Vituo vya mafuta vyenye masharti nafuu mwarobaini wa kupunguza maafa

07Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Vituo vya mafuta vyenye masharti nafuu mwarobaini wa kupunguza maafa

Ni uamuzi wa Ewura baada ya kubaini kushamiri kwa biashara holela ya mafuta baada ya ongezeko la bodaboda, pia kupunguza uchakachuaji…

Bodaboda zikisubiri wateja. Ongezeko la usafiri wa bodaboda umesababisha kushamiri kwa biashara holela ya mafuta.

MATUMIZI ya nishati ya petroli kwa maana ya mafuta ya petroli, dizeli na yale ya taa, yamekuwa yakiongezeka nchini kutokana na mahitaji ya bidhaa hizo kwa shughuli za kila siku.

Miongoni mwa kazi za mafuta hayo ni pamoja na uendeshaji wa vyombo vya usafiri kama vile magari na pikipiki na mitambo ya viwandani kama mashine za kusaga na kuchomelea.

Katika siku za hivi karibuni, mathalan, maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwamo wimbi la ongezeko la viwanda, yamesababisha pia matumizi makubwa ya mafuta hayo kwa ajili ya shughuli za kila siku.

Suala la uchukuzi na usafirishaji wa bidhaa na abiria, limesababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini na nchi zinazoendelea kwa ujumla.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, vyombo vya usafiri kama vile magari na pikipiki maarufu kama bodaboda zinazotumika kama usafiri wa haraka kwa watu wengi vinatumia mafuta kila kukicha.

Vyombo hivyo si kwamba vinatumika sana maeneo ya mijini pekee bali pia vijijini ambako usafiri wa magari na pikipiki umeshamiri. Sambamba na umuhimu huo wa usafiri, pia hatua hiyo imesababisha ongezeko la ajira miongoni mwa vijana pamoja na wamiliki wa vyombo hivyo ambavyo huwakodisha madereva.

Kama wahenga wasemavyo kufa kufaana, ongezeko la vyombo vya usafiri na mitambo kama vile mashine hadi vijijini, limesababisha kuibuka kwa biashara ya mafuta ya hasa petroli na dizeli kushamiri.

Kwa maneno mengine watu wameibua fursa kupitia biashara hiyo ambayo imetokana na kuwapo kwa vyombo vya usafiri ambavyo vimekuwa msaada mkubwa miongoni mwa wananchi. Vyombo hivyo vimekuwa vikiwasafirisha watu kutoka sehemu moja hadi nyingine na kuwa ndio usafiri wa uhakika mpaka vijijini.

Hata hivyo, biashara ya mafuta hasa petroli na dizeli katika maeneo ya vijijini imekuwa ikifanyika katika maeneo yasiyo salama kutokana na wahusika kwenda katika vituo vya mafuta na kununua bidhaa hiyo katika madumu kisha kuisafirisha hadi vijijini na kuhifadhi katika nyumba za makazi au maduka.

Maeneo hayo si salama kwa sababu yanaweza kusababisha milipuko na kuleta maafa kwa watu wanaoishi katika nyumba husika au mali zilizomo katika maduka.

Matukio kama hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara na hata kusababisha watu kupoteza maisha. Yote hiyo ni kwa sababu ya uhifadhi usio rafiki kwa afya na maisha ya wanadamu.

Miongoni mwa matukio kama hayo yamekuwa yakiripotiwa katika vyombo vya habari kutokana na baadhi ya watu kutunza mafuta ndani ya makazi au kuachia watu kuvuta sigara au kuwa na moto karibu na yalipo mafuta.

Mojawapo ni la watu watatu kupoteza maisha wilayani Tarime, Gabriel Itembe (36) alipolipukiwa mafuta wakati akimpimia mafuta mteja wake huku akiwasha kibatari.

Maafa hayo huenda kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na ukosefu wa elimu kwa umma juu ya matumizi na athari za mafuta ya petroli.

HATUA YA EWURA
Hali hiyo imesababisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kupitia kanda zake kuanza kutoa mafunzo kwa wadau wakiwamo wauzaji na watumiaji wa mafuta ya dizeli na petroli.

Mamlaka hiyo ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 imepewa jukumu la kudhibiti sekta ndogo ya mafuta kiutaalamu, kiusalama na kiuchumi, imeamua kufanya hivyo baada ya kubaini kuwa ufanyaji biashara huo pamoja na matumizi yayisodhibitiwa vinaweza kusababisha maafa makubwa.

Ewura pamoja na mambo mengine, imebaini kwamba sehemu nyingi za vijijini ambako biashara holela ya mafuta imeshamiri, hazina matangi au vituo vya kuuzia bidhaa hiyo.

Kwa kawaida, mfanyabiashara ya mafuta anapaswa kuwa na kituo ambacho wanunuzi watafika na kununua bidhaa kwa matumizi mbalimbali, jambo ambalo kwa aeneo ya vijijini ni nadra kukuta kituo cha mafuta au tangi la kuhifadhia petroli.

Katika kufanya hivyo, Ewura imeanzisha mfumo wa ujenzi wa vituo vya mafuta nyenye masharti nafuu kwenye maeneo ya vijijini ili kukabiliana na biashara ya kuuza mafuta kwenye vifaa visivyoruhusiwa kisheria.
 
Katika semina iliyofanyika hivi karibuni mjini Singida, Meneja mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema changamoto ya baadhi ya wananchi kuuza mafuta ya petroli kwenye vifaa visivyo rasmi, inatokana na uingizwaji wa vyombo vya usafiri aina ya pikipiki unaotumia mafuta kidogo kwa muda wa siku nzima.
 
“Hiyo ni changamoto ambayo imekua kutokana na kukua kwa uchumi kwa ujumla wake kwamba zimeingia pikipiki nyingi ambazo zinatumia mafuta kidogo na watu hawawezi kuwekeza kwa kujenga kituo kikubwa ukawa unauza lita 50. Kwa hiyo unakuta lita moja ya petroli unaweza kutumia kwenye pikipiki kwa siku nzima,” alisema Kaguo.
 
Baada ya kubaini madhara yatakayotokana na uuzaji holela wa mafuta kwenye vifaa visivyo rasmi, alisema mamlaka imekuja na mfumo mpya wa ujenzi wa vituo vyenye masharti nafuu kwenye maeneo ya vijijini.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuondokana na biashara ya mafuta, hususan kwenye nyumba za makazi jambo ambalo ni hatari.
 
“Napenda tu kuwafahamisha kwamba wanafanya biashara hatarishi si tu kwa taifa bali hata kwa maisha yao,” alisema.

HALI HALISI
Meneja wa Ewura Kanda ya Kati, Norbert Kyoza, alibainisha kwamba, bado kuna matatizo kwenye biashara ya mafuta na kwamba endapo wataacha kila mmoja akafanya anavyotaka, madhara yatakuja kwa wote.
 
“Anaanza mmoja kwa kufukuzia kafaida anakokapata lakini kama tunavyojua biashara faida huwa ni tamu na atakaponogewa ataanza kuchanganya na mafuta, maji unawasha unapata madhara kutokana  na kuuza mafuta yasiyo na kiwango,” alisema.
 
Hatua ya Ewura kutoa masharti nafuu kwa ujenzi wa vituo vya mafuta maeneo ya vijijini ni suluhisho kwa usalama wa wananchi na mali zao kwa sababu kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri, hasa pikipiki, madhara yangekuwa makubwa zaidi.

Jambo lingine ni kwamba uuzwaji holela wa mafuta kupitia vidumu na vioski ulikuwa wakati mwingine ukisababisha kutokuwapo udhibiti wa biashara hiyo na matokeo yake baadhi ya wauzaji kuchanganya ama petroli na mafuta mengine kwa tamaa ya kujipatia fedha.

Lakini kwa uamuzi wa mamlaka wa kuanzisha mfumo wa ujenzi wa vituo vyenye masharti nafuu vijijini, ni mpango mzuri ambao si tu utasaidia usalama wa watu na mali zao dhidi ya majanga bali hata uuzaji wa bidhaa zinazokidhi viwango.

Habari Kubwa