yako inakupa uwezo wa kupata ajira zaidi,” anashauri.

UWEZO WA KUFIKIRI

Mtambalike anasema katika ripoti hiyo ya nafasi za kazi, waajiri wengi wanalalamika vijana wa Tanzania kuwa hawaendi na wakati pamoja na mahitaji yao kutokana na kushindwa kufikiri kwa kina nini wafanye na kwa wakati gani.

Anasema idadi kubwa ya vijana wanaomaliza masomo na kuajiriwa wanashindwa kwenda na majukumu ya mwajiri kwa kushindwa kuwajibika.

“Tatizo hili linatokana na vijana wanapotoka vyuoni hawajajiandaa vilivyo katika ajira, hawana uwajibikaji na uwezo wa kutosha wa kufanya kazi,” anaongeza.

Jambo jingine ambalo vijana wengi wanajikuta wakikwama kupata ajira ni kuathiriwa na uraibu wa mitandao ya kijamii.

Anasema matumizi ya mitandao ya kijamii yamekithiri kuanzia shuleni hadi vyuoni na kusababisha wengi kuathirika katika lugha na utendaji wa kazi.

“Ndani ya mitandao kuna matumizi ya lugha isiyo rasmi ya kukatisha maneno, vijana wengi wameathirika na lugha hiyo kiasi ambacho hata kwenye barua zao za maombi ya kazi wanaandika jambo ambalo linaongeza ufinyu wa kuchaguliwa,” anasema Mtambalike.
Anasema matumizi ya mitandao iwe ya kiasi na yasimfanye mtu kuwa tegemezi kifikra na kitabia.

Mkuu wa Idara ya Vijana wa An Nahl, Ali Mnondwa, anasema kongamano hilo linawafanya vijana hao kuwa pamoja na kujadili changamono na vikwazo wakati wanakabiliana na changamoto zinazowakabili.

Anasema pamoja na kufanya vyema katika mitihani ya kidato cha nne, wanatakiwa kupewa mwanga wapi wanaelekea na nini wafanye ili kutimiza ndoto zao za maisha.

“An Nahl tunafanya makongamano haya kwa lengo la kuwapa mbinu mbadala ya kutafuta fursa za maisha pale wanapomaliza masomo yao ya juu, ni lazima watambue kila hatua ina vikwazo katika kutimiza ndoto zao,” anasema Mnondwa.

Hata hivyo, Mnondwa anasema mwakani watapanua wigo kwa kuwakutanisha wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani yao kwa lengo kuwapa njia ya kutimiza malengo ya maisha yao ya baadaye.

Asha Mohamed, mwanafunzi aliyemaliza Shule ya Sekondari Jangwani ya Dar es Salaam, anasema mafundisho waliyopata kwenye kongamano hilo yatamsaidia katika masomo yake ya ngazi za juu.

“Naamini kutokana na mada zilizotolewa zimenipa mwangaza na njia bora ya kufuata ndoto zangu na niweze kufanikiwa vyema katika elimu yangu ya juu,” anasema Asha.

Kwa upande wa Hassan Hamid Ussi, kutoka Sekondari ya Lumumba, Zanzibar, anaishukuru An Nahl kwa kumsaidia kupata mwanga katika elimu yake na kuahidi kufuata njia bora ili afanikiwe katika elimu yake.

Habari Kubwa