Vijiji Kilwa vinayobadili maisha kupitia misitu

11Feb 2016
Mashaka Mgeta
Kilwa
Nipashe
Vijiji Kilwa vinayobadili maisha kupitia misitu

TAKRIBANI kilomita 100 kutoka eneo la Kilwa Masoko yaliko makao makuu ya wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kuna kijiji cha Nainokwe. Ni moja ya vijiji vinavyotekeleza mpango wa umiliki wa misitu ya vijiji.

Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nainokwe, Mohamed Kitone (kushoto) akiwa na Kaimu Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rajab Mpulu.

Kijiji hicho kilianza mchakato wa kumiliki misitu hiyo mwaka 2006 na ikathibitishwa mwaka 2008, huku uvunaji wa mazao yake ulianza mwaka 2010.

Kikiwa kinamiliki misitu ya Kijawa ‘A’ wenye ukubwa wa hekta 8,000 na Kijawa ‘B’ yenye hekta 1,629, kijiji cha Nainokwe kimefanikiwa kusimamia misitu na hivyo kupata mapato yanayotumika kwa ajili ya huduma za kijamii.

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji hicho, Seleman Kikulu, anasema kabla ya vijiji kumilikishwa misitu, wanavijiji hawakuona manufaa ya rasilimali hiyo na hata wakawa wavivu wa kushiriki katika katika ulinzi wake.

Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Nainokwe, Rajab Mpulu, anatoa mfano katika msimu wa mwaka 2011/2012, kwamba walipata Sh. milioni 13 zilizotokana na uvunaji magogo kwenye eneo maalum lililotengwa kwa ajili hiyo.

Mpulu anasema, miongoni mwa huduma zilizofanikishwa kutokana na mapato kutoka kwenye misitu hiyo, ni ujenzi wa nyumba ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji, uchimbaji kisima kirefu na kulipia bima za afya wazee 30 wasiokuwa na uwezo kijijini humo.

Nao wakazi wa kijiji hicho wanaowakilishwa na Ismail Mwaya, wanasena maeneo hayo ya huduma za kijamii yalikuwa duni kabla ya kijiji kumilikishwa ardhi.

Mbali na manufaa ya jumla kijijini Nainokwe, wakazi wa kijiji hicho wanaelezea kunufaika kutokana na kazi wanazozifanya na kulipwa na wafanyabiashara wa mazao ya misitu.

Mmoja wa wakazi wanaonufaika kutokana na wafanyabiashara hao ni, Mohamed Kitone, anayesema wanapata ujira kutokana na kukata magogo, miti, upasuaji mbao, kuchimba dawa za asili na masalia ya miti maarufu kama vilingu.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mkazi mwingine, Rajab Likamba, anayesema wanapokata mti wa mtondoro wanalipwa kati ya Sh 10,000 hadi 15,000 kwa mti wakati vilingu (masalia ya miti) inakatwa kwa kati ya Sh 4,000 hadi 8,000.

Wakati hali ikiwa hivyo kijijini hapo, Ofisa Ardhi, Maliasili na Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Raymond Ndumbaro, anasema mamlaka hiyo (Halmashauri) inapata asilimia tano ya mapato yanayotokana na mauzo ya mazao ya misitu ya vijiji.

Anasema halmashauri inapata mapato mengine mengi, ingawaje hakutoa takwimu husika za makusanyo hayo.

MALIPO NA ULINZI

Wakati misitu hiyo ikimilikiwa na halmashauri ya wilaya, kijiji hicho kilipata asilimia tano ya mapato yaliyotokana na mazao ya misitu, lakini sasa kinapata asilimia 100 inayogawanya katika makundi makuu manne.

Mpulu anataja mafungu hayo ni asilimia 50 inayobaki kwa serikali ya kijiji, asilimia 40 inapewa Kamati ya Maliasili, asilimia tano kwa Halmashauri ya Wilaya Kilwa na nyingine tano, kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Mpingo linalotoa ushauri kuhusu uendelezaji misitu.

Mjumbe wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji hicho, Rukia Ngwenje, anasema kamati yake hufanya doria kwenye misitu kwa ratiba maalum na kushtukiza.

Pia anasema Kamanda wa Maliasili katika kamati hiyo anaongoza doria na kuwajibika kwa ulinzi wa kila siku msituni.

Hata hivyo, Ngwenje anakiri kamati yake kukabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwamo ukosefu wa mafunzo ya ulinzi na vitendea kazi kama vyombo vya usafiri na silaha za kukabiliana na majangili wa misitu.

Nainokwe ilikuwa na bunduki yenye kutumia risasi za moto, lakini ikataifishwa wakati wa `operesheni tokomeza majangili’ iliyofanyika 2013.

Hivi sasa, wajumbe wa kamati ya maliasili ya kijiji hicho wanatumia silaha za jadi kama panga, shoka, fimbo na rungu kudhibiti uvunaji haramu wa mazao ya misitu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili ya kijiji Nasima Kassim, anasema pamoja na changamoto hizo, ratiba za doria zimebaki kuwa mara mbili kwa mwezi na inapotokea dharura baada ya kupata taarifa za kuwapo waharibifu wa misitu.

MAFUNZO
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa, Ofisa Ufugaji Nyuki wa wilaya hiyo, Abushiri Mbwana, anasema wameshatoa mafunzo ya namna bora ya utendaji kazi kwa kamati hizo.

Anataja namna hizo bora ni kuweka miaka mitatu kuwa ukomo wa wajumbe wake kabla ya kufanyika uchaguzi mwingine.

Kuhusu ulinzi na mafunzo, Mbwana anasema ununuzi wa vifaa unapaswa kufanywa kupitia fedha zinazoelekezwa kwenye kamati na kwamba wanapozidiwa katika ulinzi wa misitu, ndio wanapopaswa kuomba msaada wa halmashauri.

UFUGAJI NYUKI NA UWINDAJI

Kassim Nasima, anadokeza kuwepo mpango wa kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki, ambao katika hatua ya kwanza ilianzishwa kwa mizinga 19 ya nyuki na matarajio ni kuwawezesha wasimamie msitu na kudhibiti majangili wa misitu.

Utalii wa uwindaji kwenye maeneo ya wazi yanayoungana na hifadhi za misitu ya vijiji, unachangia uharibifu uliopo sasa. Hali hiyo inatokea, wakati wawindaji wanapowafukuza wanyamapori na kuingia nao hadi ndani ya mazingira ya misitu ya vijiji.

Pendekezop lake ni kwamba, kufanyike mabadiliko yatakayowalazimisha wawindaji wanapopata vibali kutoka ama halmashauri au Wizara ya Maliasili na Utalii, kwenda kwenye vijiji vyenye misitu, ili kupata kibali na ushirikishwaji wa kamati husika.

Ofisa Ardhi, Maliasili na Mazingira wa Wilaya ya Kilwa, Raymond Ndumbaro, anasema tangu waanze kumiliki misitu, vijiji vimepata mafanikio tofauti na ilivyo kwa isiyohifadhiwa.

Kuhusu athari za uwindaji kwa misitu, Ndumbaro anasema hali hiyo itadhibitiwa ikiwa sheria, kanuni na taratibu zinazowaongoza wawindaji zitafuatwa.

Anataja faida za kutoingilia hifadhi za misitu ya vijiji na kuongozana na mabwana nyama.

Wilaya ya Kilwa ina vijiji 26 vilivyohamasishwa katika mpango wa umiliki wa misitu, sita kati ya hivyo vimekamilisha mchakato huo.

Hatua za mchakato huo ni uelimishaji jamii, kutenga eneo la msitu, kuhesabu aina na idadi ya miti iliyopo na kuainisha mipaka yam situ husika.

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa usimamizi wa misitu wanaofadhiliwa na serikali ya Finland, wakasaidia kufanikisha azma hiyo kupitia mradi wa kampeni ya Mama Misitu.

Kampeni hiyo inabeba dhamira na maono ya kuhifadhi, kulinda na kuhamasisha matumizi endelevu ya misitu, ikiwa inaratibiwa na Jumuiko la Maliasili Tanzania (TNRF).

WADAU

Anasema kuwa ufanisi katika utekelezaji umiliki misitu wa vijiji, umevutia baadhi ya mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuitembelea wilaya hiyo kwa ajili ya kujifunza.

Kwa mujibu wa Ndumbaro, mataifa ambayo raia wake wamefika wilayani humo na kutembelea vijiji kadhaa kwa ajili ya kujifunza ni pamoja na Zambia, Botswana na Namibia.

Naye Ofisa Misitu wa Wilaya ya Kilwa, Mustapha Mfangavo, anasema pamoja na umiliki wa hifadhi za misitu, baadhi ya vijiji vinatekeleza mpango shiriki wa pamoja wa hifadhi za wazi na zile zinazomilikiwa na halmashauri na serikali kuu.

Anasema misitu ya serikali kuu na ile ya wazi ipo mbali kutoka mahali walipo watumishi wa Wakala wa Misitu (TFS), hivyo mpango huo unalenga kuwashirikisha wananchi katika ulinzi.

Hata hivyo anasema hivi sasa makubaliano ya namna jamii za vijijini zitakavyonufaika na rasilimali hiyo yapo katika hatua za mwisho.

Mfangavo anasema kuwa, haikuwa rahisi wakazi wa vijiji kuukubali mpango shirikishi wa usimamizi wa misitu kutokana na hisia zilizojengeka awali kwamba lengo lilikuwa ni kuporwa rasilimali hiyo.

“Tulitumia muda mrefu kuwafafanulia na kuwaelimisha, tukiwaonyesha sheria, sera na miongozi kadhaa, lakini baada ya kubaini mafanikio sasa maombi ya umiliki wa vijiji yamekuwa mengi sana,” anasema.

WAFANYABIASHARA WALONGA

Mfanyabiashara wa mkaa, Zuberi Kassim, anasema kuwa ipo haja ya serikali kupunguza tozo zinazoelekezwa kwa mazao ya misitu, ili gharama za upatikanaji wake ziwe ndogo, jambo litakalosaidia kudhibiti wa uharibifu wa misitu.

“Unapoweka tozo nyingi, unasababisha mazao ya misitu kuwa na thamani kubwa, hivyo kuchochea uharibifu na ujangili dhidi ya rasilimali hizo,” anasema.

Mfanyabiashara huyo anasema, kupunguza gharama kunapaswa kuelekezwa katika maeneo yanayotegemea mazao ya misitu, kama nishati inayotokana na mkaa.

Anasema mkaa unatumiwa na sehemu kubwa ya jamii isiyokuwa na uwezo wa kumudu gharama za nishati nyingine kama gesi, hivyo suala hilo likishughulikiwa, mahitaji ya mkaa yatapungua au kutoweka kabisa.

Anatoa mfano kuwa, gunia la mkaa lenye ujazo wa kilo 75 hivi sasa linanunuliwa kwa Sh. 13,000 wakati ushuru wake ni Sh. 16,600.

“Unapokuwa na gharama hizo na kujumuisha za usafiri, malazi, chakula, kupakia na kupakua, utaona kwamba anayeumia sana ni mtumiaji,” anasema.

Hivyo, ni dhahiri kwamba umiliki wa misitu ya vijiji ni hatua muhimu ya kuwapo mipango ya hifadhi na uvunaji endelevu wa rasilimali hiyo na mazao yake.