Vikope, mtoto wa jicho tishio Pwani

25Nov 2018
Yasmine Protace
Kibaha
Nipashe Jumapili
Vikope, mtoto wa jicho tishio Pwani

TATIZO la vikope au trakoma, mtoto wa jicho , uoni hafifu , ukosefu wa miwani na wakati mwingine kukosekana watalaamu wa kuwahudumia wagonjwa kumewasukuma mabingwa wa macho kutoka Korea ya Kusini kusaidia huduma za macho kwa wakazi wa mkoa wa Pwani.

Dokta Jihong Bae kutoka Vision Care Korea Kusini akitibu wagonjwa wa macho, pamoja naye ni Dk. Eligreater Mnzava, (kushoto), akifuatilia vipimo vya mgonjwa.

Wataalamu hawa wanaendesha huduma kwa kushirikiana na Hospitali ya Tumbi mkoani Pwani,iliyojengwa na Shirika la Elimu Kibaha mwaka 1967, wakati huo ikianza kama kituo cha afya na leo ni hospitali ya rufani ya mkoa wa Pwani.

Pamoja na kupanda chati huko Tumbi inakabiliwa na changamoto katika kitengo cha huduma ya macho na kwa ujumla haina wodi ya macho, wataalamu wala vifaa jambo linaloirudisha nyuma katika kuwahudumia wagonjwa wa mlango huo muhimu wa fahamu.

Kwa mujibu wa daktari bingwa wa macho mkoa wa Pwani, Eligreti Mnzava, kutokana na upungufu huo wenye matatizo ya macho wanaofanyiwa upasuaji hulazwa katika wodi ya wagonjwa wa mifupa.

Akizungumza na Nipashe muda mfupi baada ya kuzinduliwa huduma za kuwapatia wananchi wa mkoa huo uchunguzi, tiba na miwani zilizofadhiliwa na Shirika la kimataifa la Vision Care la Korea Kusini anasema:

" Hatuna wodi ya macho katika hospitali hii. Huduma tunazitoa,lakini ikifikia wakati mgonjwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji na kulazwa inabidi alale katika wodi ya wagonjwa wa mifupa," anasema.

UHABA WA MADAKTARI

Anaongeza kuwa changamoto nyingine katika, hospitali hiyo ni uhaba wa madaktari wa macho akieleza kuwa wanaohitajika ni zaidi ya wawili lakini kwa sasa yupo mmoja pekee.

Anasema : “Hapa Tumbi ndiyo hospitali pekee katika mkoa wa Pwani ambao una wilaya saba. Tena ni mkoa unaotatizwa na ajali za mara kwa mara , lakini ndiye pekee inayotoa huduma za macho lakini pia haina madaktari.”.

Mnzava anaeleza kuwa kutokuwapo wataalamu wa macho katika baadhi ya wilaya za mkoa huo, kumesababisha Tumbi kuhudumia wagonjwa wengi wa macho lakini pia ikiwa inakabiliwa na ukoefu wa waganga hao.

Anaigeukia serikali akiiomba iwawezeshe itoe wataalamu wa kutosha wa kuhudumia wagonjwa wa macho katika wilaya za mkoa huo wa Pwani sizizo na wataalamu ili watumie hospitali nyingine badaya kutegemea Tumbi pekee wanapofuata kutibiwa macho na kupewa miwani.

" Katika mkoa mzima wa Pwani daktari wa macho ni mimi peke yangu. Pamoja na kwamba kuna wahudumu ambao tunasaidiana, ninapokosa kufika kazini wanaweza kufanya huduma ndogo za macho lakini zile kubwa wanaziacha hadi nitakaporudi," anasema Dk.Mnzava.

Anaongeza kuwa licha ya kwamba kuna vyuo viwili vinavyotoa mafunzo ya tiba na huduma ya macho wanaohitimu hawazidi watano lakini changamoto inayoibuka ni baadhi ya madaktari hawapendi kufanyakazi mkoani.

Kukataa vituo vya kazi vya mikoani kunasababisha wengi kurundikana mijini na hasa kukimbilia jijini Dar es Salaam, ili waweze kufanya kazi za ziada katika hospitali nyingine.

SHIDA YA MACHO

Kwa mujibu wa Mnzava tatizo la mtoto wa jicho mkoani Pwani ni kubwa na tangu matibabu yalipoanza kutolewa bure kwa msaada wa Korea Kusini katika hospitali hiyo kwa muda wa wiki moja wagonjwa wapatao 410 waligunduliwa na matatizo hayo na wengine 48 walifanyiwa upasuaji wa mtoto jicho, huku wengine wakigundulika kuwa na uono hafifu.

Kwa upande wake Hyowon Lee Meneja Msaidizi wa Vision Care kutoka Korea Kusini anasema wameamua kutoa msaada wa kutoa matibabu ya macho kwa Watanzania ili kuwawezesha wananchi wagonjwa lakini pengine hawawezi kupata huduma za macho wahudumiwe bure.

Anasema kila baada ya miezi sita asasi hiyo huja nchini kutoa matibabu ya macho.

Anasema kwa Tanzania wagonjwa ambao wamewapima macho wamewagundua kuwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho pamoja na trakoma au vikope.

Trakoma au vikope ni ugonjwa wa macho unaosambazwa na inzi wa nyumbani wanaosafirisha vimelea vya ‘Clamydia Trachomatis’ kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa watu wazima .Vikope ni hali ya kope kuota kuelekea ndani ya jicho na kuanza kukwaruza kioo cha jicho (cornea).

Ugonjwa huu husabisha jeraha kwenye kioo cha jicho na likipona huacha kovu ambalo huzuia mwanga wa kutosha kuingia ndani ya jicho na hivyo kusababisha uoni hafifu au hata upofu.

Ugonjwa huu unapatikana ukanda wa joto lakini huambatana na uchafu wa mwili na mazingira japo watu wengi hupata upofu lakini wataalamu wanaamini kuwa unaweza kuepukika na kwamba dalili zake ni macho mekundu, yanayotoa machozi muda wote, kuuma na kuwasha sana Lee anaongeza kuwa, kutokana na kuwapo matatizo ya macho kwa idadi kubwa ya watu,wanatarajia kujenga kambi ili kuwawezesha na kusaidia huduma za macho kuwa endelevu.

"Matatizo ya macho hapa Tanzania ni makubwa hasa upande wa trakoma na mtoto wa jicho, tunatarajia kujenga kambi ili kuhakikisha huduma hizo ziendelee kutolewa wakati wote kusaidia wananchi," anasema Lee.

Anaongeza kuwa mpaka ifikapo Mei mwakani,wanatarajia kuwapo na kambi 275 ambazo zitatoa huduma ya macho katika nchi mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na Afrika.

Anasema tangu waanze kutoa huduma za macho bure katika nchi mbalimbali duniani zikiwamo za Afrika watu milioni 1,9 wamenufaika na tiba hizo, huku wagonjwa wa macho wengine 223,167 wakifanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho na wagonjwa wengine wa macho 41,846 wakifanyiwa uchunguzi na kupatiwa miwani kutokana na kuwa na uono hafifu.

Dokta Lee anasema kutokana na serikali ya Korea Kusini kuwa na mahusiano mazuri na Tanzania,wamewafundisha baadhi ya madaktari kutoa huduma za macho lakini pia na kuwapatia vitendea kazi kama mashine na vifaa vya upasuaji vilivyotolewa kwa hospitali ya rufani ya Tumbi.

Akizungumzia zaidi kuhusu matibabu hayo anasema walianzisha huduma hiyo mwaka 2016 na kwamba wataendelea kuunga mkono kusaidia huduma za afya hasa kuhudumia wagonjwa wa macho..

Lee anaeleza kuwa kutokana na udogo huo wa madaktari wa macho kuna haja ya kuwaongeza ili kuwasaidia watu kupata matibabu kwa wakati na kwa ufanisi.