Vyuo uchwara vimo ,vinachochea kuzalisha madereva mbumbumbu

03Sep 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Vyuo uchwara vimo ,vinachochea kuzalisha madereva mbumbumbu

TANZANIA inatishiwa na vifo vinavyotokana na na ajali za barabarani ambavyo ni matokeo ya ulevi, uchovu na mafunzo duni yanayotolewa kwa madereva na vyuo uchwara.

Elimu hiyo isiyo na viwango hutolewa na baadhi ya vyuo vya udereva nchini, inapika wahitimu duni kwa tasnia hiyo, wanaoendesha kwa mwendokasi na kupuuza sheria za usalama barabarani.

Ajali pia huchangiwa na kuwapo miundombinu duni kama ufinyu wa barabara, mashimo, ukosefu wa taa, lakini pia ubabe barabarani na ulevi ni miongoni mwa vyanzo vya ajali hizo.

Duniani watu milioni 1.2 hupoteza maisha kutokana na ajali, milioni 50 hujeruhiwa kila mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya (WHO).

Kati ya vifo hivyo asilimia 90 vinatokea kwenye nchi zenye uchumi mdogo na wa kati, ikiwamo Afrika ambako kuna idadi ndogo ya vyombo vya moto barabarani ikilinganishwa na mataifa yaliyoendelea.

Mjumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Henry Bantu, anasema akiwasilisha mada kwenye semina kwa wanahabari iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kuhusu usalama barabarani, matumizi ya barabara sababu za ajali na njia za kuziepuka.

Anawaambia washiriki kuwa asilimia 76 ya ajali zitokeazo nchini zinasababishwa na makosa ya madereva na watu.
Anasema kati ya hizo asilimia 62 zinasababishwa na tabia, dhana, mazoea na maadili yasiyofaa kwa baadhi ya madereva.

Anaeleza kwamba ulevi, uchovu, mafunzo duni kwa baadhi ya vyuo vya udereva, mwendokasi, kupuuza sheria za usalama barabrani, miundombinu duni na ubabe barabarani ni miongoni mwa vyanzo.

Anaongeza kuwa yote hayo yanachangia ajali kutokea na kuathiri zaidi kundi kubwa la watuamiaji barabara ambao ni watembea kwa miguu.

“ Ukiwa barabarani ni kupanga, kuamua, kuangalia kabla ya kufanya maamuzi kwa kuwa ni eneo hatari ambalo linaweza kusababisha ajali. Hakuna ajali ambayo inaathari kubwa ambayo haikutarajiwa kuliko zile zinazotarajiwa,” anasema Bantu.

AINA YA AJALI
Zipo aina mbili za ajali zinazoweza kutokea ambazo zimesababishwa na dereva ambaye hakuwa makini na elimu kuhusu vifaa vya magari na tahadhari za kuchukua kabla ya kuanza safari.

Bantu anasema ajali zitokeazo zinaweza kuwa ni matokeo ya kupuuzwa kwa sheria na kanuni za usalama barabani (crash) pia ambazo zimetokana na masuala ya kiufundi zinazoitwa ‘accidents’.

Aidha, ajali hizo zinatofauti kwa kuwa zilizotokana na kupuuzwa sheria za usalama barabarani, kama vile dereva kufahamu palipowekwa kibao cha kuendesha kwa kasi ya kilometa 50 kwa saa akaendesha kwa kasi 120 kwa saa ajali ikitokea amejitakia.

Anasema vilevile dereva anayepuuza alama na ishara za barabarani kama vibao vinavyoonyesha kona, mteremko mkali, mlima, kivuko cha wanaotembea , cha mifugo, wanafunzi , maegesho, barabara kuu huyo atarajie ajali wakati wowote.

Bantu anaeleza kuwa ajali ambazo zinatokea kutokana na masuala ya kiufundi, kama vile gari ambayo ilipelekwa gereji kabla ya safari na kukaguliwa matairi na injini lakini fundi akasahau kuweka baadhi ya vifaa vya gari sawa sawa, itakuwa ni ajali ambayo imetokana na uzembe wa kiufundi.

“Mfano dereva kwa uzembe wake akasahau kufunga tairi sawasawa ajali ikitokea hii ni ‘accident’, lakini umeendesha safari ndefu kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam bila kupumzika, ukanywa vilevi ajali ikitoke hii ni ‘crash’.Ndizo ajali nyingi zinazotokea barani Afrika, ikiwamo Tanzania,” anasema Bantu.

VIFO VYA WANAOTEMBEA
Katika ajali zinazosababisha vifo ambazo zinatokea nchini, waathiriwa wakubwa ni watembea kwa miguu ambao ni asilimia 31 ya watuamiaji wa barabara.

Wengine wanaopoteza maisha ni abiria kwa asilimia 28, madereva wa pikipiki za miguu miwili au mitatu hawa ni kwa asilimia 22, madereva magari na malori asilimia saba na waendesha baiskeli ni asilimia 11.

Kati ya usafiri hatari zaidi barabarani unaosababisha ajali, vifo, majeruhi, ulemavu kwa watu wengi ni bodaboda.

Bodaboda zinatumiwa na kutegemewa zaidi mijini na vijijini, kwa kipindi cha muongo mmoja hapa nchini na kuwa kati ya ajira kubwa kwa vijana.

Inakadiriwa matumizi ya usafiri huo nchini yameongezeka na kufikia bodaboda milioni 1.5 ambazo zimesajiliwa kutoa huduma hiyo, kutoka idadi ya bodaboda 308,000 iliyokuwapo mwaka 2010, kwa mujibu wa mamlaka za usimamizi wa vyombo vya moto za Mamlaka ya Mapato (TRA) na ile ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra).

Aidha, kati ya ajali ambazo zinatokea barabarani kila siku na kusababisha vifo, zinasababishwa na bodaboda kutokana na kutovaliwa kofia ngumu, kutokufahamu sheria za barabarani, ulevi kwa dereva na kukosa kofia kwa abiria.

TAARIFA ZA MUHIMBILI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu ya Hospitali ya Muhimbili (MOI), inasema majeruhi wa ajali za barabarani wanaolazwa kwenye taasisi hiyo wanatokana na kugongwa na bodaboda, huku wanaotembea wakiwa waathirika wakubwa.

Taasisi inasema kati ya majeruhi 2,223 waliolazwa MOI mwaka 2016, zaidi ya 1,100 walikuwa wanaotembea waliogongwa na bodaboda.

Afisa Uhusiano MOI, Patrick Mvungi,akitoa takwimu za majeruhi kwenye uzinduzi wa kipindi cha elimu kwa umma, kuhusu matumizi bora ya bodaboda kwa madereva na wadau, anasema nusu ya majeruhi hao wanatoka Dar es Salaam.

Hata hivyo, kuna unafuu kwani idadi ya wagonjwa inapungua, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka jana waliokuwa 2,223 kutoka 2,692 mwaka 2015.

BODA HUINGIZA BILIONI 7 KWA SIKU

Mmoja wa waendesha bodaboda kata ya Keko jijini, Charles Tumbi, anasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo vituo vya kuegesha wakati wakisubiri na kushusha abiria.

Nyingine ni kukosa fursa za mikopo na mahusiano duni kati yao na jamii pamoja na polisi.

Anasema licha ya kazi hiyo kuajiri vijana karibu milioni 1.5 nchini na usafiri huo kutegemewa na watu wengi, unakabiliwa na changmoto kubwa na kuwafanya kukimbizana na jeshi la polisi.

“Hii ni ajira kubwa, iwapo kila bodaboda anapata Sh. 5,000 kwa siku ukizidisha mara milioni 1.5 karibu bilioni 7.5 hukusanywa kila siku .

Haya ni mapato makubwa nchi nzima, serikali irasimishe shughuli hii na kuendelea kupata elimu ya usalama barabarani,” anasema Tumbi.

TAARIFA ZA POLISI
Afisa Mnadhimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Theopista Mallya, anasema madereva wa bodaboda wameendelea kuvunja sheria za usalama barabarani kwenye taa nyekundu na kutozingatia vivuko vya pundamilia.

Mallya anasema kwa siku taarifa za ajali zinazoripotiwa nchini, kati ya tano, nne zinatokana na ajali za bodaboda zinazosababisha vifo na majeruhi.

“Katika ajali hizo za bodaboda moja lazima iwe ni pikipiki imegonga mtu, imejeruhi, abiria na dereva wote wamejeruhiwa au kufa. Wengine wamegongana wao kwa wao na wakati mwingine dereva kajibamiza kwenye nguzo, ukuta na kuumia vibaya,” anasema Kamishna Mallya.

Anasema uvunjifu wa sheria umeendelea kuongezeka barabarani na madereva wa bodaboda ni wahusika wakuu. Wanaochangia ni wale wanawapakia wanafunzi na watoto wadogo walio chini ya miaka tisa, abiria kutovaa kofia ngumu, kubeba watu mawili (mishikaki) jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Habari Kubwa