Vita mpya ya mabeki wa kati Taifa Stars

20Mar 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Vita mpya ya mabeki wa kati Taifa Stars

WAKATI Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga akitangaza kikosi cha timu ya Taifa, ametaja mabeki wa kati wanne.

nyoni erasto.

Mabeki hao ni Erasto Nyoni wa Azam FC, Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar, Abdi Banda wa Simba na Andrew Vicent Dante wa Yanga.

Kitu ambacho mashabiki wa soka wamebaki wanajiuliza ni nani atacheza na nani hatacheza kwenye kikosi hicho. Kati ya hao wanne, wawili wanatakiwa waunde ukuta wa timu ya taifa.

Wengine wawili itabidi wasubiri, ama wenzao wapate kadi, majeruhi na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Je, kati ya wachezaji wao wanne ni wachezaji gani wawili watamshawishi kocha Mayanga kuunda pacha?

1. Salim Mbonde-Mtibwa
Ni beki ambaye amekuwa akiingia na kutoka kwenye kikosi cha Taifa Stars. Amekuwa akicheza vizuri zaidi akiwa na timu yake ya Mtibwa, lakini mara zote anapokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, amekuwa beki wa kawaida.

Pamoja na hayo kwa sasa ameonekana kukomaa na kuwa mzoefu. Ana uwezo mkubwa wa kuokoa mipira kwa vichwa, lakini hana 'kontroo' sana miguuni, hivyo mara nyingi wachezaji kama hawa huchezeshwa namba nne, kama kuna beki mwingine mtulivu na mwenye uwezo wa kumiliki mpira.

2. Erasto Nyoni-Azam
Huyu ndiye anaonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kucheza kuliko wenzake. Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa kati ya wote hao waliochaguliwa, yeye ndiye ana sifa halisi za kuwa namba tano.

Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kutokuwa na papara. Ana uwezo wa kuziba na kusaidia makosa ya wenzake. Kutuliza presha ya wapinzani na hata mabeki wenzake.

Pia ni mzoefu zaidi kwenye kikosi cha timu ya taifa kuliko mwingine yoyote yule.

3. Abdi Banda-Simba
Ni mchezaji aliyekuwa kwenye kiwango cha juu kwa sasa, tangu kuanza kwa mzunguko wa pili akiwa na klabu yake ya Simba.

Urefu wake, uwezo wa kukabiliana na mastraika wababe, vurumai zake, kutotaka masihara ya kupiga chenga au kuchezacheza na mpira eneo la hatari, limemfanya kuwa kipenzi cha wanachama na mashabiki wa Simba kwa sasa.

Pia ana uwezo mkubwa wa kuruka juu na kuokoa mipira ya juu, huku akiwa na uwezo wa kumiliki mpira ni moja ya faida alizokuwa nazo kucheza namba nne.

4. Andrew Vicent 'Dante'-Yanga
Ni beki mbishi anayejituma. Kwa sasa anahesabiwa kuwa ni mmoja wa mabeki bora waliopo nchini.

Moja ya sifa yake kubwa ni kuruka vichwa na kuokoa mpira ya juu, akiwashinda hata mastraika warefu.

Uchezaji wake unaonyesha kuwa ni mzuri kucheza namba nne, huku nyuma yake akitakiwa kuwa na beki atakayekuwa akimsaidia, kosa lolote atakalofanya.

Kitu pekee kinachoweza kumkwamisha ni ufupi, hasa ikizingatiwa wenzake ni warefu, kwani kwenye mechi za kimataifa kuna mastraika warefu na wenye uwezo mkubwa wa kuutumia.

Pamoja na hayo yote jukumu la kupanga nani acheze na nani analo kocha Mayanga.

Habari Kubwa