Wababe wa 8 Mapinduzi Cup

16Jan 2017
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wababe wa 8 Mapinduzi Cup

AZAM FC ndiyo mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Simba bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar na kuifikia rekodi ya Simba ya kulitwaa mara tatu.

Azam imeingia fainali mara tatu na zote imelichukua. Kwa upande wa Simba, ilikuwa ni fainali yao ya tano, ikichukua mara tatu na mara mbili kulikosa.

Tangu michuano hiyo ianzishwe mwaka 2004, ni timu nane ambazo zimechukua kombe hilo.

1. Yanga (2004)
Timu ya Yanga ilitwaa Kombe la Mapinduzi mwaka 2004 kwa kuichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1. Awali, kwenye mechi za nusu fainali, Yanga iliichapa Taifa Jang'ombe mabao 3-0, Mtibwa ikaifunga Miembeni bao 1-0 lililofungwa na Shaaban Nditi.

Januari 12, Yanga ilibeba kombe hilo kwa mabao yaliyofungwa na Salum Swedi na Gulla Joshua, Abubakar Mkangwa akiifungia Mtibwa bao la kufutia machozi.

2. JKU (2005)
Timu ya JKU ya Zanzibar ilitwaa Kombe la Mapinduzi mwaka 2005 kwa kuichapa Mafunzo mabao 2-0, yaliyofungwa na Said Yusuph na Seif Khamisi.

3. Malindi-2007
Kombe hilo lilichezwa tena mwaka 2007 na timu ya Malindi kulitwaa. Miembeni, ilifanikiwa kuingia fainali, baada ya kuichapa Yanga bao 1-0 kwenye mechi ya nusu fainali, lakini ilijikuta ikiangukia pua mbele ya Malindi kwa kuchapwa mabao 2-0.

Mabao ya mabingwa, yote mawili yalifungwa na Hassan Seif.

4. Simba-2008
Ilitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 2008, ilipoichapa Mtibwa Sugar kwenye mechi ya fainali kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.

5. Mtibwa Sugar-2010
Kombe hilo lilichezwa tena 2010, Yanga ikitolewa mapema kwenye hatua ya makundi. Ulikuwa ni mwaka wa Mtibwa Sugar kutwaa kombe hilo, baada ya kuichapa Ocean View kwa bao 1-0, mechi ya fainali. Kwenye mechi ya nusu fainali, Mtibwa iliichakaza Simba mabao 3-0 yaliyofungwa na Dickson Daudi aliyefunga mawili na Said Mkopi moja.

Zuberi Katwila alifunga bao pekee kwenye mechi ya fainali.

6. Simba-2011
Wekundu wa Msimbazi Simba walichukua Kombe la Mapinduzi mwaka 2011 kwa kishindo wakiwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga mabao 2-0 kwenye mechi ya fainali. Kabla ya mechi hiyo, Simba iliifunga Ocean View mabao 2-1 kwenye nusu fainali, mabao ya Emmanuel Okwi na Hillary Echesa, huku Saad Ramadhani akifunga bao la kufitia machozi kwa timu yake.

Yanga ilitinga fainali kwa kuichapa Mtibwa mabao 2-1, yaliyofungwa na Kigi Makasi na Davis Mwape, huku Yusuph Nguya akifunga bao la kufutia machozi.

Mabao ya Simba kwenye mechi ya fainali yalifungwa na Patrick Ochan dakika ya 33 na Shija Mkina dakika ya 72.

7. Azam FC-2012
Timu ya Azam FC, ilifanikiwa kutwaa kombe hilo mwaka 2012.

Ilikuwa tishio msimu huo, ilipoanza kuichapa Yanga mabao 3-0, mawili ya Kipre Tchetche na moja la John Bocco na kuifanya itangulie kurudi Bara.

Kwenye mechi ya nusu fainali, Azam iliichapa Simba mabao 2-0, Kipre na Bocco wakifunga tena, na fainali ikaichapa Jamhuri mabao 3-1.

Bocco, Mrisho Ngasa waliifungia Azam, na la kujifunga la Mrisho Ahmed, huku Ally Mmanga akifunga bao la kufutia machozi.

8. Azam FC-2013
Kwa mara nyingine tena, Azam FC ilitwaa tena Kombe la Mapinduzi kwa mara ya pili mfululizo.

Mechi ya nusu fainali, iliifunga Simba kwa mikwaju 5-4 ya penalti, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.

Iliifunga Tusker ya Kenya mabao 2-1 fainali, Jockins Atudo na Gaudence.

Mwaikimba wakiifungia mabao Azam, huku Jesse Werre, straika anayetisha kwa sasa nchini Zambia akiwa na Zesco akiifungia timu yake bao la kufitia machozi.

9. KCC-2014
Timu ya KCC ya Uganda ilifanikiwa kuliondoa kombe hilo kwenye ardhi ya Tanzania, ilipoifunga Simba kwenye mechi ya fainali. KCC ilifika fainali baada ya kuchapa Azam mabao 3-2, Simba ikaichapa URA mabao 2-0 nusu fainali.
Simba ililala fainali bao 1-0 lililofungwa na Herman Waswa.

10. Simba 2015
Ni michuano inayokumbukwa na wengi, hasa mashabiki wa Simba, kwani mbali na kutwaa ubingwa, iliwatengeneza wachezaji wengi wa kikosi cha pili na kuwa tegemeo kikosi cha kwanza.

Wachezaji nao ni Manyika Peter, Ibrahim Ajibu na Hassan Isihaka. Simba ilichukua kombe kwa kuitoa Mtibwa kwa mikwaju 4-3 ya penalti, baada ya kutoka sare ya bila kufungana.

11. URA-2016
Mwaka jana URA ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 3-1 kwenye mechi ya fainali.
Simba na Yanga zote zilitolewa hatua ya nusu fainali. Wakati Simba ikichapwa bao 1-0, la Ibrahim Jeba, Yanga ilitolewa na URA kwa mikwaju ya penalti 4-3.

12. Azam-2017
Bao la dakika ya 12 la Himid Mao, aliyeachia shuti kali lililokwenda moja kwa moja hadi wavuni, liliifanya Azam kutwaa kombe hilo kwa mara ya tatu kwenye fainali hizo za 12, huku timu nane tu zikibahatika kuchukua ubingwa huo.