Viti maalum sasa vyaanza kuwachosha wanawake

15Mar 2017
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Viti maalum sasa vyaanza kuwachosha wanawake

WAKATI Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ikiendelea kuwatambua wanawake kama makundi maalum ya kupewa nafasi za viti maalum katika nafasi za ubunge na udiwani, baadhi wanaliona suala hilo kama upendeleo usio na tija ambao hauwezi kuvusha kundi hilo ambalo linataka kujikomboa.

Kama inavyokumbukwa mwaka 2009, Serikali iliongeza idadi ya Viti Maalum vya Wabunge Wanawake kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40.

Kuthibitisha kuwa, wanawake wameanza kujikomboa kwa kushika nafasi kubwa katika jamii hususani za uongozi, idadi ya wanawake wanaoshikilia majimbo ya uchaguzi inaongezeka kila mwaka wa uchaguzi.

Kadhalika idadi ya wanawake waliopata viti maalum katika uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka 2015, ilikuwa ni 64 kupitia Chama Cha Mapimduzi (CCM), wanawake 36 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanawake 10 kupitia Chama cha Wananchi (CUF).

Licha ya juhudi za serikali za kuwainua wanawake kupitia nafasi hizi za ubunge na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na wanawake wenyewe, bado suala la wanawake kupewa nafasi hizo za viti maalum inaonekana kama ni upendeleo au kuwadhoofisha.

“Yani kitendo cha serikali kuweka viti maalum ni jambo kama la upendeleo linaloonyesha kuwa wanawake hatuwezi bila kushikwa mkono wakati tunaweza,” anaeleza Gladness Geogratias (33).

Gladness ambaye ni mwajiriwa katika Benki ya Serikali ya NMB, anaamini katika kuwakomboa na kuwainua wanawake kwenye ngazi za kiuchumi na kisiasa kwa kushika nafasi za juu.

Anasema wanawake ni watu ambao wametawaliwa na woga na kutojiamini hali ambayo inawafanya wengi kushindwa kuchukua hatua na maamuzi wakihofia wataonekanaje mbele ya wanaofahamu.

Gadness anasema, kuwaandalia wanawake viti maalum au nafasi za upendeleo siyo njia pekee ya kuwafanya wapige hatua bali kwa kuwapa elimu na kuwaonyesha njia.

“Naamini mwanamke anaweza lakini hajiamini na kama atapewa moyo na wanaomzunguka ni wazi anaweza kufanya mambo makubwa. Naumizwa sana na tabia ya kututenga na kutufanya kama wahitaji badala ya kufanywa kama watu tunaoweza kufanya mambo makubwa,” anasisitiza.

Gladness ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Biashara na Fedha za Kigeni wa Benki ya NMB, pia anaamini kuwa, mwanamke kumsaidia mwanamke mwenzake ni kupiga hatua zaidi ya kimafanikio.

“Siamini katika kutokusaidiana wanawake kwa wanawake, naamini wanawake tukishikana mkono tunaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo,” anasema.

Licha ya kushika nafasi hiyo ya juu kwenye benki, amejitolea kuanzisha jukwaa la kuwawezesha wanawake wenzake kuinuka na kushika nafasi kubwa zaidi kwenye maofisi na ndani ya jamii.

Anasema jukwaa hilo, limekuwa kichocheo kikubwa cha kuwashawishi wanawake kuwa na uthubutu wa kufanya mambo makubwa na kushika nafasi za juu.

“Tunaamini kila mwanamke aliyefanikiwa alijifunza au kuiga waliofanikiwa ambao wanaweza kuwa mwalimu, mzazi au kiongozi wake,” anasema.

Nini kifanyike kuwainua wanawake

Gladness anasema anaamini kuwa, mwanamke ni mtu anayehitaji kushauri na kutiwa moyo ili kufikia hatua fulani.

Anasema mara nyingi ni waoga hivyo, serikali na viongozi wanaowazunguka wanatakiwa kuwashauri na kuwatia moyo juu ya jambo wanalotaka kufanya.

“Mwanamke bila kushikizwa kuwa anaweza hakika anarudi nyuma kwa sababu ndivyo tulivyoumbwa hivyo kinachotakiwa ni kushikwa mkono na kutiwa moyo,” anasema.

Anasema mfano yeye katika kufikia malengo yake alitiwa moyo na mwalimu wake, ambaye alimuamini na kumshawishi asome masomo ambayo yeye alikuwa hajiamini nayo.

“Lakini alikazana kuniambia wewe soma tu… nakuamini, nakufahamu utaweza, acha woga, na kweli nilisoma kwa sababu ya mwalimu lakini nilifanikiwa,” anasema.

Anaeleza kuwa, watu wenye jukumu hilo ndani ya jamii zaidi ya walimu ni mume, baba au bosi.

Anasema kionyesha kuwa anaumizwa na nafasi za wanawake kupewa, akiwa katika benki hiyo, alianzisha jukwaa la kuwahamaisha wanawake kutamani nafasi za juu.

“Wanawake ni wengi sana lakini kwenye nafasi za juu tuko wachache na hata bungeni tumebewa viti maalum, hivyo tunaangalia nini cha kufanya wanawake wengine waweze kufika walikofika,” anasema.

Anasema wanachofanya ni kuwaelimisha wanawake ambao wanafanyakazi katiba benki hiyo na walioko nje ya benki namna ya kupiga hatua na kufikia nafasi za juu.

Gladness anasema kwa wanawake wa ndani wanawasaidia wasiondoke kazini kutokana na mazingira yanayowakabili kama uzazi, mazingira na majukumu ya familia.

“Licha ya kuwa anakabiliwa na majukumu makubwa ya kazi, nina hakikisha familia yangu inatambua nafasi yangu kama mama, wajue kama ninapika isipokuwa wakati mwingine nashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya majukumu,”anasema.

Anasema kama kiongozi mwenye majukumu mazito ya kazi na mama wa familia anahakikisha anamaliza majukumu ya kazi kila siku kabla ya kurudi nyumbani.

Anasema anapomaliza kazi zake za ofisi ndipo anarudi nyumbani na kwamba wakati huo anahakikisha anatekeleza majukumu ya familia pekee.

Gladness anasema kiu yake ni kuona wanawake wanashika nafasi za juu za uongozi na kufika zaidi ya alipofika yeye.

Kadhalika anaamini katika kuongeza elimu kama njia sahihi ya kumfanya mwanamke azidi kupanda na kushika nafasi za juu.

Wanawake tunatakiwa tusiridhike na nafasi tulizoshikilia bali tujitahidi kuongeza elimu tunapopata nafasi ili kuongeza fursa ya kupanda zaidi na kushikilia nafasi za juu.

Gladness pia anaamini katika kufanya kazi kwa bidiii kutasaidia kuwakomboa wanawake licha ya kuwapo kwa changamoto za kijinsia.

“Naamini katika kufanya kazi bila kuangalia changamoto zinazotuzunguka kama za kimahusiano ofisini,” anasema.

Anaeleza zaidi kuwa, haoni faida ya mwanamke kubebwa au kupewa nafasi za juu bila kuwa na sifa kama ni jambo linalozidi kuwashusha wanawake wengine.

Anasema endapo mwanamke kama huyo atawezeshwa bila kuwa sifa inamaana aliyempa nafasi akiwa hayupo hawezi kusimama yeye kama yeye.

Namna ya kuwapata wabunge Viti Maalum

Uteuzi wa wabunge wanawake wa viti maalum, umeelekezwa katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, ibara ya 78, kifungu cha 86A cha sheria ya Taifa ya uchaguzi na sura ya 343 .

Kwa mujibu wa taratibu hizo, kila chama cha siasa kilichoshiriki katika uchaguzi mkuu ambacho kimepata angalau asilimia 5 ya kura zote halali za ubunge zilizopigwa, kitapendekeza kwa NEC majina ya wanawake kwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa wabunge.

Vile vile kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 endapo itajitokeza kuwa katika jimbo la uchaguzi, mgombea wa chama amepita bila kupingwa, idadi ya kura halali za Urais wa chama cha mgombea huyo kama chama husika kimeweka mgombea, ndizo zitatumika katika zoezi hilo la kupata uwiano.

Endapo itatokea kuwa Chama husika hakikusimamisha mgombea urais, asilimia hamsini na moja (51%) ya kura za watu wote waliojiandikisha kupiga kura katika jimbo hilo zitatumika kwa madhumuni hayo ya kutafuta uwiano.

Viti Maalum Madiwani

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Tawala za Wilaya) Sura ya 237, na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Tawala za Miji) sura ya 288, zinaeleza kuwa kutakuwa na madiwani wanawake wa Viti Maalum wasiopungua theluthi moja ya madiwani wa kuchaguliwa kwenye kata pamoja na mbunge wa jimbo lililo kwenye Halmashauri husika.

Habari Kubwa