Ving'ora na vimulimuli binafsi, marufuku barabarani

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ving'ora na vimulimuli binafsi, marufuku barabarani

KATIKA siku za hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya madereva wa vyombo vya moto yaani, magari, bajaji na pikipiki kufunga taa za vimulimuli au za rangi rangi, taa zenye mwanga mkali (spot light) na kufunga ving’ora-

-kwenye magari ya kiraia au watu binafsi na pikipiki zote za kiraia jambo ambalo ni kinyume na sheria ya kanuni za usalama barabarani.

Tabia hiyo ilimkera Kamanda wa Polisi Kanda Maalum  Dar es salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa  ambapo Agosti 5, 2019 alitoa katazo  la kupiga marufuku  magari, bajaji na pikipiki binafsi katika Mkoa wa Dar es salaam kutumia  ving’ora, taa za rangirangi na vimulimuli.

Kutokana na kujitokeza  kwa baadhi ya watu walioamua kufunga vimulimuli na ving’ora  na kuvitumia wawapo barabarani, hivyo kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara hapa nchini, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime naye alitoa ufafanuzi.

Alitoa ufafanuzi  kwa kuweka msisitizo kuwa Jeshi la Polisi nchini linaelekeza katazo hilo si kwa Mkoa wa Dar es salama tu,  bali ni kwa nchi nzima.

Madereva hupenda kufunga vifaa hivyo ili waweze kupewa kipaumbele wawapo barabarani kwa kujua au kwa kutofahamu kuwa ni kinyume  na sheria, kanuni na taratibu zilizopo jambo ambalo si sahihi.

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani sura ya 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kifungu cha 39 B (I) na (2) kinafafanua juu ya matumizi ya ishara ikiwepo ving’ora na vimulimuli.

Sheria hiyo imeeleza pale dereva atakapoona kuna ulazima wa kutoa tahadhari au kuzuia hatari dhidi ya watumiaji wengine wa barabara sheria hiyo imeendelea kueleza  dereva hatatumia  ishara hizo kwa nia yeyote zaidi na ilivyoelezwa katika kifungu hicho kidogo cha kwanza na wala  haruhusiwi kutumia ishara hizo kwa muda mrefu zaidi ya mazingira yaliyopo  yanayomlazimu kutoa tahadhari.

Aidha,  Kwa mujibu wa sheria hiyo ya Usalama barabarani kifungu 54 (1), (2),(3),(4) na (5)  vinaeleza mazingira, matumizi ya vimulimuli, ving’ora na wanaoruhusiwa  kufunga ving’ora, vimulimuli na kuvitumia kutoa  ishara za tahadhari na  watumiaji wengine kupaswa kuwapisha au kuwapa kipaumbele.

”Wanaoruhusiwa kutumia ving’ora na vimulimuli  kwa mujibu sheria hiyo ni magari ya dharura ambayo ni ya Polisi,  Majeshi ya Ulinzi, Zimamoto na Uokoaji, Magari ya kubeba Wagonjwa  au magari mengine na matela ambayo  yamepata kibali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali” alisema SACP Misime.

Magari mengine ni yale yanayotumiwa na Viongozi Wakuu wa Kitaifa  na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Hivyo  kama haupo katika makundi hayo ni kinyume cha sheria kufunga ving’ora, taa za rangirangi na vimulimuli na kuvitumia uwapo barabarani.

Kutokana na mazoea ambayo yameanza kujitokeza kwa baadhi ya watu wenye vyombo vya moto kufunga vifaa hivyo  vya kutoa ishara  na kuvitumia wawapo barabarani watambue waliopewa fursa hiyo ni magari ya misafara ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wakuu wa Vyombo vya Dola, magari ya dharura kama nilivyotaja hapo juu  na yaliyopewa kibali na Waziri  mwenye dhamana na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali na si vinginevyo,

Taarifa ya Jeshi la Polisi kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,  imesisitiza kuwa  wataendelea kuchukua hatua dhidi yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.  Pia  limetoa onyo kwa madereva wenye tabia hiyo waiache mara moja lasivyo watakamatwa.

Imetolewa na:

Ofisi ya Uhusiano

Makao Makuu  ya  Polisi.

S.L.P. 9141,

DAR ES SALAAM.

Habari Kubwa