Viongozi serikali za mitaa barabara mnaziona lakini?

14Feb 2016
Nipashe Jumapili
Viongozi serikali za mitaa barabara mnaziona lakini?

Mitaa mingi ukipita hivi sasa utakuta njia/barabara zake zimeharibika kwa kuchimbika kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha nchi nzima.

Njia/barabara hizo zimegeuka kuwa mashimo kama sio mahandaki kiasi cha kusababisha magari kupita kwa shida au kushindwa kabisa kupita. Zingine zinapita sehemu muhimu kama hospitali, ambapo wagonjwa hutakiwa kuwahishwa kwa matibabu.

Wananchi wamekuwa wakitegemea barabara hizo kwa shughuli zao za kila siku, kwa mfano kuna wale wenye usafiri wao binafsi kwa ajili ya kwenda kazini, kufanya biashara au kupeleka watoto shuleni, lakini kutokana na ubovu wa barabara hizo, wanashindwa kupita kwa hofu ya kuharibu vyombo vyao vya usafiri.

Kuna mambo mengine ya dharura yanayoweza kutokea, lakini kwa sababu ya ubovu wa barabara yakashindwa kutatuliwa kutokana na miundombinu kuwa mibovu.

Kwa mfano linapotokea janga la moto kwenye mtaa ambao barabara zake zimegeuka kuwa mashimo, nyumba inaweza kuteketea kwa kuwa gari la zimamoto litashindwa kufika eneo la tukio.

Mbali na moto, hata mtu anapokuwa mgonjwa na kutaka kuwahishwa hospitali, anaweza kupoteza maisha akiwa njiani kutokana na ubovu huo.

Viongozi wetu wa serikali za mitaa ambao moja ya jukumu lao ni kuangalia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wao, wanaonekana kutofuatilia kero hiyo ambayo kama ingetatuliwa mapema, gharama ya kufanya ukarabati isingekuwa kubwa.

Kuna maeneo mengine, machimbo ya vifusi yako karibu na mitaa na malori yanayosomba vifusi hivyo yanapita kwenye barabara hizo mbovu na kuzidi kuziharibu.

Pamoja na wananchi kulalamikia malori hayo kupita kwenye barabara hizo, viongozi wa serikali za mitaa hawaonekani kusikia kilio hicho cha wananchi huku malori yakiendelea kuharibu barabara hizo.

Kama viongozi hao wangeweka utaratibu wa kuamuru kila lori linalopita kwenye njia hizo kumwaga kifusi kwenye sehemu korofi, ingesaidia kupunguza kero na kurahisisha magari madogo kupita kwa usalama.

Hata zingefanyika jitihada za kupitisha greda ili kusawazisha barabara ziweze kupitika vizuri, ingesaidia kupunguza kero hiyo.

Wakati wa kiangazi magari yanaweza kupita kwenye njia hizo kwa sababu madereva wanaweza kukwepa mashimo, lakini mvua zinaponyesha na mashimo hayo kujaa maji, inakuwa hatari kwa sababu kama mtu ni mgeni na njia anaweza kuparamia shimo na kuliacha gari hapo hapo.

Wananchi wangeshirikishwa katika kazi hii ya kutatua kero za barabara za mitaa yao wangeshiriki kikamilifu kama ilivyokuwa kwenye suala la usafi wa mazingira.

Hakuna mtu anayependa kuishi katika mazingira mabovu yasiyokuwa na miundombinu ya kueleweka, hivyo juhudi za kuboresha maeneo yetu tunayoishi na tunayopita ni ya kwetu sote.

Kuna wale wanaodhani kazi ya kutengeneza barabara inamhusu mbunge wa eneo husika pekee, jukumu hili ni la kila kiongozi na kila mmoja wetu ili mitaa yetu na maeneo yaweze kuwa na maendeleo.

Pamoja na kwamba maeneo mengi tunayoishi hayajajengwa kwa mpangilio na hivyo kusababisha miundombinu ya barabara kuwa migumu kuiboresha, lakini katika maeneo hayo hayo, kuna barabara ambazo zinasaidia kumfikisha mtu mwenye dharura kwa urahisi, ambazo zikiboreshwa malalamiko toka kwa wananchi yanaweza kupungua.

Kutokana na barabara za mitaani kuwa mbovu, baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zipo karibu na njia hizo, wameamua kuziba kwa magogo au matairi ya gari eneo la barabara ili kuzuia magari yasipite karibu na nyumba na hivyo kusababisha barabara kuwa finyu na kupitika kwa shida.

Wakati mwingine magari yanayopita kwenye njia hizo hayastahili kabisa kutokana na ukubwa wake. Kuna yale malori yanayobeba mawe makubwa na kusababisha uzito kuwa mkubwa na barabara kuendelea kuchimbika zaidi.

Kama kungewekwa sheria ndogo ndogo zinazokataza magari yenye kubeba uzito mkubwa kupita kwenye barabara zinazopita kwenye makazi ya watu, zingesaidia kunusuru barabara hizo zisiendelee kuharibiwa.

Ingawa kuna wakati wananchi huomba kibali cha kukataza magari hayo yasipite kwenye mitaa yao, lakini madereva hupuuza amri hiyo na wakati mwingine hunyofoa mabango ya makatazo hayo kwa kuwa wanajua hakuna atakayewachukulia hatua.

Ndiyo maana wakati mwingine wananchi huamua kujichukulia sheria mkononi kwa sababu ya kuona hata wanapofuata utaratibu wa kusikilizwa kero yao, hakuna linalofanyika na tatizo linaendeleo kubwa.

Ni matarajio yangu kuwa viongozi wetu tuliowachagua ili mtuletee maendeleo kwenye mitaa yetu na kutatua kero zetu mtasikia kilio ili hata mtakapokuja tena kuomba kura zetu, tuwarudishe tena madarakani kwa utendajikazi wenu mzuri.
[email protected], simu 0774 466571

Habari Kubwa