Viongozi Mara muonekane sasa mkitekeleza maagizo

23Sep 2018
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Viongozi Mara muonekane sasa mkitekeleza maagizo

KATIKA ziara ya Rais John Magufuli, kwenye mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu na Singida, alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Wilaya ya Tarime ndiko rais alikokutana na migogoro mingi ya ardhi.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya lami ya kilometa 50, kutoka Makutano hadi Nata mkoani Mara na ujenzi wa daraja la mto Sibiti wilayani Mkalama mkoa wa Singida, ambao unaunganisha mkoa huo na Simiyu.

Akiwa Mara alikumbana na migogoro ya ardhi isiyoisha na kuwaagiza wakuu wa wilaya wa  mkoa humo na viongozi wengine wakiwamo wa sekta ya ardhi kuimaliza haraka iwezekanavyo.

Rais Magufuli alisema endapo watashindwa kufanya hivyo hawatakuwa na sababu ya kuwa madarakani wakati wananchi wakiendelea kugombania mipaka ya ardhi ndani ya nchi yao.

Aidha, aliwataka wananchi wasigombane pia viongozi wa maeneo hayo wasisubiri viongozi wa kitaifa waende wawatatulie migogoro hiyo na kuwataka wasiuaibishe mkoa wa Mara.

Baba wa Taifa amelala hapo, na wasiliingize taifa katika migororo.

Anawashangaa viongozi wa mkoa wa Mara kuacha wananchi wagombanie ardhi wakati kuna maeneo makubwa, hali inayoonyesha huenda kuna uzembe unaosababisha hayo yote yanayoendelea kujiri.

“Msigombane, lakini pia msisubiri viongozi wa kitaifa waje wawatatulie migogoro yenu. Ninawaomba sana msiniaibishe, huu ni mkoa ambao Baba wa Taifa amelala. Pia tusiingize nchi katika migororo.

“ Na viongozi wa mkoa wa Mara kwanini mnaacha wananchi wagombanie ardhi wakati kuna maeneo makubwa au mnataka mpeleke wawekezaji? Anahoji Rais.

Kwa kauli hiyo kama viongozi walikuwa wamezembea kuzitatua changamoto waamke waanze kufanya kazi ili kuhakikisha kwamba hali hiyo haijirudii na malalamiko yanaondoka.

Jambo la kuzingatia ni kwamba ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya jamii katika kujiletea maendeleo kwa kuitumia kuendeshea shughuli zote muhimu za maisha kama kilimo,  ujenzi wa makazi, viwanda, shule, hospitali na shule pamoja na kufuga.

Hivyo ni wazi kwamba inapotokea migogoro ya ardhi, hayo yote hayawezi kufanyika na badala yake ni misuguano ambayo mwisho wake huleta madhara kama ambavyo imekuwa ikitokea kati ya wakulima na wafugaji.

Ikumbukwe hata Rais alishangaa kuona viongozi mkoani Mara wakiacha migogoro ya ardhi ikiendelea.

Japo mkoa huo una maeneo makubwa ambayo wananchi wangepelekwa ili kufanya shughuli zao, akahisi huenda wana mpango wa kuweka wawekezaji.

Umuhimu wa ardhi ni mkubwa na ndiyo maana baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji na vijiji wamekuwa wakituhumiwa kujinufaisha kwa kugawa ardhi bila kuzingatia sheria, sera na kanuni zilizopo za ugawaji wa rasilimali hiyo, hali ambayo husababisha migogoro.

Binafsi ninaamini kwamba kwa maagizo ya Rais kuwataka viongozi kuhakikisha wanakutana ili kumaliza tatizo hilo, ni wazi sasa migogoro ya ardhi mkoani Mara itakuwa historia.

Nakumbuka changamoto za ardhi ndizo zilisababisha serikali kutengeneza sera na mfumo wa kisheria mwaka 1990, ambayo ilisababisha uundaji wa Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 na kutungwa kwa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, ambayo ni Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi namba nne ya mwaka 1999.

Hivi karibuni wakazi wa baadhi ya viijiji vya mkoa wa Pwani walieleza kuwa baadhi ya viongozi wa vijiji wameuza ardhi ya umma kwa wawekezaji na kuwakosesha maeneo ya kujenga shule, zahanati wala sehemu za wazi .

Wanavijiji hao wa Vikindu wilayani Mkuranga wanalalamika kuwa, kukosekana shule na zahanati kunawafanya kuzitafuta huduma hizo mkoani Dar es Salaam.

Japo tatizo la ardhi Mara pengine halijafikia kiwango cha kusababisha watu kufuata elimu na hospitali nchi au vijiji jirani ni jukumu la viongozi na wanasiasa pamoja na wananchi kutumia sheria za Ardhi na za Vijiji ili wasifike huko kwenye migogoro.

Sheria zimewaelekeza mipango na majukumu ya kutekeleza wanaponunua, kuuza ama kuwekeza kwenye ardhi za vijiji.

Kwa vile sheria zote zipo na zimekuwa zikiwaelekeza cha kufanya wazitumie kwenye mipango na matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji.

Lakini licha ya kuwapo kwa sheria hizo bado changamoto ya migogoro ya ardhi imeendelea kujitokeza. Ni wazi viongozi wanahitaji kufunzwa kuhusu sheria, sera na taratibu za ardhi hizo.

Wakati umefika serikali iangalie uwezekano wa kuwa na wanasheria wa vijiji wanaosimamia masuala yote ya kisheria kuepusha migogoro hasa ya ardhi.

Katika kutatua migogoro hiyo ni vyema pia kukuza uelewa wa wananchi kuhusu mifumo ya kisheria ya masuala ya haki za ardhi, uwezo wa uwekezaji mkubwa wa kilimo, uhusiano na ustawi wa wakulima wadogo, kilimo endelevu na maendeleo endelevu.

Kwa muda mrefu kumekuwapo na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wakulima na wawekezaji, mtu kwa mtu na kijiji kwa kijiji hali, ambayo wakati mwingine imekuwa ikisababisha watu kupoteza maisha, kupata ulemavu na upotevu wa mali zao.

Hivyo viongozi wa mkoa wa Mara ni vyema wakahakikisha wanatekeleza maagizo waliopewa na rais kwa ajili ya kutatua migogoro katika maeneo yao kabla haijaleta madhara kwa wahusika.

Ninaamini kwamba mkoa wa Mara bila migogoro ya ardhi inawezekana iwapo viongozi watajipanga na kukutanisha wale wanaogombania ardhi bila kuwapo ujanjaujanja aliousema rais.

Kuna madai kuwa kuibuka kwa migogoro ya ardhi mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini kumekuwa kukichangiwa na baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wanaotumia migogoro ili kujinufaisha wakitaka kuingia madarakani kwa lengo la kujinufaisha.

Viongozi wa aina hiyo wabanwe ili kuepusha wananchi kuumizana kwa sababu ya kugombania ardhi, vilevile kama kuna maeneo mengine yanayofaa kwa shughuli zao, basi wapelekwe huko.

Habari Kubwa