Waandishi waazimia kuimarisha vita unyanyasaji wa wanawake

15Jun 2019
Gwamaka Alipipi
Aliyekuwa Kigali, Rwanda
Nipashe
Waandishi waazimia kuimarisha vita unyanyasaji wa wanawake
  • Ni katika mkutano wao jijini Kigali nchini Rwanda

VITENDO vya unyanyasaji, ukandamizaji na ukatili kwa wanawake bado vinaendelea katika jamii mbalimbali barani Afrika.

Waandishi wa habari kutoka mataifa ya Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Guinnea Bissau, Rwanda, Kenya, Ghana na Liberia wakiwa katika mkutano mjini Kigali, Rwanda wakijadili matatizo yanayowakabili watoto wa kike na wanawake Afrika. PICHA: GWAMAKA ALIPIPI

Matukio kama vile kukeketwa, kuchomwa sehemu za siri, kubakwa, kunyang’anywa mali, kurithiwa, haki ya uzazi wa mpango ni baadhi ya matukio yanayozidi kushamiri siku hadi siku miongoni mwa jamii.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na idadi ya watu (UNFPA), kati ya wanawake na watoto wa kike milioni 100 hadi 140 wanafanyiwa vitendo vya ukeketaji.

Vilevile, kati ya wanawake na watoto wa kike milioni tatu hadi nne kutoka nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Somalia na Ethiopia wanakeketwa kwa mwaka.

Aidha, zaidi ya wanawake 800 hufariki kila siku kutokana na matatizo ya utoaji mimba.

Takwimu zinabainisha kwamba takribani wanawake na wasichana milioni moja wanafariki kutokana na vitendo vya kikatili, vingi vikiwa ni matunda ya tamaduni zilizopitwa na wakati.

Madhira haya ndiyo yaliwagusa waandishi wa habari 35 kutoka mataifa nane barani Afrika kukusanyika pamoja jijini Kigali nchini Rwanda na kuzungumza kwa pamoja kuhusu kadhia hiyo, kisha kuja na kauli moja iliyoazimia kuvitokomeza vitendo hivyo.

Azimio lililotolewa ni la kuzitaka serikali za nchi za Afrika kusimama imara kumsaidia mtoto wa kike na mwanamke dhidi ya mila potofu, pamoja na kuzifanyia marekebisho sera na sheria zilizopitwa na wakati ambazo zinamkandamiza na kumgusa moja kwa moja mwanamke.

Waandishi kutoka nchi za Ghana, Rwanda, Tanzania, Liberia, Zambia, Zimbabwe, Kenya, pamoja na Guinnea Bissau walikutana kwa siku nne kumjadili mwanamke na namna ya kumkomboa.

Shirika la Haki za Wanawake barani Afrika (Femnet) ndilo lililoratibu mkutano huo likiwa na lengo moja tu ambalo ni kumweka mwanamke huru kutoka katika vitendo vinavyomnyima uhuru, kumkandamiza na vile vinavyomnyima uhuru wa kutimiza ndoto zake katika maisha.

Wakizungumza kwenye mkutano huo, waandishi hao walieleza namna baadhi ya sheria zilizopo nchini mwao, zinavyochangia moja kwa moja kumkandamiza mwanamke.

Sally Chiwama, mwandishi mwandamizi aliyebobea katika kuhabarisha habari za haki za wanawake nchini Zambia anasema nchini kwake, serikali bado haijajitoa kwa asilimia 100 kupambana na mila na tamaduni potofu dhidi ya mwanamke.

Anasema vitendo kama ukeketaji, ndoa za utotoni, mjane kurithiwa bado vinaendelea katika baadhi ya jamii, huku serikali ikifumbia macho.

“Ni aibu kubwa japokuwa tuna sera na sheria barani Afrika, lakini bado matatizo yanaendelea… japokuwa waandishi wa habari tunaripoti na kuandika matukio haya, lakini bado serikali zetu hazitaki kufanya mapitio upya ya sheria hizo,” anasema Chiwama.

Kwa upande wake Gloria Tamba ambaye ni mwandishi kutoka Liberia anasema nchini kwake ongezeko la vifo vya wanawake na watoto wa kike kutokana na vitendo vya ukatili linaendelea, lakini serikali inaangalia tu bila ya kuchukua hatua madhubuti.

Anasema licha ya waandishi wa habari kuandika mara kadhaa habari zinazohusu vifo vya wanawake na watoto wa kike, lakini bado serikali haijachukua hatua yoyote ya kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa.

“Watoto wa kike na wanawake bado wanakufa kwa matukio yanayoweza kudhibitiwa, lakini serikali ipo na inaangalia tu bila kuchukua tahadhari yoyote ya kupambana navyo…sisi kama waandishi wa habari tusichoke kuandika na kuripoti matukio hayo,” anasema Tamba.

MKURUGENZI

Mkurugenzi Mtendaji wa Femnet, Memory Kachambwa, akitoa neno kwa waandishi hao wa habari anavitaka vyombo vya habari barani Afrika kuhakikisha vinahimiza serikali zao kupambana ili kuhakikisha idadi ya vifo vya wanawake na watoto vinatokomezwa.

“Ninajua kwenye kila nchi barani Afrika kuna sera na sheria zinazomlinda mwanamke na mtoto wa kike, lakini utekelezaji wake ni sifuri, na hii ndiyo maana serikali za Afrika zinatakiwa kuchukua hatua zaidi… haitoshi kuwa na maazimio kwenye karatasi peke yake bali utekelezaji ni muhimu,” anasema.

Anasema kati ya nchi 20 duniani zenye idadi kubwa ya vitendo vya ndoa za utotoni, 15 zipo Afrika.

Anabainisha kwamba inakadiriwa kila siku watoto wa kike 37,000 chini ya miaka 18 wanalazimishwa kuolewa, jambo ambalo linasababisha kukatishwa masomo yao na hivyo ongezeko la umaskini.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyu, inakadiriwa ifikapo mwaka 2050, matukio ya ndoa za utotoni barani Afrika yatafikia milioni 310 kulingana na ukuaji wa idadi ya watu.

Aidha, anasema vitendo vya vitisho kwa watoto wa kike na wanawake bado vinaongezeka katika nchi nyingi barani Afrika, Kenya ikiwa ni mojawapo ya mfano.

“Kesi za ubakaji wa watoto wa kike na wanawake nchini Kenya zinakadiriwa kufikia 40,000 kwa mwaka, na zinazoripotiwa ni 4,000 tu,” anasema.

Merceline Nyambala ni mwandishi wa habari kutoka Kenya ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Kenya (AMWIK).

Nyambala anabainisha kwamba  kunahitajika umoja wa hali ya juu miongoni mwa waandishi wanawake Afrika kuhakikisha wanawake na watoto wa kike wanapewa nafasi katika kueleza matatizo wanayokumbana nayo.

“Tumeshaona madhara yanayotokea kwa watoto wa kike na wanawake katika nchi zetu, sasa ni wakati wetu wa kuhakikisha serikali inakuwa sehemu ya mapambano ya kumkomboa mtoto wa kike,” anasema.

Anafafanua kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuripoti na kuandika mara kwa mara habari zinazohusu jinsia, kwani zitasaidia kuleta mabadiliko katika jamii.

Kadhalika, anavitaka vyombo vya habari hususani redio na televisheni kuzipa muda mwingi mada za jinsia, huku vyombo vya magazeti zikiandika makala nyingi zinazohusu wanawake.

“Wanawake wengi wanafariki kwa sababu ya unyanyasaji wa kijinsia, wakati wa kujifungua, pamoja na tamaduni zilizopitwa na wakati… ni jukumu letu kukemea kupitia kalamu zetu, kila serikali barani Afrika inapaswa kusimama na kukemea,” anasema Nyambala.

Anabainisha kuwa ni kipindi kirefu sasa utu wa mwanamke na mtoto wa kike umekuwa hauthaminiwi, na kwamba sasa hali imekuwa mbaya zaidi kuliko kipindi cha wakoloni.

Habari Kubwa